loader
Picha

Liparamba: Pori lenye simba weupe na tembo ‘wakimbizi’

PORI la Akiba la Liparamba linalopita katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, limejaaliwa kuwa na vivutio ambavyo havipatikani katika hifadhi nyingine nchini.

Liparamba ni hifadhi iliyopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambayo ina wanyama aina ya tembo ambao ni wakimbizi ikiwa na maana kwamba huwa wanavuka hadi hifadhi ya Niassa nchini Msumbiji kisha kurudi Tanzania kupitia pori la Liparamba hadi Pori la Akiba la Selous.

Pori hili pia limebarikiwa kuwa na wanyama adimu aina ya simba weupe ambao hawapatikani pori lingine lolote hapa nchini zaidi ya Liparamba. Meneja wa pori hilo, Ramadhani Issomanga anasema pori hilo la akiba lipo katika ukanda wa misitu maarufu duniani ya miombo ambalo lina viumbe vya kila aina wakiwemo wanyama, ndege, mimea na wadudu.

“Ni mara chache sana hapa duniani kuwepo kwa hifadhi moja ya wanyamapori ambayo inatumika na nchi mbili tofauti. Tanzania tuna bahati kwa kuwa kuna na hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba inayotumiwa na wanyama upande wa Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji,’’ anasema Issomanga.

Anabainisha kuwa pori hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 571, likiwa na eneo la ukubwa kilometa za mraba 11,396 lilikabidhiwa rasmi Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya usimamizi wa Idara ya Wanyamapori Juni 5 mwaka 2006.

Anasema ukubwa wa misitu mizito minene iliyopo katika pori hilo inachangia kupunguza hewa ukaa (CO2) na kwamba pori hilo ni eneo muhimu katika mchakato wa kunyonya hewa ukaa (carbon sink) ambao hupokea mvua za kutosha kwa msimu mmoja tu kwa mwaka.

Issomanga anabainisha zaidi kuwa pori hilo lina mito mikubwa miwili ambayo ni mto Lunyere na Lumeme ambayo inamwaga maji yake katika mto Ruvuma unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi. Anasema pori lipo katika ukanda wa madini, hivyo linaangaliwa kwa umakini dhidi ya uvamizi wa uchimbaji madini.

“Miongoni mwa vivutio adimu ni uoto wa asili wa miti jamii ya miombo zikiwemo aina 60 za miombo, nyasi adimu aina 35, aina 80 za ndege na wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo tembo, simba, chui, parahali, tandala, pundamilia, nyati, kuro, pofu, kima, mamba, kiboko, ngiri na wanyama wengine,’’ anasema Issomanga.

Kwa mujibu wa mhifadhi huyo, pori hilo lina uoto wa asili ambao haujaharibiwa katika ukanda wa wilaya za Mbinga na Nyasa na kwamba pori hilo linatoa matunzo ya tembo wakimbizi kutoka Msumbiji kuja Tanzania na kurudi Msumbiji na kwamba utafiti umebaini wanyama wengine wakifika Tanzania hawarudi Msumbiji.

Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Challe, anasema kuwa pori hilo lina kiwango cha juu cha hifadhi ambacho kinatiliwa mkazo kisheria katika ulinzi, usimamizi, uendelezaji na matumizi ya malihai ikiwemo misitu, samaki na wanyamapori hivyo uhifadhi umejumuisha sekta nzima ya maendeleo ya mazingira, maliasili na utalii kwa gharama nafuu.

“Hili eneo ni la kipekee katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo, lipo karibu na Ziwa Nyasa, wengi watavutiwa na eneo hili kuona msitu mzuri wa asili usioharibiwa sanjari na wanyama adimu wakiwemo chui, simba, palahala na tandala wakubwa,” anasema Challe.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme anatoa rai kwa watanzania na wageni kutoka nje ya nchi kwenda kutalii katika pori la akiba la Liparamba lenye simba weupe na tembo wakimbizi, hali ambayo inaongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii ambayo imeanza kufunguka katika Mkoa wa Ruvuma.

Mndeme anasema licha ya kuwepo wanyama hao adimu, hifadhi ya Liparamba pia ina maporomoko ya maji ya Mto Ruvuma, hivyo ameshauri watanzania kujenga utamaduni wa kutalii katika hifadhi hiyo ili kuona wanyama, ndege, mimea, wadudu na maporomoko ya maji.

Hata hivyo, Mndeme anasema serikali mkoani Ruvuma imejipanga kuufanya mji wa Mbambabay wilayani Nyasa kuwa kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma kutokana na kuwepo vivutio vya aina zote za utalii. Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba anasema milango ya utalii Nyasa imefunguka ambapo hivi sasa siku za mwisho wa juma idadi kubwa ya watalii wanafika Mbambabay hasa baada ya serikali kutengeneza barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay ambapo hivi sasa kilometa 40 kati ya 67 zimekwishawekwa lami.

“Hivi sasa tunapokea watalii wa kutoka nje ya nchi wengi wao wakiwa wanatoka nchi za Uingereza, Ujerumani, India na nchi nyingine za Ulaya na Marekani. Watalii wakitoka Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro wengi wamekuwa wanafika kumalizia utalii wao Ziwa Nyasa,’’ anasisitiza Chilumba.

Anavipongeza vyombo vya habari likiwemo gazeti la HabariLeo kutangaza habari za utalii mwambao mwa Ziwa Nyasa ambapo hivi sasa wanapokea watalii wa nje na wa ndani ya nchi na kwamba wanatarajia baada ya kukamilika mradi mkubwa wa barabara ya lami baadaye mwaka huu idadi ya watalii inaweza kuongezeka maradufu na kufungua fursa za uwekezaji.

Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Nyasa, Bugingo Bugingo anasema Ziwa Nyasa ni kuvutio kikubwa cha Utalii kwa ukanda wa kusini kwa kuwa limesheheni vitu vingi ndani yake na tabia tofauti ukilinganisha na maziwa mengine ya hapa nchini na kwingineko. Anazitaja baadhi ya tabia za ziwa hilo kuwa ni uwepo wa maji meupe na maangavu eneo lote la ziwa na mawe marefu ambayo yanavutia wageni wengi.

“Tabia nyingine ya Ziwa Nyasa ni kuwa na mawimbi makubwa, fukwe nzuri na zenye sifa tofauti, visiwa, mawe kuonekana kama sakafu eneo la Chiwindi, fukwe zenye udongo wa mfinyanzi, kina cha maji kuwa kifupi kwa umbali mrefu na mchanga mdogo ambao watu wa kale walitumia kusugulia meno ili yawe meupe,’’ anasema Bugingo.

Kulingana na mtaalamu huyo, asilimia 15 ya aina za samaki wa maji baridi duniani wanapatikana ziwa Nyasa ambapo kuna aina ya samaki tofauti zaidi ya 600 kutokana na ripoti ya utafiti wa 2011. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ziwa Nyasa lina aina ya samaki wa mapambo zaidi ya 400 na viumbe wengineo ambao hawapatikani katika ziwa lolote duniani.

Utafiti umebaini kuwa tangu mwaka 1960 samaki hao wa mapambo kutoka katika Ziwa Nyasa walianza kuuzwa katika nchi za Ulaya na Marekani, ambapo nchi nyingi kama vile Japan, Sweden, Uturuki, Denmark, Canada, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zilivutiwa na samaki wa mapambo kutoka Ziwa Nyasa kutokana na kuwa na sifa ya kipekee. Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetenga bajeti ya shilingi trilioni moja ili kupanua utalii katika ukanda wa kusini ikiwemo mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni baruapepe albano. midelo@gmail.com, simu 0784765917

WALIMU 151 wa shule za msingi na sekondari Manispaa ya ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi