loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watanzania waelewe deni la nje ni himilivu

MCHUMI kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza, Profesa Christopher Adam amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambazo hazipo katika hatari kubwa ya kudorora kiuchumi kutokana na kuwa na kiwango cha chini cha madeni.

Profesa Adam alisema hayo wakati akitoa mada katika kongamano la wazi, lililofanyika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam na kuwahusisha watu mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa chuo hicho.

Katika mada yake, mchumi huo alisema katika utafiti uliofanyika mwaka jana, Tanzania, Senegal na Uganda ndizo nchi pekee zilizokuwa katika msimamo salama wa uwiano wa madeni katika nchi nyingi, zilizopo katika ukanda huo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka jana.

Katika kongamano hilo ambalo mada kuu yake ilikuwa ‘Je, ni kwa kiasi gani nchi za Afrika zinakabiliwa na tatizo jipya la madeni?’ ikilenga kupata mtazamo kwa wataalamu mbalimbali, mchumi huyo alisema zipo baadhi ya nchi ndani ya bara hilo, ambazo zimekuwa na madeni makubwa, kiasi cha kushindwa kuyamudu.

Ripoti hii ya utafiti kuhusu ukweli wa deni la Tanzania katika uso wa dunia, imekuja katika kipindi muafaka ambapo kumekuwa na taarifa nyingi za upotoshaji kuhusu hali ya uchumi na deni la nje la Tanzania.

Mara kadhaa serikali imekuwa ikieleza kuwa deni la Tanzania nje ni himilivu kiasi cha kuifanya kutokuwa katika hatari ya kulemewa, lakini wapo watu wasio na nia njema na uzalendo kwa taifa, wamekuwa wanabeza taarifa hizo za serikali.

Mathalani wakati wa hotuba za bajeti, wapo wanasiasa ambao kwa makusudi wamekuwa wanapotosha ukweli kuhusu deni la Tanzania nje, kwa kuwaaminisha wananchi kuwa Tanzania ni nchi inayokabiliwa na mzigo mzito wa madeni nje ya nchi na kuwa katika hali ya kutokopesheka.

Matokeo ya utafiti huu wa hivi karibuni uliobainishwa na Profesa Adam kutoka Chuo Kikuu kinachoheshimika duniani, yanathibitisha ukweli wa taarifa za serikali kuwa deni ni himilivu na yanafuta kabisa taarifa za upotoshaji kwamba Tanzania ina zigo zito la madeni.

Kama alivyosema Profesa Adam, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu tu katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo haipo katika hatari ya kudorora kwa uchumi wake kutokana na kuwa na kiwango cha chini sana cha madeni kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi za ukanda huo.

Kutokana na utafiti huo ni matumaini yetu kuwa wale wote wanaopenda kuzusha taarifa ambazo si za kitafiti, sasa wataitumia ripoti hii kuueleza umma wa Watanzania na jumuiya ya kimataifa ukweli kwamba deni la nje la Tanzania ni himilivu na hakuna hatari ya uchumi wake kudorora badala yake utashamiri kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025.

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), Jumanne ya wiki hii lilizindua ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi