loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rugemalira aomba orodha waliopokea mgao Escrow

MFANYABIASHARA maarufu nchini, James Rugemalira ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa amemuandikia barua Gavana wa Benki Kuu (BoT), akimuomba amuorodheshee watu wote, waliopokea fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ili ajisafi she.

Aidha, alidai ameandika notisi kwa taasisi tisa za serikali ikiwemo Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga akiomba mahakama hiyo, imuondoe katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.

Taasisi nyingine zilizoandikiwa notisi hiyo ni Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Diwani Athumani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Gavana wa BoT, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamishna wa Magereza, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Clement Mashamba na Msajili wa Mahakama, ambapo alidai taasisi zote zimepokea taarifa hiyo.

Rugemalira alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa. Mshitakiwa huyo wa pili, alinyoosha mkono na kuieleza mahakama kuwa aliandika barua kwenda BoT akisema yeye hajapatiwa hata senti moja kutoka kwenye akaunti ya Escrow na kwamba fedha alizopewa yeye ni zile zilizotolewa kwa amri ya mahakama kwa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP).

“Nimemuomba Gavana kuorodhesha watu wote waliopokea fedha kutoka akaunti ya Escrow ili nijisafishe kwa sababu sikupokea hata senti moja. Majibu ya Gavana aliniambia atatoa orodha hiyo mpaka pale atakapopata amri halali ya mahakama ya kufanya hivyo,”alidai Rugemalira.

Awali, Rugemalira alidai alileta maombi mahakamani hapo kwamba aliandika barua kwenda kwa Kamishna wa TRA, akieleza namna Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong walivyokua wakikwepa kodi na ushuru wa forodha wa Sh bilioni 1.5. Alidai ameandika barua ya nyongeza na kuikabidhi Takukuru ili watakapotoa majibu watoe kwa usahihi.

“Februari 11 mwaka huu nilitoa notisi inayoelezea matatizo hata yalivyokuwa na kwamba kuna vipengele vya sheria havitekelezwi. Katika notisi hii nimeeleza ikiwa hawataniondoa kwenye kesi hii, hawataweza kukamilisha upelelezi na filimbi nilizopiga, zitasaidia kukamata wezi,” alidai.

Mshitakiwa huyo aliomba kukutana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kabla ya kwenda mahabusu kwa ajili ya kumpa ufafanuzi kuhusu kesi hiyo.

Kwamba kama hawatamtoa katika kesi hiyo, ataleta maombi maalum ya kutaka kuondolewa kwenye kesi hiyo. Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, mwaka huu kwa kutajwa.

Mbali na Rugemalira, washitakiwa wengine ni Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power (IPTL) na Mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments