loader
Picha

Elimu ya kujitegemea ikizingatiwa uchumi wa viwanda utafanikiwa

ELIMU ya msingi ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya mtoto kitaaluma, kimaadili na ukuzaji wa vipaji mbalimbali. Misingi ya uzalendo, ikiwa ni pamoja na uadilifu, kuthamini na kufanya kazi kwa bidii, hujengwa katika ngazi ya elimu ya msingi. Baada ya kupata uhuru mwaka 1961, Mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius K.

Nyerere, kwa kujua umuhimu wa elimu kwa taifa linalotaka kujitegemea, alianzisha mfumo wa Elimu ya Msingi kwa Wote uliojulikana zaidi kwa jina la UPE. Kupata uhuru ilikuwa kazi ngumu, lakini pia kupata uhuru na kujitegemea kama taifa huru haikuwa kazi rahisi hata kidogo.

Ili taifa liweze kujitegemea, lazima watu wake wawe na elimu bora. Taifa lenye wasomi wazuri hupata viongozi bora, wataalamu mbalimbali na wazalishaji mali wazuri na hivyo, hupiga hatua haraka katika maendeleo.

Hata hivyo, kupata tu elimu haikutosha ilikuwa ni lazima jamii ipate elimu ya kujitegemea kuanzia shule ya msingi. Pamoja na malengo ya elimu ya kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni umaskini, ujinga na maradhi, elimu ya kujitegemea ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.

Mwalimu Nyerere katika harakati zake za kuwakomboa wananchi kiuchumi, kisiasa na kitamaduni alianzisha Somo la Elimu ya Kujitegemea (EK) katika shule za msingi. Elimu hii pamoja na mambo mengine, ililenga kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujitegemea katika kufanya kazi za uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji, ufundi na kazi nyingine kama hizo.

Kila shule ilikuwa na mashamba na bustani za shule kila mwanafunzi alishiriki katika shughuli za uzalishaji mali hapo shuleni. Watoto pia walifundishwa na kujifunza elimu ya upishi, utengenezaji wa vitu mbalimbali. Haya na mengine walijifunza katika masomo ya Sayansi, Sanaa na Ufundi.

Elimu ya msingi enzi za Mwalimu Nyerere, pamoja na kumpatia mwanafunzi taaluma ya kuendelea na masomo ya sekondari, pia ililenga kumfanya mhitimu aweze kujitegemea katika uzalishaji mali na kuendesha maisha kwa wale ambao hawakufanikiwa kwenda sekondari. Hata kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari bado elimu ya kujitegemea iliendelea kutiliwa mkazo.

Katika kuipa elimu ya kujitegemea kipaumbele, kulianzishwa vyuo vya ufundi, sekondari za michepuo ya fundi, kilimo na biashara. Wahitimu wa shule ya msingi baadhi walijiunga na sekondari, huku baadhi yao wakijiunga na vyuo vya ufundi, kilimo, ufugaji na ualimu.

Wanafunzi wote hao walikwenda huko wakiwa tayari na stadi za elimu ya kujitegemea na hata waliobaki nyumbani waliendelea na uzalishaji mali. Vyuo vya ufundi havikuwa na maana kwenda kwa wanafunzi walioshindwa kujiunga sekondari kama wengi wanavyofikiria kwa sasa. Vyuo hivyo vilikuwa mahsusi kwa kutoa mafunzo na elimu ya ufundi kwa vijana katika kujenga nguvu kazi ya taifa.

Pamoja na shule za sekondari za mchepuo ya kilimo, ufundi na biashara, shule nyingine pia zilikuwa na uzalishaji mali kutegemeana na mazingira ya shule husika. Kwa kifupi, kila mwanafunzi shuleni alifundishwa na kushiriki katika kazi za uzalishaji mali. Elimu ya kujitegemea kama falsafa ya Mwalimu Nyerere tangu kuasisiwa kwake mwaka 1967 ilijikita zaidi katika kufuta kusumba za kikoloni na usoni, kuoanisha nadharia na vitendo.

Hata hivyo imesaidia kujenga Watanzania katika utu, upendo, amani, umoja, kujiamini na fahari ya utaifa. Baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha sita na chuo, wanafunzi walijiunga na mafunzo katika kambi mbalimbali za kutoa mafunzo ya kujenga taifa (JKT).

Huko wanafunzi na wanachuo walifundishwa uzalishaji mali, uzalendo, ukakamavu na mambo mengine yanayohusiana ujenzi wa taifa letu kwa jumla. Baada ya kuanza kuwapata wasomi na wataalamu wa Kitanzania, Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuanzisha viwanda vingi nchini. Moja ya viashiria vya nchi kujitegemea kiuchumi ni kuwa na viwanda vingi vinavyozalisha kwa kutumia malighafi za ndani.

Hili, ndilo analolisisitiza Rais John Magufuli tangu aingie madarakani mwaka 2015 akilenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Mataifa yote yaliyoendelea yaliwekeza katika elimu na baadaye kuwa na mapinduzi makubwa ya viwanda.

Ili nchi iweze kuzalisha na kuendesha viwanda vyake na kuinua uchumi wake, lazima itumie malighafi za ndani ya nchi. Ndiyo maana hata Rais Magufuli anatoa msukumo mkubwa kwa watanzania kuendesha kilimo chenye tija ili viwanda vipate malighafi za ndani na hivyo, badala ya kuuza malighafi, Tanzania iuze bidhaa halisi.

Ikumbukwe kuwa, Elimu ya Kujitegemea hutoa wazalishaji bora katika kilimo, ufugaji, uvuvi, na ujasiriamali. Makundi haya yote ni muhimu katika uchumi wa viwanda.

Katika miaka ya hivi karibuni, somo la Elimu ya Kujitegemea limeachwa kutiliwa mkazo shuleni. Wanafunzi wengi wa shule ya msingi na sekondari hawana stadi za elimu ya kujitegemea. Siyo kwa wanafunzi tu, bali hata baadhi ya wazazi wanaona kazi za uzalishaji mali shuleni zinazofanywa na watoto wao ni kama adhabu.

Wengi hawapendi watoto wao wafanye kazi za mikono shuleni. Hili ni kosa linalowaharibia watoto maisha katika siku za usoni nan i hasara kwa taifa. Kibaya zaidi watoto wakiwa nyumbani wengi wao hawafanyi hata kazi ndogo ndogo za mikono, badala yake wanafanyiwa kila kitu na wazazi wao na wengine kufanyiwa kila kitu na wafanyakazi wa ndani.

Wengi tumekuwa na fikra potofu za kudhani shuleni ni kusoma masomo ya kawaida tu, na cha zaidi ni kutaka wanafunzi wafaulu mitihani yao na kupata madaraja ya juu. Faida na umuhimu wa elimu siyo tu kufaulu mtihani kwa kupata alama za juu, bali elimu lazima impatie mhitimu uwezo wa kujitegemea. Shule za msingi na hasa za watu binafsi na taasisi za dini zimekuwa na ushindani mkubwa katika wanafunzi kufaulu mitihani zaidi kuliko kazi za uzalishaji mali shuleni.

Eti sasa limekuwa kosa kubwa kumkuta mwanafunzi katika baadhi ya shule hizi za msingi na sekondari, akifagia darasani hata kumwagilia maua shuleni. Wao shule ni kusoma darasani na si kufanya kazi zozote za mikono. Bila kujali mtoto anasoma shule ya umma ama ya binafsi, wote hawa ni Watanzania ambao hatimaye, watapaswa kujitegemea kwa kuendesha familia zao na katika ujenzi wa taifa kwa jumla.

Kimsingi, elimu ya kujitegemea ni muhimu kwao. Kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere na Tanzania ya viwanda kwa wakati ule, Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza sera ya Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ni ukweli usiopingika kwamba ni ngumu kwa taifa kujitegemea kiuchumi bila kuwa na viwanda vingi vinavyozalisha kwa kutumia wataalamu wengi na malighafi nyingi za ndani ya nchi.

Inatia moyo na kuleta matumaini kuwa serikali imerudisha falsafa ya elimu ya kujitegemea katika mtaala wa elimu ya msingi hali itakayosaidia kuwapa vijana maarifa, ujuzi na moyo wa kupenda kufanya kazi za uzalishaji katika misingi ya kujitegemea. Pamoja na habari hii njema, bado kuna haja ya kupitiwa kwa umakini mtaala huo, na walimu kama wawezeshaji wapatie mafunzo ya kutosha ili kuweza kuendana na yaliyomo katika mtaala huo.

Elimu ya kujitegemea inapaswa kupewa kipaumbele na kufundishwa kwa bidii katika ngazi zote za elimu nchini. Kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu. Uchumi wa viwanda utafanikiwa kwa haraka kama wataalamu na wazalishaji mali watakuwa na maarifa na ujuzi ya kutosha huku falsafa ya kujitegemea ikiwa miongoni mwao.

Taasisi za elimu ya juu pia zina majukumu makubwa katika kufanikisha uchumi wa viwanda majukumu hayo yapo katika kufundisha, kufanya utafiti, kutoa shauri elekezi na kutoa huduma kwa jamii.

Taasisi za elimu ya juu zimekuwa zikifundisha kwa miaka mingi, lakini kinachotakiwa sasa ni kutumia mitaala inayozingatia viwanda. Katika kuandaa na kuhuisha mitaala ni muhimu kuzingatia misingi ya viwanda ili kuwa na wahitimu wanaohitaji sokoni na wanaokidhi vigezo.

Aidha, taasisi hizi zinapaswa kujipambanua vyema katika umahiri katika uchumi wa viwanda ili kila anayetaka kupata suluhu ya changamoto yoyote aliyonayo aipate kwa wakati. Matokeo ya tafiti yasibakie tu kabatini, bali yatolewe kwa wadau wa viwanda ili kusaidia katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda nchini.

Uchumi wa viwanda umelenga kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kufanya taifa kujitegemea. Falsafa ya elimu ya kujitegemea ikitekelezwa kwa vitendo, uchumi wa viwanda utafanikiwa kwa haraka.

Mwandishi ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili. Kitaaluma ni mwalimu. Anapatikana kwa 0755985966

“TEMBO ndiye mnyama anayeongoza kwa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu ...

foto
Mwandishi: Samson Sombi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi