loader
Picha

Mvua itumike kukabili njaa

USHAURI kwamba jamii ni vema kutumia fursa ya mvua inayoendelea kunyesha kwa kugeukia kilimo katika kujikwamua kiuchumi na kuondokana na upungufu wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini, haunabudi kupewa kipaumbele.

Tunasema ni muhimu kuufanyia kazi ushauri huo kutoka kwa mtaalamu wa kilimo ambaye pia ni Ofisa Kilimo msataafu wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Aithan Chaula anayejishughulisha na uzalishaji wa mbegu za mazao mbalimbali ikiwemo karanga na mtama.

Chaula katika mahojiano na gazeti hili juzi, anasema mvua kubwa inayoendelea kunyesha, ni baraka kwa wakulima kuitumia kama fursa kuweza kupanda mazao yanayostahimili mvua kubwa.

Mtaalamu huyo katika mahojiano hayo anasema, baadhi ya watu wanatafsiri kilimo kama ni shughuli ambayo hufanywa na watu wa vijijini, tafsiri ambayo imekifanya kilimo mbali na kuimbwa kwamba ni uti wa mgongo, kupendwa na watu wachache na pengine kutothaminiwa kama fursa ya kupambana na umasikini.

Kwa mujibu wa mtalaamu huyo wa kilimo ambaye ni ofisa mstaafu wa serikali anayethamini kilimo hicho kwa kujikita katika ulimaji wa karanga na mtama, sekta hiyo ni bora iheshimiwe na kuboreshwa ili kutoka katika jembe la mkono, kwenda kwenye kilimo cha kisasa.

Anasema baadhi ya wakulima wanahitaji elimu katika kukabiliana na changamoto katika kulima, kupanda, kuvuna na kuhifadhi ili waweze kuzalisha mazao ya kutosha.

Pia anaiomba serikali kupitia maofisa ugani, kusaidia wakulima hasa kwenye maeneo ya vijijini ili waweze kuachana na kilimo cha mazoea.

Nasi tunaungana na mtazamo wake katika kutumia fursa ya mvua ambayo inanyesha katika maeneo mengi ya nchi, ili kukabiliana na uhaba wa chakula na hasa katika baadhi ya maeneo ambayo karibu kila mwaka yanakuwa na shida ya chakula.

Mtaalamu huyo anasema, kutokana na mwaka huu kuwa na mvua za kutosha, hali ya mazao ni nzuri na wakulima wanaweza kulima na kupanda tena kutokana na unyevu uliopo kwenye udongo.

Lakini pia, lazima wataalamu wasaidie kuchanganua aina ya udongo na aina ya mazao yanayoendana na mazao ili kuwawezesha wakulima kufaidi fursa hii.

Ni wakati muafaka wataalamu wa kilimo kutoka maofisini na kwenda mashambani ambako kuna wahusika wanaohitaji ushauri wa kitaalamu.

Kama ambavyo Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba Tanzania ina kila kitu, ni kweli. Tuna eneo kubwa ambalo halijalimwa, maeneo mengi yana rutuba ya kutosha na tuna nguvu kazi ya vijana ambao hawana kazi, hivyo ni vema mvua hii ikawa chachu ya kuondokana na adha ya njaa kwa kutumia kilimo kwa kuwa mvua ipo na ni ya kutosha.

HATIMAYE Benki ya Dunia imetoa mkopo wa gharama nafuu wa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi