loader
Picha

PAC ilivyoyashukia mashirika ya umma pasua kichwa

SERIKALI imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu zaidi mashirika na taasisi zake za umma katika kuhakikisha zinafuata taratibu zilizowekwa kwenye uendeshaji wake, ikiwa ni pamoja na kusaidia vita dhidi ya ufi sadi.

Mbali ya serikali yenyewe kufuatilia, Bunge pia kupitia kamati zake za kudumu zinafuatilia kwa karibu uendeshaji wa mashirika na taasisi za umma na mojawapo ni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Baada ya kamati huu kufuatilia huwasilisha bungeni taarifa za kazi zake na wabunge kujadili na kupitisha maazimio. Kwa mwaka jana, imezifuatilia hesabu za mashirika mengi na miongoni mwake ambayo madudu yao yamewekwa hadharani ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). PAC imetaka shirika hili lichunguzwe pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Hali kadhalika wabunge wanaeleza ulegevu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na jinsi Shirika la Madini la Taifa (Stamico) lilivyokuwa hoi ingawa Waziri wake wa Madini, Dotto Biteko anabainisha jinsi sasa shirika hilo linavyojitahidi kutoka ICU. NSSF imeonekana kutofuata taratibu ambapo Bunge limeazimia serikali kulichukulia hatua kwa kitendo cha kufanya uwekezaji kwenye hisa za Kampuni ya Simu ya Vodacom licha ya Benki Kuu (BoT) kutoipa kibali na kusababisha shirika hilo kutopata mapato stahiki.

Azimio hilo limetokana na ushauri uliotolewa na PAC katika taarifa ya shughuli zake za mwaka 2019 iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka bungeni.

“Uchambuzi wa Kamati katika Taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) ulibaini kuwa uwekezaji wa NSSF katika hisa za Vodacom haukuzingatia mwongozo wa uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na uwekezaji huo unatoa riba ndogo kuliko riba inayotolewa na dhamana za serikali hivyo kuikosesha NSSF mapato stahiki. Ni kwa mantiki hiyo serikali inatakiwa ifanye uchunguzi wa kina wa suala hili na kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi,” anasema Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Naghenjwa Kaboyoka Mwongozo wa uwekezaji katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii unaelekeza kwamba, mifuko iwekeze katika maeneo ambayo faida zake ni kubwa kuliko hati fungani (Dhamana) za serikali. Aidha, kwa maeneo ambayo faida yake ni ndogo kuliko dhamana za serikali, Mfuko husika utatakiwa kupata idhini ya BoT kabla ya kuwekeza katika maeneo hayo.

Mwenyekiti huyo anasema taarifa ya CAG imebainisha kuwa Aprili 5, 2017 NSSF iliomba ridhaa ya BoT ili kuwekeza katika hisa za Vodacom ambazo faida yake ilikuwa chini ukilinganisha na dhamana za serikali. Hata hivyo, kabla ya ridhaa husika kutolewa, Aprili 10, 2017 Bodi ya NSSF iliidhinisha mfuko kutumia Sh bilioni 40 katika kuwekeza katika ununuzi wa hisa za Vodacom bila ya kupata kibali cha BoT.

Aprili 20, 2017, BoT ilikataa kuidhinisha uwekezaji huo kwa msingi kuwa faida itakayopatikana ni ndogo ukilinganisha na faida ambayo NSSF ingepata kwa kununua dhamana za Serikali.

“Mathalani, endapo NSSF wangewekeza kwenye dhamana za muda mfupi (Treasury bills) zingetoa faida ya asilimia 15 na zile za muda mrefu (Bonds) kwa miaka mitano zingetoa faida kwa asilimia 17.92, Faida zilizofafanuliwa ni tofauti na faida za asilimia mbili ambayo NSSF inapata kwa mwaka kwa kuwekeza katika hisa za Vodacom. Kwa msingi huo, uwekezaji husika ulikiuka mwongozo wa uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na una athari katika kutengeneza faida kwa shirika,” anasema Kaboyoka.

Kwa upande wa NHC, PAC inasema kutokana na miradi mingi ya nyumba kusimamishwa kuna uwezekano kwa NHC kushtakiwa na wakandarasi, hivyo serikali inatakiwa iangalie namna bora ya kuiwezesha NHC kukamilisha miradi ambayo ilikuwa katika hatua za mwisho za utekelezaji ili kupunguza hasara ambayo tayari imepatikana.

Kamati hiyo imetaja baadhi ya miradi iliyosimama ni wa nyumba 711 uliopo Kawe, Dar es Salaam wenye thamani ya Sh bilioni 142.55. Mradi huo umesimama tangu mwanzoni mwa mwaka 2017 kutokana na ukosefu wa fedha. Pia nyumba 771 eneo hilo la Kawe zimesimama ujenzi wake. Mradi mwingine ni wa ujenzi wa Victoria Palace wenye thamani ya Sh bilioni 34.14.

Mradi huo umesimama tangu mwaka 2017, ambapo pamoja na kusimama CAG alibaini ongezeko la gharama kwa zaidi ya Sh bilioni 6.86 ambalo anakiri hazikutolewa maelezo ya msingi.

“Uwezekano wa NHC kupata hasara endapo itavunja mkataba na wakandarasi ni kubwa. Mathalani, taarifa ya CAG inafafanua kuwa NHC watalazimika kuwalipa wakandarasi Sh bilioni 99.99 kama gharama za kuvunjwa mkataba. Aidha, NHC watalazimika kurejesha Sh bilioni 2.6 kwa wateja waliokwishaanza kulipia manunuzi ya nyumba hizo hapo awali,” anafafanua Kaboyoka.

Anaongeza kwamba ni dhahiri kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ulianza bila kufuata taratyibu zilizopo. Sambamba na hilo anasema Bunge pia limeazimia serikali iangalie namna bora ya kuliwezesha Shirika la Nyumba (NHC) kukamilisha miradi ambayo ilikuwa katika hatua za mwisho za utekelezaji ambayo imesimamishwa ili kupunguza hasara ambayo tayari imepatikana.

Bunge limeazimia serikali iendelee na uchunguzi wa kina wa miradi yote ya NHC ili kubaini dosari zilizopo katika miradi husika kwani baadhi ya miradi imebainika kuwa ilitekelezwa kwa gharama zisizo halisia na usimamizi wake haukuwa na ufanisi.

“Kuna viashiria vya kutowajibika ipasavyo kwa uliokuwa uongozi wa NHC katika kuhakiki gharama za miradi hiyo. Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuangalia namna bora ya kukamilisha miradi hiyo ili kuepusha hasara kubwa ambayo NHC inaweza kupata hapo baadaye,” anasema mwenyekiti huyo wa PAC.

Anasema kamati hiyo imebaini kutokamilika kwa wakati miradi inayotekelezwa na Wakala wa Majengo (TBA), hali inayoisababishia serikali hasara kwa kuongeza gharama za ujenzi na kuwanyima wateja fursa za kutumia miradi husika kwa wakati mwafaka.

“Bunge linaazimia TBA waboreshe na kuimarisha kitengo cha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha miradi yote inaanza na kukamilika kwa kuzingatia muda uliokubalika kimkataba na wabuni utaratibu wenye ufanisi wa udhibiti wa mifumo ya ndani katika utekelezaji wa miradi hasa katika eneo la matumizi ya fedha, vifaa vya ujenzi na rasilimali watu ili kuharakisha utekelezaji wa miradi,” anasema.

TBA ilipewa majukumu ya ujenzi wa majengo na taasisi mbalimbali za serikali kwa mikataba yenye gharama za takribani Sh 24,068,482,27816. Katika kushughulikia hoja ya TBA kutokamilisha miradi kwa wakati, kamati ilibaini dosari katika baadhi ya miradi, vifaa vya ujenzi vilivyotolewa havikuwa vimepimwa na wahandisi wa miradi kwa kuzingatia makisio ya gharama za ujenzi (BOQ) Miradi ambayo TBA imeshindwa kukamilisha kwa wakati ni mradi wa ujenzi wa nyumba za “Magomeni Quarters” wenye thamani ya Sh bilioni 20.

Miradi mingine inayotekelezwa na TBA na ambayo ina dosari za utekelezaji ni pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Songwe, Makao Makuu ya TANROADS - Dodoma, Jengo la Tume ya Maadili - Dodoma, Jengo la Tume ya Uchaguzi – Dodoma, Jengo la Halmashauri ya Mji – Tarime, Jengo la Halmashauri ya Wilaya – Butiama na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa – Geita.

Kuhusu utendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wamebaini dosari kubwa za kiutendaji ikiwa ni pamoja na CAG kutoa “disclaimer of opinion” (kushindwa kutoa maoni yake) katika hesabu za shirika hivyo Bunge limeazimia serikali kupitia Ofisi ya Msajili (TRO) wa Hazina iimarishe usimamizi wa karibu wa STAMICO ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya shughuli za utendaji wa kila siku wa shirika hilo, Serikali pia imeshauriwa na bunge ifanye mapitio ya mikataba yote ambayo STAMICO imeingia na kampuni tanzu ili kuhakikisha makubaliano katika mikataba yanatekelezwa ipasavyo na masharti hasi yanaondolewa na STAMICO ifanye uthamini wa mali zake ili kutambua thamani halisi ya mali za kampuni kwa sasa.

Mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2018 CAG alishindwa kutoa maoni ya ukaguzi katika Shirika la Madini la Taifa (Disclaimer of opinion). Hii ni mojawapo ya hati ya ukaguzi ambayo hutolewa pindi Mkaguzi anaposhindwa kupata taarifa muhimu za kukamilisha ukaguzi wake na hivyo kukwazwa kwa mawanda ya ukaguzi. Jambo hili limeenda sambamba na kuongezeka kwa hasara ya shirika kutoka Sh 715, 621, 000 (Juni, 2017) hadi Sh 2,387,167,000 (Juni, 2018). STAMICO ilipata hati hiyo kutokana na kutojumuishwa kwa taarifa za hesabu za Kampuni Tanzu za STAMIGOLD Limited na Kyerwa Tin Company Limited katika hesabu jumuifu za STAMICO.

Jambo hili ni kinyume na kanuni ya 9 na ya 10 ya Kanuni za Uandaaji wa Hesabu kimataifa. Ni kwa msingi huo, hali halisi ya mali na madeni ya kampuni hizo tanzu haijulikani hadi sasa. PAC inasema thamani ya jumla ya Sh bilioni 33 ambayo ni thamani ya uwekezaji uliofanywa na STAMICO katika kampuni tanzu haina uhalisia. CAG alishindwa kupata uthibitisho wa kutosha wa thamani hiyo kutokana na kutokuwepo na taarifa sahihi za uwekezaji.

Alisema hadi sasa STAMICO imeshindwa kubaini iwapo inapata hasara au faida katika uwekezaji iliofanya katika mgodi wa Buckreef Gold Company Limited. Uwekezaji huu ulianza tangu mwaka 2011. Kutokutambua faida au hasara kutokana na uwekezaji wa hisa katika mgodi huo ni kinyume na matakwa ya Kanuni za Kimataifa za Ukaguzi na hivyo kukwamisha jitihada za kuongeza faida kwa Serikali.

“Uchambuzi wa Kamati ulibaini pia kuwa STAMICO ilikuwa haijafanya tathmini ya makubaliano baina yake na Kampuni ya Tanzanite One Mining Company ili kubaini iwapo makubaliano yao ni ya uendeshaji wa pamoja wa mgodi au ni makubaliano ya ubia. Changamoto nyingine inayokwaza ufanisi wa STAMICO ilikuwa ni kwa shirika hilo kushindwa kutambua asilimia 10 ya thamani ya uwekezaji wake katika Kampuni ya Itetemia. Kwa STAMICO kushindwa kutambua jambo hili, kunaashiria kwamba STAMICO haipati faida stahiki zinazotokana na shughuli za uchimbaji zinazofanywa na Kampuni ya Itetemia Mining Company.

Hata hivyo, Waziri wa Madini, Dotto Biteko wakati anajibu hoja kabla azimio hilo kupitishwa, anasema tangu iundwe STAMICO kwenye miaka ya 1960 kwa mara ya kwanza imefanya biashara na kupata Sh bilioni 24.

Ilikuwa Desemba mwaka jana. Katika mwaa 2019 baadhi yamaeneo ambayo PAC imeyashughulikia ambayo ni hayo iliyoona ina matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma kama yalivyoainishwa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) na kutoa mapendekezo yake ili kupunguza matumizi hayo mabaya ya fedha za umma.

“TEMBO ndiye mnyama anayeongoza kwa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu ...

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi