loader
Picha

NEC kuongeza vituo vya kupiga kura

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema inatarajia kuongeza zaidi vituo vya kupiga kura nchi nzima, kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Hatua hiyo ina lengo la kutoa fursa kwa Watanzania, kuwachagua viongozi wao kuanzia madiwani, wabunge na Rais. Kwa sasa kuna vituo 37,814 nchini kote.

Aidha, imebainika kuwa maombi mengi ya wananchi, haki ya kikatiba na kusuasua kwa watu kujitokeza, kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wakisubiri siku ya mwisho ndio sababu ya NEC kuongeza muda wa uboreshaji hadi Februari 23, mwaka huu.

Awali, uboreshaji huo ulitangazwa kuanza Februari 14 na ulitarajiwa kukamilika jana Februari 20 na ulifanyika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, ikiwa ni ya mwisho ya kuboresha daftari hilo nchini, Bara na Visiwani.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk Wilson Mahera aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuwa tume hiyo imeongeza muda wa kuboresha daftari mkoani Dar es Salaam. Alitaka wananchi wenye sifa, kujitokeza kuboresha taarifa zao.

Alisema uamuzi huo wa kuongeza muda, uliamuliwa na NEC katika chake kilichokaa juzi, baada ya tathimini walioifanya kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Dar es Salaam.

Dk Mahera alisema sababu za kuongeza muda ni pamoja na wingi wa watu katika mkoa huo, maombi mengi ya wananchi, sikukuu ya Valentine inayoadhimishwa kila mwaka Februari 14, siku za mapumziko na idadi kubwa kujitokeza juzi, jambo lililoonesha huenda wapo watu wengi hawajajitokeza katika siku hizo saba.

“Tume imeamua na kuelekeza kuwa muda wa zoezi la kuboresha daftari la kudumu katika mkoa wa Dar es Salaam uongezwe kwa siku tatu, ambapo zoezi hilo litakamilika tarehe 23, Jumapili na litaendelea katika vituo vyote kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni,” alisema Dk Mahera. Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi kuhusu idadi ya vituo nchini, Dk Mahera alisema kwa mkoa wa Dar es Salaam vipo vituo 1,961 vya kujiandikisha ikiwa na nyongeza ya vituo 47. Kwa nchi nzima kabla ya Uchaguzi Mkuu, vituo vitaongezwa zaidi ya 37,814 vilivyopo sasa. “Nchi nzima tumeongeza vituo kutoka 36,549 na sasa 37407 Bara, huku Zanzibar kukiwa na vituo 407 kutoka 380.

Jumla tuna vituo 37,814 nchi nzima na vituo vitakuwa vingi zaidi ya hivyo kuwa vituo vya kupigia kura tutakapoweka wazi daftari,” alisema. Mwaka 2015, NEC katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura iliandikisha wapiga kura 23,161,440 nchi nzima.

Mwaka huu wanatarajiwa kuwa wengi zaidi kutokana na vijana wengi kufikisha umri wa miaka 18 kisheria, kama sifa ya kupiga na kupigiwa kura.

Gazeti hili lilishuhudia juzi na jana wananchi wengi wamejitokeza katika vituo vya kuboresha. Katika kituo cha Shule ya Msingi Magole, Kata ya Mzinga, Wilaya ya Ilala, wananchi wengi walijitokeza, wakiwemo wanawake na vijana wenye miaka 18 hadi 22.

Asilimia kubwa walikuwa wanafunzi wa shule za sekondari. Baadhi yao walisema wamefika kujiandikisha, kwa sababu wanataka vitambulisho.

Wengine walisema wana dhamira ya dhati ya kutimiza haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi kwa maslahi ya nchi. Katika Kituo cha Mwanagati, uandikishaji ulionekana kuwa shwari na idadi ya waliokuja kujiandikisha haikuwa kubwa kulinganisha na ile ya Magole. Wengi wao walikuwa ni wanafunzi wa shule za sekondari.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru imewafutia mashitaka washitakiwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha na Anna Mwikola

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi