loader
Picha

'Malezi Polisi yameniwezesha kupata PHD'

MAKAO Makuu ya Kanisa Katoliki duniani yalipotangaza kuridhia mchakato wa kumfanya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kuwa Mwenyeheri ikiwa ni hatua ya kuelekea kutangazwa Mtakatifu, watu wengi walishangaa kuwa inawezekanaje mwanasiasa na kiongozi mkuu wa dola kufi kia hatua hiyo.

Hata hivyo, watu na mamlaka mbalimbali za Kanisa zilifafanua zikisema, kuwa mkuu wa nchi au askari au nafasi yoyote katika jamii, hakumzuii mtu kuishi maisha yanayompendeza Mungu kwa kupitia nafasi yake.

Hadi sasa mchakato huo wa Nyerere ambaye sasa kikanisa (Katoliki) ana hadhi ya Mtumishi wa Mungu, unaendelea.

Vivyo hivyo, ndivyo wanavyoshangaa watu wanapomsikia mtu ambaye ni askari, akiwa mchungaji au kiongozi wa dini ingawa kama alivyokuwa akisema Mkuu wa Jeshi (IGP) Mstaafu Said Mwema kuwa, viongozi wa dini wanafanya doria za kiroho kwa binadamu na askari au mamlaka za kiserikali, zinafanya doria za kimwili kwa binadamu huyo huyo.

Kwa msingi huo, inapotokea askari akawa kiongozi wa kiroho (dini) ni jambo jema kwani atatumia karama zake zote kufanya doria ya kiroho na kimwili kwa mwanadamu huyo anayemhudumia. Hili ni jambo jema ingawa waliopo, si wengi.

Vivyo hivyo, mara nyingi watumishi wa serikali hasa viongozi na wanasiasa wengi, ndio husikika kuwa wametunukiwa shahada ya udaktari ya heshima; ni nadra kama ilivyotokea kwa Christina Onyango, askari polisi wa kawaida, kulitumikia Jeshi hadi chuo kikuu nje ya nchi na nje ya Bara la Afrika, kumtambua na kumpa tuzo ya udaktari wa heshima.

Christina Onyango, askari polisi wa kike katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala; ndiye mwasisi wa wazo la kuanzisha kituo cha huduma za pamoja kwa waathitrika wa ukatili wa kijinsia (One Stop Center) katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.

Christina ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima katika Tabia za Binadamu na Utamaduni (utu) kutoka Chuo Kikuu cha Leadimpact cha Colorado nchini Marekani na sasa, ni daktari.

Baada ya maandamano yaliyoongozwa na bendi ya polisi kuingia ukumbini Karimjee, sherehe za kumtunuku shahada hiyo maarufu PhD in Humanity, zikafanyika Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Leadimpact, Askofu Mkuu Dk Cletus Bassay DD katika barua yake ya Januari 16, mwaka huu kwa Christina anasema:

“Digrii ya Udkatari wa falsafa ya heshima, hapewi mtu kwa sababu ya kusoma kwa sababu si ya kitaaluma, bali hutolewa kwa kuangalia mafanikio katika shughuli alizokwishafanya mtu kama utambuzi na shukrani kwa mchango wake katika jamii. Kwetu Chuo Kikuu cha Leadimpact, ni kielelezo chetu cha upendo.”

Barua inasema: “Kwa niaba ya Bodi ya Chuo Kikuu cha Leadimpact USA, ninakuandikia kukupongeza kwa kuteuliwa kupokea Shahada ya Udaktari wa Heshima katika tabia za binadamu na utamaduni (humanity).”

Akizungumza katika sherehe za kutunuku tuzo hiyo, Askofu Mkuu Dk Cletus Bassay DD, anampongeza Rais John Magufuli na Mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere kwa kulijengea taifa misingi imara ya utu.

“Nyerere alisema Waafrika hamwezi kuendelea kama bado mnatawaliwa na fikra za wale wanaowaambia fikra zenu hazifai na ndiyo maana pia nampongeza Rais Magufuli kwa kazi ya kulinda amani na kuchochea maendeleo … Rais wenu anafanya kazi njema sana,” anasema

JESHI LA POLISI

Kutokana na hatua hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa anasema jeshi hilo limeipokea heshima hiyo kwa mikono miwili na kwa heshima kubwa.

“Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tumeichukulia Tuzo ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa ya Heshima kwa uzito mkubwa. Utumishi wake uliotukuka ndio umefanya chuo kikuu cha kimataifa (Leadimpact) kumpaisha na kwa kweli, hata sisi ametupaisha. Polisi tutaendelea kutambua na kuenzi heshima hii aliyotuletea…” anasema Kamanda Mambosasa.

Baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Dk Christina Onyango analipongeza Jeshi la Polisi nchini akisema tuzo hiyo ni matokeo ya malezi bora ya polisi nchini kwa watumishi wake.

“Bila polisi kunipokea na kunipanga katika dawati hilo (dawati la jinsia), na bila polisi kunipa mafunzo na kunilea kiuadilifu, nisingeweza kufikia hatua hii. Kwa kweli ninalishukuru Jeshi la Polisi…” alisema Dk Christina.

TAASISI WANAHARAKATI WA HAKI ZA BINADAMU

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben anazungumzia tuzo ya Christina akisema imemtia moyo na watetezi wengine wa haki za binadamu.

“Mmoja wetu anapofanya jambo jema likaonekana na kutambuliwa na umma, inakuwa ni tuzo yetu sote. Kwa kweli imenitia moyo sana maana inaonesha kazi ya wanaharahadikati siyo ya bure katika jamii,” alisema Rose.

Akaongeza: “Mchango wake umeonekana, umebadilisha na kusaidia jamii hivyo chuo kikuu hicho kimefanya jambo la maana na kuwaonesha wengine kuwa wanaopigania haki za binadamu zikiwamo za watoto na wanawake, hawapaswi kukata tamaa maana umma unatambua mchango wao.”

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WilDAF) Tanzania, Anna Kulaya, anasema: “Christina ni miongoni mwa askari polisi wanaojitoa kwa hali na mali kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na kulinda hjaki za binadamu; kwa kweli, anastahili sana na Tanzania tungepata watu wengi kama Christina katika hili, ukatili wa kijinsia huenda ungekoma.”

WENGINE NAO WAMO

Wengine waliopewa tuzo hiyo ya tabia za binadamu na utamaduni (utu) maarufu PhD in Humanity jijini Dar es Salaam ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Jumaa Mhina na baadhi ya viongozi wa dini wakiwamo kutoka Kenya, Botswana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania.

WANAOTUNUKIWA PhD YA HESHIMA

Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hiyo, Askofu John Bagenyeka, alisema: “Tuzo hii ya shahada ya uzamivu ya heshima katika humanity, hupewa watu waliofanya mambo ya kibinadamu kusaidia wengine kwa kiwango kisicho cha kawaida; waliojitoa sana kuliko wajibu wao, hasa kwa kusukumwa na wito.”

Akaongeza: “Upekee wa huyu ni kwamba ni askari mwanamke mwenye ajira, majukumu na mshahara wake, lakini amejitoa sana kusaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia na kutoa elimu hata kwa viongozi wa dini na makundi mbalimbali; hata makanisa na amekuwa akifuatilia sana kuona waathirika wanasaidiwa ipasavyo…, watu wajue wajibu mkubwa walio nao katika kuwalinda watoto na kupambana dhidi ya ukatili…”

“Hata viongozi wa dini na makundi mbalimbali amekuwa akifuatilia sana kuona waathirika wanasaidiwa ipasavyo….,” alisema Askofu Bagenyeka. Kwa mujibu wa Bagenyeka, tuzo ya shahada ya uzamivu ya heshima katika humanity, hutolewa kwa watu waliofanya mambo ya kibinadamu kusaidia wengine kwa kiwango kisicho cha kawaida kwa kujitoa kuliko wajibu wao, hasa kwa kusukumwa na wito.

ALIYOYAFANYA CHRISTINA

Kwa mujibu wa uchunguzi, miongoni mwa mambo yaliyokifanya Chuo Kikuu cha Leadimpact kumpa tuzo hiyo Christina Onyango, ni pamoja na namna alivyojitoa kutetea haki za binadamu hasa ulinzi wa haki za mtoto na kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Baada ya kutunukiwa, Dk Christina anasema miongoni mwa mambo yaliyosababisha kutunukiwa tuzo hiyo ya heshima ni: “Ni uwezo wangu katika kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, kuelimisha jamii kuhusu aina zote za ukatili na namna ya kuzuia ukatili huo usitokee katika jamii na hasa namna ya kushughulikia matukio na kesi zinazohusu vitendo hivyo.”

Anaongeza: “Chuo kikuu hicho kimetambua mchango wangu katika utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 katika kuzuia ndoa za utotoni, kuzuia vitendo vya ubakaji na ulawiti hasa kwa watoto, kushughulikia kesi za watoto wachanga wanaotupwa baada ya kuzaliwa na kushiriki kikamilifu kuzuia ukeketaji mkoani Dar es Salaam hasa maeneo ya Kitunda wilayani Ilala. Mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini anasema:

“Ni wazi chuo kikuu hicho kimetambua mchango wa Christina ndani ya Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Ilala kama Mratibu wa Maadhaimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili Duniani yanayofanyika kila mwaka.”

Anaongeza: “Christina ameunganisha familia nyingi zilizotengana kwa kurudisha nyumbani watoto waliokimbia familia zao na hata kuwaunganisha wanandoa wengi waliotengana.”

“Amekuwa akiandaa semina na mafunzo mengi katika shule za sekondari, msingi, vyuo na vyuo vikuu na hata katika maeneo ya kazi kuhusu madhara ya rushwa ya ngono katika jamiii na namna bora ya kushiriki… Kwa kweli, ameliongezea heshima jeshi letu la Polisi nchini.”

WIKI iliyopita tulianza kuangalia kasumba miongoni mwa jamii kudhani kwamba ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi