loader
Picha

Watunzi wa riwaya watakapokutana na wasomaji Dar

“HUYU ndiye Edi Ganzel uliyekuwa ukimuuliza sana,” aliniambia Mzee Barnabas Maro, akinitambulisha kwa mmoja wa watunzi mahiri wa riwaya kuwahi kutokea nchini.

Wakati huo, mwaka 1998, Mzee Barnabas Maro, maarufu Kamba Ulaya, alikuwa mhariri wa makala wa gazeti la Nipashe huku mtunzi huyo akitoa hadithi yake moja katika gazeti hilo iliyokuwa maarufu sana.

Kwa jinsi nilivyokuwa ninavutiwa na mtunzi huyo ambaye sasa hivi ni marehemu, nilifurahi sana kumwona mubashara na kupata nafasi ya kubadilishana naye mawazo. Baadhi ya vitabu vyake ninavyovikumbuka nilivyovisoma miaka ya 1980 ni Ndoto ya Mwendawazimu, Kitanzi, Faili Maalumu, Jogoo la Shamba, Kijasho Chembamba na Kifo cha Kishenzi.

Wakati ninakutana na mtunzi huyo nguli ambaye sasa ni marehemu, hizi mnazoita ‘selfie’ hazikuwepo, vinginevyo ningepiga naye picha lukuki. Furaha niliyoipata siku hiyo, ni kama niliyoipata siku nilipokutana na mtunzi mwingine mahiri, Faraji Katalambula, katika msiba wa jamaa yake mmoja maeneo ya Mbagala, Dar es Salaam.

Sikuamini macho yangu kwamba niko mbele ya mtunzi aliyekuwa akinikosha sana kwa visa alivyokuwa akibuni. Nasikia Katalambuka pia kwa sasa ni marehemu. Yeye alinikosha kwa riwaya zake za kusisimua kama Buriani, Simu ya Kifo, Ugeni wa Wasiwasi, Niadhibu Tafadhali, Pili Pilipili na nyinginezo.

Licha ya kubahatika kuwaona mubashara watunzi kadhaa nguli wa riwaya kama Hammie Rajabu na Ben Mtobwa, sijawahi kuonana na watunzi wengine ambao nilipenda pia riwaya zao kama John Simbamwene, Godfrey Nyasulu, Aristablus Musiba, Leo Odera Omolo, Mohamed Saidi Abdullah (MSA), Euphrase Kezilahabi, Shafi Adam Shafi, John Rutayisingwa na wengineo.

Wengi wa watunzi hawa wameshafariki dunia ingawa baadhi bado wako hai. Kama ukisoma makala haya ukaona ninatiririka vizuri au kama ulishasoma riwaya yangu yoyote kwenye magazeti ukaona naandika vitu vya kueleweka, basi jua kwamba lugha yangu imeboreshwa sana na riwaya za watunzi hao. Nimegundua kwamba wanangu wanapoandika insha, sioni mtiririko unaovutia na bila shaka ni kukosa kusoma riwaya nyingi kama ilivyokuwa kwangu zama hizo na hata sasa.

Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira Tanzania (Uwaridi) umeandaa tukio muhimu sana litakalojiri Jumapili ya wiki hii, Februari 23 litakalowakutanisha watunzi wa riwaya nchini na wasomaji wao. Hatua hii imeonesha hakika kwamba hizi ni zama mpya ambapo sasa wasomaji wa riwaya wa sasa hawatakuwa kama mimi, kusoma riwaya na kutamani kumwona mtunzi lakini mazingira yakiwa hayaruhusu.

Rais wa Uwaridi, Hussein Tuwa, aliniambia kwamba katika tukio hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (zamani Chuo cha Posta), Kijitonyama, Dar es Salaam kuanzia saa saba mchana ni la kwanza na la aina yake nchini. Tuwa anasema wazo la kuandaa tukio hilo lilikuja kutokana na wasomaji wengi kuonesha nia ya kutaka kukutana na watunzi mbalimbali wa riwaya nchini ili kubadilishana nao mawazo.

“Wasomaji watapata fursa ya kuzungumza na watunzi, kujua changamoto zao na watunzi kusikia hisia za wasomaji kuhusu kazi mbalimbali za fasihi wanazofanya,” aliniambia Tuwa.

Mtunzi huyo mahiri katika zama hizi tulizo nazo anasema hatua hiyo inalenga pia kuhamasisha usomaji zaidi wa vitabu nchini na kwamba wasomaji pia watapata nafasi ya kuwasikia watunzi wakijieleza kuhusu maisha yao na kupiga nao picha kwenye zulia jekundu.

“Katika eneo la tukio kutakuwa na watunzi wengi, lakini kwa kuanzia tutatambulisha rasmi watunzi watatu na kila baada ya miezi kadhaa tutakuwa tunatambulisha watunzi wengine watatu. Hawa watapata nafasi ya kueleza historia na kazi zao na wasomaji kuwauliza maswali,” anasema.

Tuwa anayetamba na kitabu cha Mkimbizi, anasema wanatarajia wawe wakipandisha watunzi wawili wanaochipukia na mmoja mkongwe au mwenye jina kubwa. Watunzi ambao wanatarajiwa kutambulishwa Jumapili hii ni Lilian Mbaga ambaye ‘ametisha’ na riwaya yake ya Hatinafsi na Lello Mmasy aliyepagawisha wasomaji na kitabu chake cha Mimi na Rais.

Mtunzi ambaye pengine wengi watatamani sana kumwona ni Tuwa mwenyewe, ambaye vitabu vyake kadhaa vimekuwa vikitumika katika mitaala ya elimu nchini. Rais huyo wa Uwaridi anasema wasomaji pia watapata fursa ya kununua vitabu mbalimbali vya riwaya vitakavyouzwa kwa bei nafuu kidogo, tofauti na vinapouzwa kwenye maduka ya vitabu. Anataja baadhi ya vitabu vitakavyouzwa siku hiyo kuwa ni Mkimbizi na Mfadhili alivyotunga yeye Tuwa, Kiroba Cheusi cha Laura Pettie, Hakinafsi na Mimi na Rais, Chotara cha Joseph Shalua na vinginevyo vingi.

“Tumeanzia tukio hili la aina yake Dar es Salaam lakini lengo ni kulipeleka katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu bila kusahau Zanzibar ambako kuna watunzi wakubwa na wasomaji wazuri wa riwaya zetu,” anasema rais huyo na kuongeza hata hivyo kwamba bado wanakaribisha wadhamini katika kulifanikisha.

Mtunzi mwingine maarufu nchini, Beka Mfaume, ameipongeza Uwaridi kwa kuandaa tukio hilo akisema litasaidia sana kurejesha utamaduni wa kusoma vitabu nchini.

“Serikali kwa njia moja au nyingine inawajibika kuunga mkono Uwaridi ambayo imepania kuleta maarifa kwa wananchi kupitia kwa wasoma riwaya na kuwajua waandishi wake,” anasema Beka katika taarifa yake ya kuipongeza Uwaridi.

Beka anaongeza: “Hii Jumapili Februari 23 ni siku kubwa sana kwa waandishi na wasomaji wa riwaya waliopo Dar es Salaam kuhudhuria tukio hili la kihistoria ambalo ni la kwanza kutokea katika nchi yetu.’ Beka anazidi kuipongeza Uwaridi kwa kurudisha heshima kwa Mtanzania kwa kuchangia kumfanya apende kusoma vitabu ambapo ataburudika na kujipatia maarifa mbalimbali.

“Uwaridi imeweza kuwaleta pamoja waandishi wa riwaya wenye viwango vya kimataifa. Hili ni jambo jema sana,” anasema.

Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa Uwaridi, Maundu Mwingizi, Uwaridi ilianza rasmi mwaka 2016 baada ya kusajiliwa rasmi ingawa shughuli zake anasema zilianza mapema kabla ya hapo. Kwa mujibu wa Maundu, malengo ya Uwaridi ni pamoja na kuboresha kazi za riwaya nchini, kukuza fasihi, kuinua ari ya usomaji wa vitabu na kufuatilia haki kazi za watunzi wa riwaya waliopo hai na waliotangulia mbele za haki.

Akifafanua kuhusu uboreshaji wa kazi za Riwaya unaofanywa na Uwaridi, Maundu anakiri kwamba hapo nyuma kulikuwa kumeibuka uandishi holela wa riwaya na watunzi wengi kutozingatia maadili au kukosea lugha.

Anasema kupitia Uwaridi, kila hadithi inapitiwa na wahariri mahiri na maudhui kufanyiwa utafiti kuona yanavyosadifu hali halisi ili kitabu kikitoka kiwe kimekidhi viwango. Ni kwa mantiki hiyo, Maundu anawahimiza Watanzania kusoma vitabu, hususani vyenye nembo ya Uwaridi ambapo watanufaika na mengi, ikiwa ni pamoja na lugha sanifu ya Kiswahili.

Anawahimiza pia watengeneza filamu nchini kuwasiliana na Uwaridi ambako watanunua hadithi zenye viwango na hivyo kuboresha soko la filamu la Tanzania badala ya hali ya sasa kuokoteza hadithi zisizo na viwango mitaani.

WIKI iliyopita tulianza kuangalia kasumba miongoni mwa jamii kudhani kwamba ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi