loader
Picha

Bil 25/- zahitajika kurejesha miundombinu

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema zinahitajika Sh bilioni 25 kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya reli na barabara katika hali yake ya kawaida baada ya kuharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

Aidha fedha hizo ni makadirio yaliyofanyika Januari 30 mwaka huu ya matengenezo ya miundombinu hiyo ambayo mingi iliharibiwa vibaya. Kamwelwe alisema hayo wakati akifungua mkutano wa 13 wa kupima utendaji katika sekta ya uchukuzi uliofanyika jijini Dar es Salaam ambao uliwashirikisha wadau wote wa sekta ya uchukuzi wakiwemo serikali, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia, wanataaluma na sekta binafsi.

Alisema kwa sababu mvua bado zinaendelea kunyesha na Machi ndiyo kuna mvua kubwa za masika bado haieleweki mpaka mwisho uharibifu utafikia kiasi gani. Alisema kutokana na umuhimu wa miundombinu hiyo, serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa barabara kwani hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2019 mtandao wa barabara nchini ulikuwa na thamani ya Doda za Marekani milioni 8,582 ambao serikali kupitia Mfuko wa barabara unaendelea kutenga fedha.

Kamwelwe alisema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu hiyo unaenda sambamba na kuimarisha usalama kwa kuweka alama za barabarani ambazo kwa mujibu wa takwimu zilizopo idadi ya malori yaliyohusika kwenye ajali ilipungua kwa asilimia 35 kutoka malori 838 hadi kufikia malori 544 kwa kipindi kilichoishia Juni mwaka jana.

“Katika kipindi hicho vifo vimepungua kutoka ajali 1,563 mpaka 938, punguzo la asilimia 39.6. Ajali za mabasi zimepungua kutoka ajali 1,005 mpaka 724 punguzo la asilimia 27.96 na vifo vimepungua kwa asilimia 31.11,”alisema.

Waziri huyo alisema kwa mwaka wa fedha 2019/20 wizara hiyo imepanga kuendelea na matengenezo ya barabara yanayosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (Tarura) kwa kutumia fedha za maendeleo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu alisema ubovu wa miundombinu unaosababishwa na mvua unawapa wakati mgumu kwani kuna wakati magari hayafiki yanakokwenda, yanalala njiani kwa ajili ya kukatika kwa barabara.

Alisema kwa kuwa serikali imeeleza jinsi ilivyojipanga kukarabati, ombi lao kwa serikali ifanye haraka hasa kwenye mikoa ile iliyoathirika kwa kuwa watu wengi wamekopa fedha benki, hivyo magari hayo yasipofanya kazi watashindwa kuirejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mrutu alisema baada ya miundombinu ya treni kukamilika idadi kubwa ya watu watatumia usafiri huo badala ya mabasi kwa kuwa inatembea kwa kasi zaidi. Alitoa mfano kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro treni ya mwendo kasi (SGR) ikianza itatumia saa moja na basi itatumia saa tano hivyo watu wengi watapanda treni.

“Ni vizuri wenye mabasi waanze kufikiria na serikali iwatengenezee miundumbinu ili wawekeze kwenye treni,” alisema.

Awali Mkurugenzi wa Ujenzi viwanja vya ndege, Emmanuel Raphael alisema mkutano huo umejadili maendeleo ya sekta ya usafiri hususan kwenye sekta ya ujenzi eneo la usafiri wa barabara.

“Tumeona umekuwa ni mzigo mkubwa kwa serikali kusafirisha watu pamoja na bidhaa kwa hiyo serikali imeweka mikakati mipya ya kuimarisha njia nyingine mbadala, kwa mfano usafiri wa reli na wa anga ili kusafirisha watu kwa urahisi zaidi na hivyo kukimbiza kasi ya kukuza uchumi,”alisema.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru imewafutia mashitaka washitakiwa ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi