loader
Picha

Wafanyakazi Automech, Reliance kulipwa

KILOMETA 58 kutoka Kakonko mjini kuna kijiji cha Nyanzige kilichopo katika kata ya Nyamtukuza, Tarafa ya Nyaronga wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma. Katika kata hii ya Nyamtukuza kuna shule kadhaa, moja wapo ni Shule ya Msingi Nyanzige.

Shule hapo nakutana na wanafunzi kadhaa. Kuna ambao hawana tatizo katika kuwezeshwa na wazazi wao kufika shuleni lakini kuna ambao wanahangaika kupata mahitaji muhimu ili kuwafanya waende shule.

Pamoja na hatua ya serikali ya kutoa elimu bila malipo watoto hawa wanaoshindwa kufika shuleni kila siku inatokana, pamoja na mambo mengine, na wazazi au walezi wao kutowajibika katika kuwatimizia mahitaji muhimu. Vijana wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la tano na mdogo wake darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyanzige ni kati ya wanafunzi wanaoonja madhila ya wazazi au walezi kushindwa kuwatimizia mahitaji yao ya msingi ili kuwawezesha kuhudhuria masomo.

Wanafunzi hao walishafiwa na mama yao mzazi na hivyo muda mwingi wamekuwa wakilelewa na baba yao. Hata hivyo, hadi ni shida kwao kupata mahitaji muhimu, chakula na mavazi.

“Tunaishi na baba yetu lakini muda mwingi huwa hayupo nyumbani. Anaishi huko milimani ambako anafanya kazi za kulima. Wakati mwingine mimi na mdogo wangu hapa nyumbani tunakosa mahitaji ya shule na chakula, hivyo inabidi tufanye vibarua ili tupate fedha,” anasema mmoja wao ambaye ndiye mkubwa Watoto hao wanasema ni kazi ngumu kusoma na huku wakifanya vibarua vya kulima mshamba baada ya kutoka shuleni lakini kutokana na mazingira, hawana namna.

Kijana mwingine mwenye umri wa miaka 14, mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo ya Nyanzige anasema anaishi na wazazi wake katika familia yao ya watoto 10. Anasema hali ya nyumbani kupata mahitaji ni ngumu sana na kila mara baba yao anasema hana fedha za kuwagharimia mahitaji yao, hivyo huwataka watafute namna ya kupata mahitaji yao, hasa ya shule.

“Mimi napenda kusoma lakini inabidi nifanye vibarua kupata pesa ninunue sare za shule na viatu… Najisikia aibu kuja shuleni bila sare na viatu,” anasema.

Mwanafunzi mwingine mwenye umri wa miaka 12 wa darasa la tano katika shule hiyo anasema baba yake alishafariki dunia na sasa anaishi na mama yake. Anasema muda mwingi anautumia kwa kufanya kazi za shamba mbali na nyumba kwao. Kutokana na hilo mwanafunzi huyo ambaye anaishi na dada yake anasema wanalazimika kujitafutia mahitaji ya nyumbani na shuleni kwa kufanya vibarua mashambani ili wapate pesa.

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo ya Nyanzige anayesoma darasa la saba anasema mwaka 2015 alifiwa na baba yake, hali iliyosababisha mama yake kuhamia Geita kwa madai ya kwenda kutafuta maisha. Anasema kuondoka kwa mama yake kumeongeza changamoto ya maisha na hivyo kulazimika kuanza kufanya vibarua ili kupata fedha za kujikimu.

Uchunguzi wa mwandishi katika kata ya Nyamtukuza unaonesha kwamba hali ya wazazi kutelekeza familia zao imesababisha watoto wengi kuacha masomo, kujiingiza kwenye kazi za vibarua na wasichana kupata ujauzito sambamba na kufanyishwa kazi ngumu kinyume na umri wao au wakati mwingine kufanyiwa vitendo vya kudhalilishwa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyanzige, Jumanne Kanemela, anasema wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la wazazi kushindwa kugharamia mahitaji ya watoto wao hasa sare za shule, vitabu na viatu, hali ambayo inafanya wanafunzi wengi kuja shule na nguo za nyumbani. Anasema kwa sasa wanao wanafunzi wasio na sare lakini hatua inayofuata ni kutumia uongozi wa serikali ya kijiji kuita wazazi ili kuwaeleza ni namna gani wanapaswa kutekeleza wajibu wao.

“Kutelekezwa kwa watoto ni tatizo kubwa kwa maeneo haya na hasa wazazi kuacha watoto wao na kuhamia mashambani kwenye kilimo.

“Miaka ya nyuma tatizo la wazazi kutelekeza watoto halikuwa kubwa lakini utoro ulikithiri kwa sababu wazazi walikuwa wakiwachukua watoto na kwenda nao mashambani au kuwatoa kwa watu wanaotafuta watoto kwa ajili ya vibarua ndani ya mkoa na nje ya mkoa. Baada ya serikali kuweka mkazo kuhakikisha wanafunzi wanasoma, kwa sasa utoro umepungua lakini tatizo la wazazi kutelekeza watoto ndiyo limeshika kasi,” anasema Kanemera.

Mwalimu huyo mkuu anasema sababu kubwa ya wanafunzi kushindwa kuwa na sare na madaftari kunachangiwa na baadhi ya wazazi kutoona umuhimu wa elimu. Mzazi au mlezi anayeamini katika elimu ya mwanawe hawezi kushindwa kabisa kumsaidia mwanae mahitaji muhimu na hasa kwa kuzingatia ada na michango iliyokuwa inawakwaza wanafunzi wengi imeondolewa na serikali, anasema.

Uchunguzi katika Shule ya Msingi Churazo katika kata hiyo, unaonesha pia kwamba kuna watoto wengi ambao wanakumbana na shida za wazazi kushindwa kuwatimizia mahitaji muhimui ya kibinadamu na hivyo kushindwa kuhudhuria shule kwa asilimia 100. Inaeleza kwamba kwa miaka miwili iliyopita shule hiyo iliwanunulia wanafunzi zaidi ya 100 madaftari na kuwatafutia sare za shule baada ya wazazi wao kushindwa kufanya hivyo.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Sylivia Mgina, anasema licha ya baadhi ya wanafunzi kuishi na wazazi au walezi wao, bado watoto wengi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kukosa mahitaji muhimu ya shule kutokana na wazazi hao kutoona umuhimu wa jambo hilo. Kadhalika, anasema tatizo wakati mwingine linasababishwa na wazazi na walezi kukihama kijiji na kwenda kuishi mashambani au kwenda kutafuta maisha nje ya mkoa na kutelekeza watoto.

Askari mgambo katika kijiji cha Churazo, Ndalugije Kakuru anasema alilazimika kuwachukua watoto wawili waliokuwa wakisoma shule ya msingi Churazo na kuishi nao nyumbani kwake baada ya kuwakuta wakiwa katika hali mbaya baada ya kutelekezwa na wazazi wao. Mwenyekiti wa kijiji cha Kinyinya, Herman Machebete, anasema tabia ya ulevi kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani ni miongoni mwa sababu zinazochangia wazazi kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa watoto.

“Wakati wa mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), hata fedha za wanafunzi mashuleni zilikuwa zikitumiwa vibaya na baadhi ya wazazi kuzinywea pombe,” anasema.

Anasema hali hiyo ilisababisha wanafunzi kukosa sare na mahitaji muhimu ya kibinadamu, jambo hilo walilisimamia na hali ikawa nzuri kidogo. Taarifa iliyotolewa na Ofisa Elimu wa mkoa Kigoma kuhusu matokeo ya darasa la saba mwaka 2018 inaonyesha kuwa wakati wanafunzi 25,704 walifaulu kujiunga na kidato cha kwanza Januari mwaka jana jumla ya wanafunzi 409 waliosajiliwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2012 walishindwa kumaliza shule. Anasema mimba kwa wanafunzi ni miongoni mwa visababishi hivyo ambapo kwa miaka miwili, wanafunzi 190 walipata mimba mkoani Kigoma.

Kanali Hosea Ndagala, Mkuu wa wilaya Kakonko anasema hajapata taarifa sahihi kuhusu ukubwa wa tatizo la wazazi kutelekeza watoto wao ingawa anajua lipo tatizo la wazazi kushindwa kuwanunulia sare na madaftari.

“Suala hilo tunalifanyia kazi na serikali za vijiji na kata zimepewa agizo la kuhakikisha wanasimamia jukumu la kuona wazazi wanagharimia mahitaji ya watoto wao baada ya serikali kugharamia mahitaji ya msingi ya shuleni ikiwemo ada kupitia mpango wa elimu bila malipo,” anasema Ndagala.

Mkuu huyo wa wilaya anasema kwa mujibu wa idara ya taifa ya takwimu (NBS), wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya tano maskini zaidi nchini lakini uhalisia kwa sasa hali haiko hivyo.

“Tunazo fursa nyingi na tunazitumia, ipo miradi ya kilimo ambapo serikali kupitia halmashauri ina mipango mbalimbali ambayo inatekelezwa. Lakini tunalo soko la ujirani lililopo mpakani na Burundi ambalo ni kichocheo kikubwa cha biashara na uchumi,” anasema Mkuu huyo wa wilaya.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Masumbuko Stephano, anasema mwamko mdogo wa wazazi umechangia kuwafanya washindwe kugharamia mahitaji muhimu ya watoto wao. Ripoti ya mwaka 2016 ya Utafiti wa pamoja wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha kuwa watoto milioni 4.3 wenye umri wa miaka mitano hadi 17 nchini waliacha shule.

Ripoti hiyo (Tanzania Country report on out of school children) inaonesha kuwa kati ya hao, watoto milioni 2.5 hawakuwa wamesoma kabisa. Sambamba na hiyo, ripoti ya utafiti kuhusu ukatili dhidi ya watoto nchini iliotolewa mwaka 2011 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) inaonesha kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24 waliofanyiwa ukatili wakati wanakua.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa asilimia 20 ya watoto wenye umri kati ya miaka 10 - 14 nchini Tanzania hawaishi na wazazi wao wa kuwazaa au wenye nasaba nao huku asilimia 41 ya vijana wakiwa wameshajiingiza kwenye ajira.

Wakati hali ikiwa hivyo Mkataba wa kimataifa wa haki za watoto unaeleza wazi wajibu wa serikali na wazazi katika kuhakikisha wanasimamia malezi, makuzi na huduma muhimu kwa mtoto ikiwemo elimu na afya. Kuwepo kwa taarifa hizo za utafiti kunaonyesha kuwa wazazi wanalo jukumu kubwa katika kuwasimamia watoto wao kuhakikisha wanapata mahitaji yao ya msingi kama ambayo imeelezwa kwenye Mkataba wa kimataifa wa haki za watoto (CRC).

Mkataba wa kimataifa wa haki za watoto unaeleza wazi wajibu wa serikali na wazazi katika kuhakikisha wanasimamia malezi, makuzi na huduma muhimu kwa mtoto ikiwemo elimu na afya. Ibara ya 4 ya mkataba huo inaeleza kuwa serikali zote ambazo zimeridhia mkataba huu zina wajibu wa kuhakikisha haki zote za watoto zinalindwa, kutekelezwa na kuthaminiwa na kila mtu.

USHAURI ni suala lenye umuhimu wa ...

foto
Mwandishi: Fadhili abdallah

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi