loader
Picha

Mauzo ya almasi yaipatia Tanzania Dola milioni 89.3

THAMANI ya madini ya vito ya almasi yenye uzito wa carats 416,749.51, iliyouzwa nje kutoka Tanzania katika kipindi cha mwaka 2019 ni Dola za Marekani milioni 89.3.

Katika hilo, mrabaha ulikuwa Dola za Marekani milioni 5.4 na ada ya ukaguzi Dola za Marekani 893,346.02. Madini hayo yanayotumika zaidi katika urembo, yalifuatiwa kwa mauzo na Tanzanite, ambayo kwa soko la ndani mapato yaliyotokana na mrabaha kutokana kwa wachimbaji wadogo, yameongezeka kufikia Sh bilioni 2.9 mwaka 2019 kutoka Sh milioni 70 mwaka 2015.

Hayo yalibainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alipozungumza na gazeti hili jana kuhusu maonesho ya madini ya kimataifa, yanayoanza leo jijini Dar es Salaam, ambapo nchi kumi na mbili zitashiriki maonesho hayo.

Aidha, Kwa mujibu wa Profesa Msanjila, maonesho hayo ya siku mbili yatakayofunguliwa rasmi kesho Jumapili na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, yanahudhuriwa na mawaziri wa madini wan chi hizo 12.

Profesa Msanjila alisema japo hakuwa na takwimu wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopanda kwa uzalishaji na uuzaji wa almasi duniani.

Alisema soko kubwa la almasi liko jiji la Antwerp nchini Ubelgiji, ambako asilimia 80 ya almasi duniani huuzwa hapo. Pamoja na kiwango hicho cha almasi ya Tanzania kuuzwa duniani katika mwaka uliopita, alisema sheria inataka asilimia 5 ya almasi yote inayozalishwa nchini, lazima iuzwe kwenye soko la madini lilipo Shinyanga.

Alisema kupitia soko hilo, wanunuzi wakubwa wa almasi kutoka sehemu mbalimbali duniani, pia hufika kununua almasi katika soko hilo. Madini ya almasi na Tanzanite hutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kutengeneza pete, mikufu, kunakshi mikoba, saa, viatu na kalamu.

Lakini, pia almasi hutumika katika kukata vitu, kung’arishia vitu na kutengeneza vitu vya kucholongea au kutobolea vitu vingine. Akifafanua, kuhusu maonesho hayo, Profesa Msanjila alisema sambamba na maonesho hayo, kitazinduliwa cheti cha uhalisia wa madini ya Tanzanite kinachokidhi vigezo vya kimataifa katika usafirishaji wa madini hayo kote duniani. Alisema cheti hicho kitaonesha kuwa madini hayo ni ya nchi gani na hayatachangia katika umwagaji damu duniani.

“Nchi 12 ikiwemo Tanzania, Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Gambia, Kenya, Uganda, Congo Brazaville, Angola na Msumbiji zitashiriki maonesho haya. Lakini pia mashirika ya kimataifa yakiwemo ya kutoka Marekani nayo yatashiriki,”alisema Profesa Msanjila.

Alisema ujumbe kutoka nchi hizo, utaongozwa na mawaziri wa madini wa nchi husika. Kupitia maonesho hayo, vitu mbalimbali vilivyotengenezwa kwa madini ya vito vitaoneshwa pamoja na teknolojia ya namna ya kuyakata.

Pia, mada mbalimbali zitatolewa. Profesa Msanjila alisema kuwa wachimbaji wa ngazi zote wakiwemo wachimbaji wadogo watashiriki, wadau wa madini na wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya madini nao watashiriki. Mbali na madini ya vito, madini mengine aina ya metali ikiwemo zink, shaba na dhahabu yataoneshwa.

WATU 324 wamewekwa katika sehemu maalumu ya uangalizi, wakiwemo wauguzi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi