loader
Picha

Mechi ngumu zilizotikisa Simba, Yanga

LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea, timu zikiingia mzunguko wa 23 kusaka pointi tatu muhimu katika mbio za kuwania taji kwa msimu wa 2019/2020.

Macho ya watu wengi yamekuwa yakijielekeza kwa mabingwa watetezi, Simba na mabingwa wa kihistoria, Yanga kama wataendelea na ama ushindi au kupoteza. Timu hizo zimekuwa zikifuatiliwa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mashabiki na wanachama hivyo, mmoja akishinda, kupata sare au kupoteza basi kunakuwa maneno mengi ya utani ilimradi kusogeza siku.

Lakini tujikumbushie mechi zilizokuwa na mvuto na ugumu kwa timu hizo kongwe ambazo kwa namna moja au nyingi zilivuta hisia za mashabiki wao hadi kuzungumza sana mtaani.

SIMBA vs YANGA

Mechi ya mzunguko wa kwanza iliyowakutanisha watani hao wa jadi Simba na Yanga haitasahaulika msimu huu kutokana na mambo yafuatayo: Kwanza, kulikuwa na mtazamo kuwa bingwa mtetezi Simba ana kikosi bora kuliko watani zao Yanga na hilo lilionesha kutokana na takwimu za mechi zao za awali.

Mtazamo huo ulisababisha Simba kujiamini ndio maana hata mashabiki wao walijaa kwa wingi uwanjani wakiamini wanaenda kuua mtu lakini matokeo yalikwenda tofauti na matarajio. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Na ilikuwa hivi, zilipokezana vijiti kwani dakika 45 za kipindi cha kwanza wekundu waliongoza katika umiliki wa mpira na bao 1-0. Lakini walivyorudi kipindi cha pili pia wakafunga bao la pili dakika za awali wakaongoza mabao 2-0.

Mashabiki wa Yanga wakiwa wameshakata tamaa kwa kile wanachokiona uwanjani kwa kuongozwa mabao 2-0, haikupita muda mrefu Yanga wakapata bao kisha wakaendeleza mapambano na umiliki na kupata bao la pili. Kitendo cha kurudi na nguvu na kusawazisha kiliwapa furaha mashabiki wao hadi mpira unakwisha matokeo hayo ni kama yalikuwa ushindi na furaha kwa Yanga kuliko Simba kwani hawakuamini kilichotokea.

Furaha ile ilitokana na desturi iliyowahi kujengeka kwa kuangalia baadhi ya matukio ya huko nyuma yakionesha kuwa Yanga akitanguliwa kufunga ni ngumu kusawazisha lakini Simba akitanguliwa ni rahisi kusawazisha.

YANGA vs KAGERA

Hii mechi haitasahaulika katika historia ya Yanga, Kagera akimfunga Yanga mabao mengi tena kwenye uwanja wake wa nyumbani. Labda unaweza kusema mchezo waliofungwa awali na Ruvu Shooting bao 1-0 uliuma kiasi ila huo wa Kagera kwa sababu walifungwa mabao mengi iliwauma zaidi. Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Yanga ilifungwa mabao 3-0.

Ni mchezo ambao hakuna aliyetarajia matokeo hayo. Ni matokeo yaliyowaumiza ila kwa mara ya kwanza Yanga walikubali hawakulalamika kama inavyokuwa miaka ya huko nyuma.

Desturi iliyokuwa huko nyuma Yanga au Simba ikifungwa na timu ndogo ilikuwa ikilalamika sana lakini siku hiyo mashabiki wakiwa na uchungu walisimama katika basi ya wachezaji na kuwapigia makofi ishara ya kukubaliana kuwa ni sehemu ya mchezo. SIMBA vs JKT Huu ni mchezo uliokuwa mgumu kwa Simba iliyofungwa bao 1-0.

Hakuna aliyetarajia matokeo hayo ukilinganisha na viwango vya timu zote mbili lakini ndivyo matokeo yalivyokuwa. Si kwamba Simba ilikuwa haijawahi kufungwa kwani tayari ilikuwa na doa moja baada ya kufungwa mchezo wa awali dhidi ya Mwadui bao 1-0 lakini kwa huo wa JKT walijiamini.

YANGA vs MBEYA CITY

Yanga ilicheza na Mbeya City hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mchezo huo waliotoka sare ya bao 1-1 uliwaumiza wenyeji kwa sababu zifuatazo. Bao la Mbeya City lilikuwa la Yanga waliojifunga kupitia kwa beki wao Lamine Moro. Na wageni hao walikuwa wanacheza kana kwamba hawataki kwa maana ya kupoteza muda lakini kingine wenyeji walikuwa wakishambulia sana lakini ilikuwa ngumu kufunga mpaka dakika karibia za mwishoni ndio wakasawazisha.

Mechi hiyo Yanga ni kama ilitegemea kupata ushindi wa pointi tatu lakini mambo yalikuwa ni magumu kwao tofauti na matarajio na hata ukilinganisha ubora ni timu mbili tofauti.

SIMBA vs PRISONS

Hii mechi walitoka sare 0-0. Ni mchezo ambao Simba walikuwa wanatamani mpira uishe kutokana na kasi waliyokuja nayo wapinzani. Kingine ni kwamba Prisons walikuwa hawajapoteza mchezo wowote hivyo, walikuwa wanajiamini tofauti na walivyochukuliwa na Simba.

YANGA vs PRISONS

Kabla ya kukutana hivi karibuni tayari walikuwa wamekutana mara mbili kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) na ligi na zote Yanga iliwafunga Prisons. Lakini katika mchezo huu, Prisons hawakukubali tena kufungwa walikuja na mbinu tofauti ambazo ziliwabana Yanga na kushindwa kupenya kiurahisi katika ngome yao. Mchezo huu matokeo yalikuwa ni sare 0-0.

Lakini Yanga ilikuwa haina bahati pamoja na kuonesha ubora katika umiliki wa mpira walipata nafasi nyingi wakazipoteza wakapata hadi penalti wakaipoteza pia baada ya Bernad Morrison kuipaisha. Ni mchezo ambao kama ungewapa matokeo mazuri wangekuwa na matumaini ya kusogea kutoka nafasi waliyokuwepo lakini mambo yaliwaendea vibaya.

SIMBA vs POLISI

Mchezo huu ulikuwa mgumu lakini uliishia pazuri. Nusura matokeo yawe sare ya bao 1-1 juhudi za wekundu hao ziliwafanya kupata ushindi dakika za nyongeza yaani ilikuwa inasomeka 95 na wao wakafunga bao la pili na la ushindi na mpira ukaisha.

Mechi hii Simba licha ya kushinda hawatakaa wasahau namna ilivyokuwa ngumu kwao yaani wapigana kweli hadi kupata ushindi kwani wengi walikuwa wameshaanza kuondoka uwanjani wakiamini ni sare. Hizo ni baadhi ya mechi, zipo nyingi tu kwa mfano Yanga na Polisi Tanzania na nyingine nyingi.

MSAJILI Msaidizi wa Vyama vya Michezo Jiji la Arusha, Benson ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi