loader
Picha

Mabilioni yamwagwa ya kujenga barabara Kigoma

SERIKALI ya Tanzania imetiliana saini mkataba na wakandarasi wanne wa kampuni ya ujenzi ya China kwa ajili ya barabara ya kiwango cha lami kutoka Kabingo wilayani Kakonko hadi Manyovu wilayani Buhigwe yenye urefu wa kilometa 260 kwa gharama ya Sh bilioni 584.7.

Waziri wa Ujenzi, Isack Kamwelwe aliongoza viongozi wa Serikali ya Tanzania kushuhudia utiaji saini huo ambao Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale aliongoza utiaji saini huo kwa Serikali ya Tanzania ambao unafanyika kutokana na mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) huku Serikali ya Tanzania ikitoa kiasi cha Sh bilioni 58 kuchangia ujenzi huo.

Akizungumza kabla ya utiaji saini, Kamwelwe alisema ujenzi huo wa barabara ni matokeo ya ahadi aliyotoa Dk John Magufuli wakati wa kampeni za urais mwaka 2015. Alisema aliona ukanda wa magharibi una changamoto kubwa.

Akitoa taarifa kabla ya utiaji saini huo, Mfugale alisema mradi huo wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umegawanywa kwenye vipande vinne kuwezesha ujenzi wake kufanywa kwa haraka na katika kipindi cha miaka mitatu barabara hiyo inapaswa ianze kutumika.

Aliwataja wakandarasi hao kuwa ni Zhejiang Communication Construction Group Co. Ltd iliyopewa kipande cha Manyovu hadi Kasulu kilometa 68.2 kwa gharama ya Sh bilioni 76.1 na Sinohydro Corporation Ltd iliyopewa kipande cha kuanzia Kasulu Mjini hadi Mvugwe wilayani Kasulu kilometa 70.5 kwa gharama ya Sh bilioni 83.7.

Wengine ni STECOL Corporation iliyopewa kipande cha kuanzia Kijiji cha Mvugwe hadi eneo la njia panda ya Kambi ya Wakimbizi Nduta wilayani Kibondo kilometa 59.3 kwa gharama ya Sh bilioni 84.7 na China Hennan International Cooperation Group (CHICCO) kilometa 62.5 iliyopewa kipande cha kuanzia njia panda ya Kambi ya Wakimbizi ya Nduta hadi Kijiji cha Kabingo kwa gharama ya Sh bilioni 95.5.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema atasimamia kwa karibu kuhakikisha fedha za utekelezaji wa mradi huo zinatolewa kwa wakati ili kuwezesha kutekelezwa kwa muda huo uliopangwa.

Dk Mpango alisema ujenzi wa barabara hiyo siyo muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Kigoma na watu wake pekee, bali kwa Taifa kutokana na mkoa kuwa kitovu cha uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa barabara la Afrika; na kuongeza kuwa lazima Tanroads waoneshe weledi wao katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa viwango na wakati huku akionya wakandarasi kutoyumbisha na kuomba kuongezewa muda bila sababu.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema barabara hiyo ni tukio muhimu kwa mkoa huo kwani kuna watu ambao hawajawahi kuona lami hivyo kwao jambo hilo lilileta manung’uko makubwa na kujiona kama siyo sehemu ya Tanzania.

Akitoa neno kwa niaba ya wananchi wake, Mkuu wa mkoa, Emmanuel Maganga alisema kwao mradi huo ni moja ya miradi iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo kwani ni mkoa wa kimkakati kwa ajili ya soko la Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu. Aliwataka wakandarasi kuzingatia kuajiri vijana kutoka mkoani humo katika kazi ambazo hazihitaji utaalamu.

WATU 324 wamewekwa katika sehemu maalumu ya uangalizi, wakiwemo wauguzi ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah, Kigoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi