loader
Picha

Majaliwa akerwa madai holela ya fidia

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameonesha kukerwa kwake na kitendo cha wananchi wa mkoa wa Kigoma, kudai fi dia ya mamilioni ya fedha, hivyo kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyolenga kuwapatia nafuu wananchi.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi wa mkoa wa Kigoma, kutoa ushirikiano kwa kutoa maeneo bila fidia, kuwezesha miradi mingi kutekelezwa. Alisema hayo alipozungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa Kigoma, kilichofanyika mjini Kigoma jana.

Majaliwa alisema kuwa ipo miradi mingi, ambayo utekelezaji wake ungekuwa umefanyika na kuleta tija na maendeleo kwa wananchi, lakini hadi sasa baadhi ya miradi hiyo haijafanyika. Miongoni mwa miradi ambayo imekumbwa na changamoto hiyo ni ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa eneo la Ujiji mjini Kigoma, ambapo wananchi wanataka kulipwa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kutoa eneo.

Hivyo, mradi huo umekwama kwa sasa. Hata hivyo,Waziri Mkuu alisema serikali imeagiza litafutwe eneo lingine. Hali hiyo pia imekumba Uwanja wa Ndege wa Kigoma, ambao umechelewa kufanyiwa ukarabati, kwa kuongeza njia ya kurukia, kutokana na wananchi kudai fidia kubwa ya makaburi kuliko fidia iliyofanyiwa tathmini.

“Ni lazima wananchi waonyeshe uzalendo kwa kutoa ushirikiano kwa serikali, kwa kutoa maeneo yao kuwezesha kufanyika kwa utekelezaji wa miradi. Miradi hii ni ya kwetu, hivyo tukubali kwamba serikali itumie maeneo hayo bila fidia. Na inapopaswa kutoa, basi angalau fidia inayotolewa wananchi waridhike,”alisema Majaliwa.

Pia aliwataka viongozi wa CCM, kuendelea kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye maeneo yao, ikiwemo kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kuondoa kero na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Alisema kuwa viongozi wakemee wanapoona miradi haijafikia lengo la utekelezaji lililowekwa. Aliwataka viongozi hao kusema kwa uwazi kuhusu jambo hilo na pia wasiache kupongeza, wanapoona ipo miradi imefanya vizuri.

Alisema kuwa ni lazima watendaji na wataalamu wa halmashauri, wazipitie kero na changamoto zinazowakabili wananchi, kwa kuziwekea mipango na kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika.

Kuna mabango yatakuja kwenye mkutano wangu na mikutano mbalimbali ya viongozi. Natoa wito msinyang’anye wala kuyachana mabango hayo. Andikeni kilichoandikwa na kwenda kufanyia kazi kero zinazolalamikiwa” alisema.

Akizungumzia suala la Vitambulisho vya Taifa, Majaliwa alisema kuwa kila mtanzania atapata Kitambulisho cha Taifa. Kwamba uchache wa watumishi na vifaa, ulichangia kuchelewa kwa vitambulisho hivyo na kwamba serikali imeshaanza kufanyia kazi masuala hayo.

Pamoja na hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema uhakiki wa watu wanaopaswa kupata vitambulisho utafanyika, hasa kwa mikoa ya mipakani ukiwemo mkoa Kigoma, kwani kuna mwingiliano mkubwa wa wageni kutoka nchi jirani, wanaoshabihiana na wenyeji. Hivyo, kunapokuwa na shaka, lazima vyombo vya ulinzi na usalama vijiridhishe kwa hilo.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeshauri ujenzi wa ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah, Kigoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi