loader
Picha

Mbaga kwenye historia ya Upare inayosisimua

MWAKA 1918 katika mji wa Heliopolis uliopo karibu na jiji la Cairo, Misri kulipatikana karatasi ndogo katika muswada wa kitabu uliokuwa ukisema yafuatayo: ‘‘Tafadhali hakikisha kwamba muswada huu unaandikwa katika mfumo wa kitabu na kukabidhiwa kwa wananchi wa kabila la Kipare kwa sababu ni historia yao”.

Ujumbe huo ulitekelezwa baada ya miaka 90 ambapo mwaka 2008 kitabu hicho kilizinduliwa katika mji mdogo wa Upareni wa Mbaga. Mtu aliyeandika muswada huo alikuwa ni mateka katika vita ya kwanza ya dunia, aliyetwaliwa kutoka maeneo ya Kusini ya Milima ya Upare, eneo la Mbaga.

Kama mwanaanthropolojia, anapopumzika kufanya kazi zake za kimisionari alitumia muda wake kufanya tafiti mbalimbali zilizohusu mila na tamaduni za watu wa Pare ikiwamo imani zao.

Mmisionari huyu kwa utafiti wake alitoa kitu ambacho kila mtu wa Upareni anakikubali kwamba kweli kimegusa mila na utamaduni wao. Kitabu hicho kilichozinduliwa mwaka 2008 kinachotambulika kama Lute Luvivi-Lwedi (The curse and the blessings) kilichoandikwa na Jacob J.

Dannholz ni moja ya vitu vinavyotambulisha watu wa kabila la Pare tangu miaka mingi iliyopita. Vilima vya Mbaga vipo katika ukanda wa kaskazini wa mpangilio wa milima wa Tao la Mashariki, vikianzia katika uwanda wa Same na kupanda taratibu hadi katika vilima vya Mbaga.

Kukiwa na historia ya uwapo wa Wajerumani hasa majengo yake ya mawe, maporomoko madogo ya maji na ardhi yenye rutuba ya aina yake, eneo hili linatoa taswira nzuri sana kwa mtu anayetaka kuona kijiji cha Kiafrika kilichopendeza. Kutokana na uzuri wake, baadhi ya kampuni za usafiri wa kitalii zinataja eneo hili kama moja ya maeneo muhimu ya kutembelea.

Katika utalii wake huko Mbaga ama unaweza kuamua kupanda milima hadi kwenye msitu wa Shengena kufika kwenye vilele vyake kiasi cha mita 2,460 kutoka usawa wa bahari na kuiangalia mbuga ya Mkomazi na pia kujifunza historia ya mwamba wa Malameni au mapango ya Mkumbavana ama kuona uzuri wa Tona Moorland na mlima Ranzi.

Kiukweli ukifika eneo hilo utaweza kufurahia historia ya Wapare na utamaduni wao na kuona moja ya mbuga yenye vionjo vingi vya mimea ambapo asilimia 90 ya mimea iliyopo Tanzania inapatikana na huku theluthi moja ni ile mimea adimu duniani. Ukifika Mbaga pia utapata maelezo kwamba gari la kwanza kufika Mbaga Manka ilikuwa ni mwaka 1958 likiendeshwa na Ofisa Maendeleo wa wilaya aliyetambulika kwa jina la Bwana H. Mason, ambapo shule ya kwanza kwa ajili ya wananchi wa Kipare ilianzishwa na Wajerumani mwaka 1908.

Mmisionari wa Kijerumani, Dannholz aliandika kitabu kiitwacho In the Bondage of Evil Spirits, katika muda wa miaka 110 aliyoishi Mbaga. Pamoja na historia tamu ya Mbaga, kwa sasa zipo juhudi za kutengeneza miundombinu ya kuboresha utembezi katika maeneo hayo ambapo kuna majengo ya Wajerumani yaliyojengwa kwa mawe (maboma) likiwamo kanisa, hospitali na nyumba mbalimbali za makazi.

Kwenye milima ya Upare ambako imeungana na milima ya Usambara kuna pia maporomoko ya Thornton yenye urefu wa futi 446 ambayo yaliitwa kama kumbukumbu ya Richard Thornton aliyefika eneo hilo akiwa na Mjerumani Baron von Der Decken.

Wavumbuzi hao wa Ulaya walipima anguko la maporomoko hayo na kubaini kwamba yalikuwa futi 446. Mbuga ya Mkomazi ambayo lango lake la kuingilia la Zange lipo kiasi cha kilomita sita kutoka kituo cha mabasi cha Same, ni eneo jingine ambalo mtu anayetaka kuiona Mbaga katika matanuzi yake ataweza kuifaidi.

Katika maeneo haya yote ya Mbaga nyumba ya kupumzikia wageni ya Tona inayotazama mbuga ya Mkomazi ndio kimbilio la watu wanaotaka kutembelea na kufanya tafiti katika mbuga ya Mkomazi ambayo ina vipepeo wengi kama rasilimali kubwa ya utalii. Tona Lodge kwa kuangalia historia kubwa iliyopo katika milima hiyo ya Upare imeanzisha utalii wa asili maarufu kama utalii wa kitamaduni.

Ikiwa katikati ya kijiji cha Mbaga kiasi cha kilomita 130 Kusini mwa Moshi, nyumba hiyo ilianzishwa mwaka 1998 kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Pare kuvuna fedha kwa ajili ya maendeleo ya wakazi wa eneo hilo. Kazi kubwa inayofanywa na Tona Lodge imepongezwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Pare, Dk Charles Mjema. Askofu huyo anasema kwamba utalii wa asili umekuwa chachu ya kufungua maeneo mengi yaliyokuwa hayajulikani kabisa kama vivutio vya utalii, Upareni na kwingineko.

Anamshukuru mratibu wa shughuli za utalii Same, Elly Kimbwereza, kwa kusimamia utalii na hasa wa asili kuleta maendeleo katika eneo la Upareni. Askofu huyo anasema Kimbwereza kupitia Utalli wa Asili alishiriki katika ukarabati majengo na barabara katika zahanati ya Mbaga, Manka iliyojengwa tangu enzi za utawala wa Wajerumani katika vilele vya milima ya Pare Kusini eneo la Mbaga.

Aidha amekuwa akihimiza watu kutambua umuhimu wa eneo la Mbaga kwamba linaweza kujipatia maendeleo kupitia utalii wa asili na hasa kualika Wajerumani kuona walichokiacha takribani miaka zaidi ya 100 iliyopita.

Kiukweli majengo mengi yaliyojengwa enzi za Wajerumani zaidi ya miaka 120 iliyopita bado yapo. Majengo hayo yakiwemo zahanati, nyumba za kuishi watumishi na kanisa lililojengwa wakati mmoja na kanisa la Azania Front lililopo jijini Dar es Salaam, yakiwa bado yanatumika na hivyo kutoa taswira ya kumeremeta kwa utalii wa Mbaga katika milima hiyo ya Upareni.

Kwa upande wake, Elly Kimbwereza anasisitiza katika mazungumzo kwamba uwajibikaji kwa jamii ndiyo sera kuu ya mradi wa Tona kufanikiwa na hasa kutokana na juhudi za kuhakikisha kwamba kila kitu kinachoweza kuuzika kwa utalii wa asili kinajulikana na kinahifadhiwa. Tona Lodge inafanya juhudi za pekee kutoa washawasha ya utalii wa kiikolojia na uhifadhi wa mazingira.

Kutokana na uelewa, Kimbwereza anapigania kuendelea kuwapo kwa msitu wa Shengena ambao umekuwa katika gazeti la serikali kama hifadhi kutoka mwaka 1951. Msitu huu ni muhimu kutokana na kuwa chanzo cha maji Pare Kusini. Ndio chanzo cha mito kama Nakombo, Hingilili, Saseni na Mhoke ambayo humwaga maji mto Pangani.

WALIMU 151 wa shule za msingi na sekondari Manispaa ya ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi