loader
Picha

Mbowe, Mashinji kuhukumiwa Machi 10

BAADA ya miaka miwili ya vuta nikuvute katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi nane wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji aliyehamia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 10, mwaka huu kutoa hukumu.

Katika kesi hiyo namna 112/2018 mambo mbalimbali yalijitokeza ikiwemo Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko kufutiwa dhamana na kukaa gerezani takribani miezi mitatu hadi Mahakama Kuu ilipotengua uamuzi wa kufutiwa dhamana huku washitakiwa wengine wakionywa na kutakiwa kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana kwa kuruka masharti.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu Chadema na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Iringa mjini Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Ester Bulaya na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema kuwa sheria inaelekeza pande zote (mashitaka na utetezi) kufanya majumuisho ili kuisaidia mahakama kutoa uamuzi kwa kuangalia masuala ya kisheria yaliyoibuliwa wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo.

Alisema wametoa maelekezo kwa pande zote kuwasilisha hoja zao mara baada ya mahakama kukamilisha uchapaji wa nyaraka zilizopo kwenye kesi hiyo na kuwagawia mawakili wa pande zote.

“Natambua kuwa kesi hii ina mvuto kwa jamii hivyo ni lazima iishe ili kila mmoja aweze kuendelea na shughuli zake. Majumuisho ya mwisho mnatakiwa muyawasilishe siku tano za kazi,” alisema Hakimu Simba na kuongeza:

“Hii kesi ina kurasa zaidi ya 1,000 ambazo natakiwa kupitia na kutoa hukumu hivyo hukumu ya kesi hii itatolewa Machi 10, mwaka huu saa 4:30 asubuhi.”

Kabla ya kesi hiyo kuanza, Dk Mashinji alikutana na viongozi wa Chadema ikiwa ni siku chache tangu alipohamia CCM. Dk Mashinji ambaye alifika mahakamani hapo na kuanza kusalimiana na viongozi mbalimbali wa Chadema ikiwemo wale anaoshitakiwa nao isipokuwa Mdee ambaye alikataa kumpatia mkono huku akiendelea kuchezea simu yake ya mkononi.

Pia Dk Mashinji alionana na Mbowe wakiwa ndani ya chumba cha mahakama licha ya kutopeana mikono na mpaka anaondoka mahakamani hapo alikuwa peke yake tofauti na mwanzo.

Mwaka 2018, viongozi hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka 13 ikiwemo ya kufanya mkusanyiko usio halali uliosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru imewafutia mashitaka washitakiwa ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi