loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Iddi Simba kuzikwa leo Magomeni

ALIYEKUWA Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa na mbunge wa Ilala Iddi Simba, amefariki na atazikwa leo kwenye makaburi ya Mwinyi Mkuu Magomeni jijini Dar es Salaam baada ya Swala ya Ijumaa.

Msemaji wa Familia, ambaye ni mdogo wa Marehemu, Ahmad Simba, alisema marehemu ataswaliwa Msikiti wa Manyema uliopo Kariakoo Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Ahmad, Simba alikuwa akisumbuliwa maradhi mbalimbali kwa muda wa miaka mitatu, ikiwemo shinikizo la damu, tezi dume na tatizo katika utumbo mkubwa.

Katika kipindi hicho alifanyiwa upasuaji nchini India na hapa nchini. Hadi anaaga dunia jana saa 5:00 asubuhi, alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na alikuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI). Wasifu wa Iddi Simba Simba alizaliwa Oktoba 8 mwaka 1935 na aliingia kwenye siasa mwaka 1993.

Baadaye alichaguliwa kuwa Mbunge wa Ilala kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Alipata elimu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo Chuo Kikuu cha Punjab, Pakistani na Chuo Kikuu cha Toulouse nchini Ufaransa.

Simba aliwahi kuwa mkurugenzi katika benki mbalimbali za kimataifa ikiwamo Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki mwaka 1968-1978. Mwaka 1978-1980, Simba alikuwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika jijini Abijan, Ivory Coast. Pia Simba aliwahi kufanya kazi Benki ya Dunia nchini Marekani na Redio Tanzania.

Hapa nchini, Simba aliwahi kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango katika Wizara ya Uchumi na Mipango na Waziri wa Viwanda na Biashara “Mzee Simba aliishi maisha ya kawaida na alikuwa mtu wa dini sana. Alipenda ndugu zake na watu wengine. Daima alitusisitiza wanafamilia tuishi kwa upendo,”alisema Ahmad.

Kutokana na kushika imani yake ya dini vizuri, aliteuliwa kuwa Mshauri wa Mambo ya Dini katika Msikiti wa Mtoro na Msikiti wa Manyema. Marehemu ameacha mke, Khadija Simba na watoto wanne, ambapo wa kiume ni mmoja na watatu wakike watatu, akiwemo mwanahabari maarufu, Sauda Simba.

Pia ameacha wajukuu sita. Wakati huo huo, aliyewahi kuwa Mkuu wa mikoa ya Mara, Kagera na Mtwara na aliyebuni jina la Azimio la Arusha, Kanali Nsa Kaisi amefariki dunia jana. Watu mbalimbali waliotuma taarifa mtandaoni jana, akiwemo Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Mark Mwandosya, walieleza kuwa wamepokea taarifa ya kifo hicho kwa majonzi makubwa.

Kwa mujibu wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwenye kitabu chake cha My Life My Purpose alichokizindua mwaka jana, Kaisi ndiye aliyetoa jina la Azimio la Arusha.

Katika kitabu hicho, Mkapa alieleza jinsi Kaisi alivyotoa jina hilo la Azimio la Arusha, kwamba katika gazeti la The Nationalist walikuwa wakilitumia neno ‘Arusha Declaration’ (Azimio la Arusha), ndipo Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere akalipenda na kulitumia kwenye maamuzi, yaliyofikiwa Arusha, ya tamko rasmi la kisiasa lilikosudiwa kuongoza Tanzania katika njia ya ujamaa.

Kaisi aliwahi kuwa mwandishi wa habari mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na The Nationalist. Pia aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na Mshauri wa Masuala ya Siasa wa Rais Mkapa. Alifariki usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa akitibiwa. Msiba upo nyumbani kwake Oysterbay na utaagwa kesho Jumamosi na kusafirishwa kwenda Mbeya kwa mazishi.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments