loader
Picha

Wakulima changamkieni fursa hii

VIUATILIFU ni sumu ambayo hutumika kuua, kuangamiza, kufukuza au kuzuia visumbufu katika mimea mashambani. Visumbufu vya mimea vinaweza kuwa wadudu, kuvu (fungasi), magugu na baadhi ya wanyama na ndege.

Kiuatilifu kinaweza kunyunyizwa kwa kutumia bomba la kawaida (sprayer) au kutumia tangi maalumu, lililoshikizwa kwenye trekta au ndege, ili kiuatilifu kiweze kufanya kazi kwa lengo lililokusudiwa. Kwa Tanzania ambayo wananchi wake takribani asilimia 70 wanategemea kilimo kama kitega uchumi, matumizi sahihi ya viuatilifu ni muhimu ili kukifanya kilimo hicho kuwa bora.

Ukweli ni kwamba mazao shambani, haijalishi mazao ya chakula au ya biashara, endapo mkulima asipotumia pembejeo ipasavyo ikiwemo viuatilifu, huweza kuteketea au kuleta uvunaji hafifu kwa kushambuliwa na wadudu.

Taasisi ya Utafiti wa Viutailifu Ukanda wa Tropiki (TPRI), imekuwa ikisimamia na kutoa mafunzo kwa wakulima ya namna ya kutumia viuatilifu sahihi ili kuepusha jamii na magonjwa yatokanayo na matumizi ya sumu za kuulia wadudu waharibifu wanaoshambulia mazao. Kwa mujibu wa taasisi hiyo matumizi mabaya au yasiyo sahihi ya viuatilifu hivyo, husababisha magonjwa kwa walaji wa mazao hayo.

Pamoja na matumizi hayo yasiyo sahihi ya viuatilifu, pia wakulima wa Tanzania wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kununua viuatilifu hivyo feki na kusababisha wapate hasara kubwa, kwa mazao yao kuharibiwa.

Kutokana na hali hiyo, Agosti, mwaka jana Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua Maonesho ya 27 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) kitaifa mkoani Simiyu, aliagiza Wizara ya Kilimo kushughulikia kasoro zilizopo katika upatikanaji wa pembejeo, hasa mbolea, mbegu na viuatilifu ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo.

Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima juu ya kupelekewa pembejeo, ambazo hazina ubora na wakati mwingine kuwafikia zikiwa zimechelewa na kuwafanya wazalishe kidogo.

Hata hivyo, katika kutafutia suluhu suala hilo, taasisi ya TPRI kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), wameingia mkataba wa maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa kuhakiki viuatilifu kwa kutumia simu ya mkononi.

Mfumo huo umepewa jina la ‘T–Hakiki’ ni huduma ya simu ya mkononi, ambayo itamwezesha mkulima kupata taarifa ya viuatilifu, vilivyoajiriwa na kwa matumizi sahihi ili kuleta tija katika kilimo. Utoaji wa huduma hiyo, unatarajiwa kuanza mwezi ujao baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu zinazotakiwa.

Kwa mujibu wa TTCL, mfumo huo utakuwa suluhisho la kuondoa viuatilifu feki sokoni na kuongeza kasi ya matumizi ya viuatilifu sahihi vya kilimo na ufugaji. Jambo la muhimu kwa sasa ni kwa huduma hiyo, kusambazwa nchi nzima huku wakulima wakipatiwa elimu ya jinsi ya kuitumia ili kuweza mapata matokeo chanya.

Hivyo, ni fursa kwao kuchangamkia huduma hiyo na kuitumia ipasavyo ili kuepusha kutumia viuatilifu feki na kuhatarisha maisha yao na mlaji.

IMERIPOTIWA kuwa baadhi ya hoteli kubwa nchini, zimeanza kusitisha huduma ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi