loader
Picha

Kina Lugola kesi ya uhujumu yanukia

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), inatarajia kulipeleka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP) jalada la uchunguzi la mkataba wa ununuzi wa vifaa vya jeshi la zimamoto, linalowahusu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola na aliyekuwa Kamishina wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye.

Taasisi hiyo imesema baada ya uchunguzi wao, imebaini kuwa suala hilo linahusiana na uhujumu uchumi, hivyo imeamua kulipeleka jalada kwa DPP kwa hatua zaidi, kulingana na sheria zilizopo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo alisema hatua hiyo imekuja, baada ya kukamilisha uchunguzi wa suala hilo kwa zaidi ya asilimia 99.

Akifafanua, alisema walibaini viongozi hao na wenzao 15, walitenda makosa ya uhujumu uchumi, kwa kuingia mkataba huo wa ununuzi wa vifaa vya jeshi la zimamoto vya zaidi ya Sh. trilioni moja.

“Baada ya maelekezo ya Rais John Magufuli kututaka tufanye uchunguzi huo, mara moja tulianza kukusanya vielelezo na kufanya mahojiano na watu mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, watumishi wa serikali na makampuni husika katika mkataba huo,” alisema Brigedia Jenarali Mbungo Brigedia Jenerali Mbungo alisema kimsingi uchunguzi wao, umebaini kuwa sakata hilo linahusisha uhujumu wa uchumi na taasisi hiyo haiwezi kuwafikisha mahakamani watuhunmiwa hao.

Hivyo, wanachukua hatua ya kulipeleka jalada la uchunguzi huo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka ili aweze kuchukua hatua za kuwafikisha wahusika mahakamani.

“Takukuru inashughulika na masuala yanayohusiana na hongo, uchunguzi wetu uliyafanyia kazi mambo yote yaliyohusiana na mkataba huo hadi ilipokamilisha uchunguzi wake na kubaini kuwa walifanya mambo yote nje ya mamlaka ya kisheria, licha ya uwepo wa miongozo na taratibu za manunuzi.

“Tumesema uchunguzi umekamilika kwa asilimia 99.9 kwa sababu ushahidi muhimu dhidi ya wahusika wa tuhuma hii tayari umepatikana. Kilichobaki ni taratibu za uwasilishaji wa jalada hili la uchunguzi katika Ofisi za Taifa za Mashitaka kwa hatua zaidi,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo .

Aidha, kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Kampuni ya Rom Solution iliyokuwa imeingia mkataba huo na viongozi hao, wameshawasilisha nia ya kuvunja mkataba huo bila masharti yoyote, kutokana na kile kilichojitokeza.

Awali, akielezea kuhusu uchunguzi huo, Brigedia Jenerali Mbungo alisema zaidi ulilenga kuthibitisha iwapo kama kuna uwezekano wa baadhi ya watumishi, kufanya uzembe kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutozishauri mamlaka zao, kuhusu taratibu mbalimbali za usajili wa makampuni pamoja na uzingatiwaji wa sheria ya ununuzi wa umma.

Pamoja na hilo, alisema uchunguzi huo ulilenga kubaini kama kuna makosa ya kushawishi, kuomba au kupokea rushwa kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Lakini, pia, kutaka kujiridhisha iwapo waliosaini makubaliano hayo, kwa niaba ya pande mbili husika, walikuwa na uhalali wa kisheria wa kufanya hivyo.

“Aidha uchunguzi ulitaka kujiridhisha kama kampuni husika, zina uhalali wa kisheria wa kuingia makubaliano yoyote ya kizabuni na taasisi za hapa nchini na kama kuna masuala ya ukwepaji wa kodi halali ya Serikali au ubadhirifu wa mali za umma,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Pia, walitaka kubaini kama kuna matumizi mabaya ya madaraka, kama ilivyotamkwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 Mapema Januari 23 mwaka huu Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Lugola, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Andengenye aliyekuwa Kamishina Jenerali wa Jeshi la Zimamoto, kwa tuhuma ya kuhusika na uingiaji wa mkataba wa ununuzi wa vifaa hivyo.

Kufuatia uamuzi huo, Rais John Magufuli alimteua Geogre Simbachawene kuchukua nafasi ya Lugola. Nafasi ya Andengenye imechukuliwa na Naibu Kamishna wa Mgereza (DCP), John Masunga.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeshauri ujenzi wa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi