loader
Picha

Licha ya changamoto, Tanzania bado kinara Afrika kuvutia utalii

KUWEPO kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na makazi ya watu katika maeneo ya vivutio vya utalii vya asili ni baadhi ya sababu zinazochochea kushuka kwa ubora wa vivutio vingi vya utalii vya asili.

Hali hii imetokea Tanzania na kuifanya kushika nafasi ya 12 duniani kutoka nafasi ya pili mwaka 2014. Chanzo kikuu kilichochangia kinatajwa kuwa ni uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya hifadhi.

Hiyo ina maana kuwa Tanzania imeporomoka kwa nafasi 10 ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa mujibu wa Ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) ya mwaka 2019.

Ripoti hiyo inayoangazia mazingira wezeshi kwa utalii, miundombinu, maliasili na utamaduni katika nchi 140 duniani iliitaja Tanzania katika nafasi ya 12 duniani kwa ubora wa vivutio vingi vya utalii vya asili.

Ripoti hiyo ya utafiti wa Ushindani wa Safari na Utalii iliyotolewa mwaka 2019 na WEF pia imeeleza kuwa Tanzania bado inashika nafasi ya kwanza barani Afrika, kutokana na kuwepo kwa sera na mikakati madhubuti ya kulinda na kuendeleza rasilimali za asili ambazo zimekuwa zikihitajika zaidi katika kuvutia watalii.

Dalili za Tanzania kuporomoka katika ubora wa vivutio vya utalii vya asili duniani, zilianza kuonekana katika matokeo ya awali ya utafiti wa WEF unaofanyika kila baada ya miaka mitano ambapo, kabla, ilishika nafasi ya nane duniani.

Mei 21, mwaka jana, akiwa bungeni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alisema matokeo ya katikati ya utafiti huo unaofanyika kila baada ya miaka mitano yalionesha kuwa Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya pili mpaka ya nane kwa vivutio vya asili duniani.

Dk Kigwangalla alisema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Vunjo, James Mbatia, na kutaja sababu kubwa iliyosababisha Tanzania kushuka ni kuwepo kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na makazi ya watu katika maeneo ya vivutio vya utalii vya asili.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kazi kubwa imefanyika katika Serikali ya awamu ya tano ya kuwaondoa wananchi ambao wamevamia maeneo hayo lakini pia kupandisha hadhi baadhi ya maeneo ya asili ili yahifadhiwe na kulindwa.

Pamoja na matokeo hayo, bado Tanzania inafanya vizuri katika maeneo mengine ya kuendeleza rasilimali za asili. Ripoti ya WEF, imeeleza kuwa mbali na Tanzania kuporomoka katika ubora wa vivutio vya utalii vya asili duniani, inashika nafasi ya 10 kwa uhifadhi wa maliasili na nafasi ya 18 kwa kuhifadhi na kuendeleza maeneo yake yaliyoorodheshwa katika maeneo muhimu ya urithi wa dunia ikiwemo Pori la Akiba la Selous na Mlima Kilimanjaro.

Ripoti hiyo imechapishwa kwa malengo ya kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, safari na kuwaleta pamoja viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta hii inafikia mahitaji ya miundombinu ya safari na utalii ya karne ya 21.

Pia inalenga kuwasaidia watunga sera kufahamu madhara mbalimbali yanayoweza kuibuka kutokana na sera hizo katika sekta ya utalii na safari hasa katika kufanya maamuzi na uwekezaji. Kwa kuwa bado Tanzania inashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na vivutio vingi vya asili, jambo hili linaendelea kuiweka katika nafasi nzuri ya kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Hii pia imetangazwa na mtandao wa kampuni mashuhuri duniani kwa utalii na vivutio ya safaribookings. com ya nchini Uholanzi, baada ya kuweka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kwa vivutio bora kwa watalii kuvitembelea mwaka 2020. Mtandao wa safaribookings. com ndiyo mtandao mkubwa wa ukuzaji wa safari za Afrika na umekuwa ukifanya tathmini ya zaidi ya wataalamu 2,500 na wale wanaoshiriki katika safari hizo kabla ya kutangaza. Tathmini hizo ziliandikwa na watalii walioenda safari pamoja na wataalamu bingwa wa Afrika.

Mtandao huo unasema kuwa uchanganuzi huo pia ulibaini kwamba Tanzania ilipata umaarufu wake kutokana na idadi ya wanyama mbalimbali, hasa wanyama wakuu watano, maarufu kama ‘Big Five’ wanaopatikana katika mbuga na hifadhi mbalimbali za Tanzania, na wote watano wanapatikana katika Kreta ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mbali na Tanzania, nchi zinazofuatia kuanzia nafasi ya pili barani Afrika ni Botswana, Zambia, Kenya, Afrika Kusini, Namibia, Uganda na Zimbabwe inayoshika nafasi ya nane. Karibu asilimia 40 ya nchi hii inalindwa kwa ajili ya uhifadhi, jambo linalotajwa kuwa linarahisisha kwa safari za kitalii. Mbali na hifadhi ya Serengeti zipo pia hifadhi za Ruaha, Katavi, Rubondo, Ziwa Manyara, Mikumi n.k. kimsingi zipo hifadhi za taifa 16 ambazo zina fursa kubwa za uwekezaji na kuvutia wageni.

Pia ina maeneo mengine muhimu kwa utalii kama mapori ya akiba, fukwe za bahari, maeneo ya kihistoria, milima, maziwa, maporomoko ya maji, mapango n.k. Kwa miaka ya karibuni nchi hii imeshuhudia watu mbalimbali maarufu duniani wakizuru taifa hili ili kutembelea maeneo tofauti ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Hii ni mbali ya makundi ya watalii kutoka China na Israeli wanaotembelea vivutio vyetu mara kwa mara.

Watu maarufu wanaotajwa kwenye ripoti ya mtandao wa safaribookings.com ni mwanamuziki maarufu wa Marekani, Usher Raymond, aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Manchester United na Real Madrid David Beckham, aliyekuwa mchezaji wa Liverpool, Mamadou Sakho, mchezaji wa Everton Morgan Schneiderlin na nyota wa filamu kutoka Marekani, Will Smith na Harrison Ford. Hawa walitembelea mbuga za Serengeti na Mlima Kilimanjaro.

Mtandao huo pia uliitaja Zambia kuwa taifa lenye kivutio kizuri cha misitu huku wataalamu wote wakikubaliana kwamba mazingira ya misitu nchini humo ni mazuri zaidi. Vilevile nchi ya Zambia ilitajwa kuwa taifa lenye maisha bora ya ndege. Namibia na Kenya zilitajwa kuwa bora katika mandhari nzuri pamoja na ndege waliopo.

0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

BUNGE limeridhishwa na upatikanaji wa fedha za kutekeleza mradi wa ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi