loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Taasisi inavyosaidia serikali kupambana na saratani

BAADA ya kupiga kambi kwa siku tofauti 15 katika vituo 15 na kuwaona wananchi 974, kampeni ya kupima bure saratani ya matiti na tezi dume inayoendeshwa na Associazone Ruvuma Onlus imeshauri watu 33 kufi ka hospitali ya Muhimbili au Ocean Road kwa ajili ya kuangaliwa zaidi afya zao hususani viashiria vya saratani ya matiti na tezi dume.

Kitu ambacho waendesha kampeni wamejifunza ni kwamba ipo haja kwa Watanzania kujikita zaidi katika afya zao kwani wengi wao huenda kupimwa wakiwa wamekwishajichokea. Wahusika katika kampeni hiyo wanashauri watanzania kuhakikisha kwamba wanaweka akiba ya kutosha kwa ajili ya kuchunguza na kuuguza miili yao kabla hali haijabadilika na kuwa mbaya na ikashindikana kuokolewa kimatibabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi ya Associazone Ruvuma Onlus ambayo inafanya kazi ya kupima saratani ya matiti na tezi dume kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Idara ya Afya, kwa ufadhili wa Associazione Ruvuma onlus Italy mwitikio wa wananchi katika kampeni yao hasa wanawake ni mkubwa zaidi.

Msimamizi wa kampeni hiyo, Renatus Rwechungura anasema kwamba wakitumia vifaa vya kisasa kabisa na kliniki inayohamishika wamefanya uchunguzi wa afya za waliofika na kubaini kwamba mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa hasa unaposogeza huduma karibu na wananchi.

Vile vile mwamko kwa upande wa wanaume kuchunguzwa tezi dume umeongezeka baada ya kubaini kwamba mtindo wa kupima ni wa kisasa kwa kutumia ultrasound badala ya kipimo cha zamani cha kutumia kidole, ambacho watu walikuwa wanaona kama wanadhalilishwa. Wakitumia gari maalumu lililoletwa kwa ufadhili wa Associazione Ruvuma onlus Italy anasema walishapiga kambi Gdb Social Centre Tegeta, Tegeta Mission dispensary, Consolata Dispensary- Mbagala, Cardinal Rugambwa Hospital- Ukonga, Vijibweni Hospital, Jangwani- Kariakoo, Antonia Verna Dispensary, Kawe na sokoni Mbezi Luis.

Anasema katika utoaji huduma wamebaini mambo mengi pamoja na haja kubwa ya kuhakikisha kwamba huduma hizo zinasogezwa karibu na wananchi hasa wale wasiokuwa na kitu ambao ndio waliofika na kufanya maulizo mengi. “Tumekuwa tukihudumia watu zaidi ya 100 katika kambi zetu, na kuna wakati tunapata tabu ya kuendelea kutoa huduma, ingawa Kariakoo tulitoa huduma hadi saa 4 usiku na hasa kwa wanaume waliokuwa wakiangalia tezi dume,” anasema Renatus akiwa katika kituo cha Mbezi Luis.

Katika kituo hicho waliona watu 103 tangu saa mbili walipoanza hadi saa kumi na moja walipofunga huduma kwa sababu za kiufundi zinazoambatana na kanuni za utoaji wa huduma. Kwa mujibu wa Renatus waliofanyiwa kipimo cha ultrasound ni 93, mtu mmoja akapewa hati ya rufani kwa matibabu zaidi wakati mmoja alikutwa na uvimbe wa kawaida wa ziwa na wanaume wanane walikutwa na uvimbe.

Katika kituo hicho ambapo zaidi ya watu wanne walifika muda usio muafaka na kuambiwa wajipange upya kwa kambi itakayokuwa Kimara Februari 28, mwaka huu, walisema kwamba huduma hiyo ni ukombozi kwao, kwani hawana fedha za kuangaliwa katika hospitali ambazo kipimo cha ultra sound pekee hawakimudu.

Katika taarifa yake, anasema kwamba kwenye kampeni hiyo ambapo wanaume wamekuwa viumbe adimu (kwa uhaba wao) wanawake wamekuwa wakiifuata hiyo huduma pia wakitaka kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Hapa ndipo unapoona shida, sisi tunaangalia tezi dume na saratani ya matiti, lakini wanawake waliofika hapa zaidi ya 500 wanataka kufanyiwa uchunguzi wa saratani, labda kwa sababu ya kampeni kubwa ambayo taifa imeshaendesha,” anasema Renatus katika mahojiano.

Kazi ya kupima bure saratani ya matiti na tezi dume ilianzishwa na taasisi ya Associazone Ruvuma Onlus Desemba 14, mwaka 2019 na wanatarajia kukamilisha mwishoni mwa Machi, mwaka huu, endapo hawatafanikiwa kupata wafadhili watakaochangia ili huduma hiyo iendelee kutolewa.

Mtendaji wa associazone Ruvuma ya hapa nchini, Happy Seiph anasema kwamba kutokana na mahitaji kuwa makubwa ameandika barua kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi hususani Italia kuona kama wanaweza kusaidia zaidi.

“Najitahidi kuomba tena ufadhili lakini wafadhili wetu wakubwa ambao wamenunua mashine tunazofanyia kazi ambao ndio sister Organization yetu, Associazione Ruvuma onlus Italy nao wana majukumu Italia,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwa kama serikali na mashirika, watu binafsi wakisaidia angalau kudhamini Sh 10,000 kwa kila mtu itasaidia kulipia gharama za uendeshaji na kuendeleza huduma hiyo na kuitanua mikoani kwa jinsi watu walivyoitikia Dar es Salaam. Aidha, anasema kwamba watu wengi waliofika walionekana wana tatizo kwa muda mrefu lakini walikosa uwezo wa kufanya vipimo na inawezekana kabisa tatizo limekuwa kubwa kwa kipindi chote cha kusubiri.

Vile vile Happy anasema kuwa baada ya kuwapatia majibu watu waliogundulika kuwa wana viashiria vya saratani au uvimbe wagonjwa hao wamekuwa wakielekezwa waende kwenye hospitali kubwa kama Muhimbili na Ocean Road Cancer Institute kwa uchunguzi zaidi. Baadae wao hufanya ufuatiliaji kuona kama wanakwenda kwa vipimo zaidi na kujua kama wamepata matibabu na kama wana changamoto mbalimbali.

Katika ufuatiliaji wamegundua kuwa wengi wao baada ya kupewa taarifa za awali katika kutafuta matibabu wamerudi na kukaa nyumbani kwa kukosa fedha za matibabu au wanaogopa kuanza matibabu kwa kuwa wamelekezwa na ndugu zao eti ukigusa saratani au uvimbe hautapona. Kimsingi, elimu ya kutosha inahitajika kwa wananchi kujua maisha baada ya kugunduliwa na saratani vinginevyo kazi wanayofanya ya uchunguzi itakuwa haina tija.

Kwa mujibu wa wataalamu wanawake walio na umri wa miaka 30 walio na historia katika familia ya jamaa zao kuugua saratani ya matiti, wanapaswa kufanyiwa ukaguzi wa kila mwaka kubaini mapema iwapo wanaugua ugonjwa huo, shirika la misaada linasema.

Aidha, utafiti unaonesha kwamba saratani hutambulika mapema wakati wanawake wenye umri wa kati ya miaka 35 hadi 39 walio katika hatari ya kuugua wanapofanyiwa ukaguzi wa kila mwaka yaani mammograms. Utafiti huo uliofanywa na watafiti katika Chuo Kikuu cha Manchester, kimetoa picha za wanawake 2,899 wa umri huo walioonekana kuwa katika hatari kubwa na ya wastani ya kuugua ugonjwa huo baada ya kumuona daktari. Ukaguzi huo umegundua uvimbe 35 wa ndani ya matiti, baadhi ukiwa ni mdogo na uliotambuliwa mapema - ishara kwamba haujasambaa mwilini.

“Kwa wanawake wenye historia katika familia, kuondosha uvimbe pasi kufanywa upasuaji huenda ni njia ya kuzuia saratani ,” anasema Profesa Gareth Evans, mhariri mkuu wa utafiti huo.

Aidha, anaeleza kuwa utafiti huo unaonesha kwamba kufanyiwa ukaguzi wa kila mwaka inasaidia katika kutambua uvimbe mapema na kuushughulikia. Saratani ni aina ya ugonjwa unaosababisha ukuaji wa seli za mwili kubadilika na kukua bila mpangilio maalumu. Saratani ya matiti hutokea kwenye titi ambalo kwa kawaida lina sehemu ya kutengeneza maziwa ijulikanayo kama lobules na aina fulani ya mishipa inayounganisha hizo lobules na chuchu za titi. Sehemu kubwa iliyobakia ya matiti inajumuisha mafuta na tishu ambazo kitaalamu zinaitwa connective and lymphatic tissue.

Saratani ya matiti inayotokea kwenye lobules huitwa lobular carcinoma na ile inayotokea kwenye ducts huitwa ductal carcinoma. Ingawa, saratani ya matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.

Ingawa uwezekano wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu inaeleweka kwamba kadri umri wa mtu unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa mkubwa.

Wanawake walio na umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa (mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45. Dalili za saratani kusambaa mwilini ni maumivu ya mifupa, maumivu kwenye titi, vidonda kwenye ngozi, kuvimba mkono karibu na eneo la saratani na kupungua uzito.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi