loader
Picha

Namna ya kudhibiti viwavijeshi kwenye mazao

VIWAVIJESHI ni larva katika hatua ya ukuaji wa vipepeo wanaodaiwa kuruka nyakati za usiku. Hushambulia mimea na mazao ya aina mbalimbali na kusababisha hasara kwa wakulima.

Viwavijeshi wanaoitwa kwa kizungu, ‘spodoptera frugiperda’ wana asili ya maeneo ya kitropiki ya Amerika, Argentina na maeneo ya Caribbean. Kwa mara ya kwanza, waligundulika Afrika mwaka 2016.

Shirika la Afya Duniani (FAO) linasema walianza kuonekana katika nchi za Benin, Nigeria, Sao Tome and Principe, na Togo. Hadi Januari 30, 2018, viwavijeshi walikuwa wameshagundulika na kutolewa taarifa katika nchi zote za Kusini mwa Jangwa la Sahara isipokuwa Djibouti, Eritrea na Lesotho.

Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, walionekana mwaka 2017 katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa. Mpaka sasa wamefika zaidi ya mikoa 15 ya Tanzania.

Hushambulia mimea na mazao zaidi ya 80, lakini hupendelea zaidi mimea jamii ya nafaka kama mahindi, mtama, uwele, mpunga, shayiri, ngano na miwa na mazao ya mboga.

Mwaka jana wadudu hawa waharibifu wa mazao waliripotiwa kuonekana katika maeneo ya Mtibwa na Dizungu (Turiani) mkoani Morogoro. Tangu muda huo, wataalamu mbalimbali wa kilimo wamekuwa wakifanya tafiti za kuwadhibiti, lakini bado ni changamoto.

Mtaalamu wa Kilimo Endelevu kutoka Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Frank Marwa anabainisha njia madhubuti za kukabiliana na mdudu huyo ili asiangamize mimea kwa kuhamasisha kucheza na muda wa ukuaji wake pamoja na ukuaji wa zao la mahindi.

Marwa ambaye ni Meneja wa Shamba la SAT, lililopo eneo la Vianzi wilaya ni Mvomero katika Mkoa wa Morogoro, anasema wadudu hao wakishambulia shamba wanapunguza uzalishaji kwa asilimia 85 hivyo ni hatari kwa uchumi wa nchi. Anasema kipepeo wa viwavijeshi hutaga mayai mengi ambayo huanguliwa baada ya siku 3-5.

Anasema: “Baada ya mayai kuanguliwa kiluwiluwi (kiwavi) hutokea ambacho huishi kwa muda wa siku 14-28…” Kutoka katika hatua ya kiwavi, buu hutokea ambapo naye hudumu kwa muda wa siku 7-14.

Kutoka katika hatua ya buu ndipo kipepeo kamili hutokea na anaweza kuishi kwa wastani wa siku 14. Kipepeo huruka hadi kilomita 100 kwa siku hivyo huweza kuruka kilomita 2000 katika maisha yake yote huku kipepeo jike akiweza kutaga mayai hadi 2000 katika maisha yake. Kiluilui (larva) ndicho hushambulia mimea na huishi kwa siku 14-28. Kipepeo wa kiwavijeshi huweza kuwa na vizazi 6-12 kwa msimu.

Anabainisha kuwa, akiwa katika hatua ya buu, ni vigumu kumdhibiti kwani huingia ardhini, lakini katika hatua ya mayai na kipepeo kabisa ni rahisi kwani unaweza kuwatega.

Marwa anasema: “Njia madhubuti ya kummaliza ni wakati mahindi yakiwa na majani yasiyozidi 10 kwani ndipo anapoingia na akishaingia, kumdhibiti ni vigumu maana anakuwa ndani ya hindi na kuathiri ukuaji wake kwa kuteketeza mbelewele.”

Kwa mujibu wa Marwa, changamoto ya kumdhibiti inatokana na kuwa ndani, hivyo kila ukipiga dawa haiingii kumfikia hivyo ni vema katika kuwadhibiti wakifika hatua ya kipepeo ili asitage kwa kumwekea mtego wenye protine kisha akifuata anaingia mtegoni.

Aidha anasema, ukiona dalili za maambukizi unapaswa kupiga dawa chini ya majani ya mahindi kwani ndipo wanahifadhi mayai yao yasinyeshewe mvua. Anasema amekuwa akishambulia katika hatua ya uzalishaji wa mahindi kwani ukijua sifa za mdudu ni rahisi kumdhibiti kwa kuhakikisha hatua ya mahindi kuwa na majani 10 unapiga dawa kabla hajaanza kujificha.

Marwa ambaye ni Meneja wa Mafunzo wa Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai (SAT) lililopo katika Kijiji cha Vianzi, Kata ya Lubungo wilayani Mvomelo. Anasema kiwavijeshi ni mdudu msumbufu katika mazao hasa nafaka kama mahindi, mbaazi na ngano na amekuwa akisumbua na wataalamu kushindwa kumdhibiti kwa sababu nyingi hususan kwa zao la mahindi.

Anasema mahindi yana hatua tatu katika ukuaji. Kwanza, mahindi yanakuwa katika hatua ya kuota na majani mawili, pili mhindi kuwa majani 10 mpaka 15 na tatu ni uzalishaji ambapo yanatoa mbelewele. Udhibiti kwa mdudu huyu ili asiharibu mahindi, hufanyika zaidi katika hatua ya pili akiwa hajavuka katika hatua ya uzalishaji kwani hatua hiyo zinakuwa mbelewele ila ziko ndani huwezi kuziona na anatamani kula hivyo uzalishaji ni mgumu madhara yake ni asilimia 85 kupunguza uzalishaji.

“Mdudu huyu anatakiwa kudhibitiwa kabla ya uzalishaji wa mbelewele na dalili zake kama ameingia, kwenye mmea kuna matundu madogo madogo, hivyo inakuwa rahisi kumdhibiti kwa dawa yoyote na ukimwacha, mhindi ukavuka hatua hiyo anakuwa amehama na kuwa na ngozi ngumu hivyo dawa kushindwa kumuua,” anasema.

KUMDHIBITI MDUDU HUYU

Marwa anahimiza wakulima kutumia dawa za asili kwa kuandaa kilo mbili za unga wa mmea aina ya mwarobaini mbichi. Anasema: “Twanga na pilipili kwa kupima mikono miwili ya pilipili kwa makadirio robo unaweka matawi manne ya aloevera.”

“Kama kuna mvua, tumia mafuta ya kula kijiko kimoja cha chakula ili kuleta mnato unaoifanya dawa ibaki kwenye mmea wakati wa mvua na kitunguu swaumu ambacho harufu yake haipendwi na wadudu hivyo kuondoka.”

Anafahamisha kuwa, aloevera huongeza virutubisho katika mmea. Kisha, weka lita moja ya maji na kuacha kwa saa 12 hadi 24. Anasema dawa zote hizo unakadiria kwani hata ikiongezeka haina madhara na katika mchanganyiko huo, lita 20 unatakiwa kuchanganya na maji kwa lita 20 unaongeza lita 10 na kupata lita 30 unazopuliza katika robo ekari.

“Katika kumdhibiti mdudu huyu asiingie kwenye mhindi, unatakiwa kupuliza dawa hii mara kwa mara. Kwa mfano, ukipuliza Alhamisi unatakiwa kupuliza tena Jumatatu ili ikiwa atajaribu kuingia, akute kuna kinga hali itakayomfanya adondoke na kufa kwa kuwa maeneo hayo si rafiki,” anasema.

Anaeleza madhara ya kiwavijeshi katika mmea kuwa ni pamoja na kushambulia majani na kuufanya mmea kushindwa kukua vizuri, kushambulia shina na kuufanya mmea kuanguka na kufa.

Marwa anasema matumizi ya viuatilifu kuwadhibiti husababisha madhara kiafya kwa mlaji kupitia mazao ya mimea (phytotoxicity) na kushambulia mbelewele na kusababisha hali duni ya uchavushaji. Aidha, hushambulia punje na kusababisha mavuno duni huku hali hiyo ikipunguza ubora wa mavuno.

Anabainisha kuwa, kiuchumi wadudu hao husababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kwa kununua viuatilifu ili kuwadhibiti na pia, wanapofanikiwa kushambulia shamba zima, humlazimu mkulima kupanda upya. “Hata serikali inaweza kutumia bajeti kubwa katika mipango ya kudhibiti visumbufu hivyo….” anasema Marwa.

Anaongeza: “Wadudu hawa pia husababisha njaa na hatimaye umaskini kwa wakulima na pengine taifa kwa jumla kwani hata matumizi ya viuatilifu kudhibiti wadudu hawa husababisha uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha gharama nyingine za kutunza mazingira.”

WIKI iliyopita tulianza kuangalia kasumba miongoni mwa jamii kudhani kwamba ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi