loader
Picha

Nchi yetu iko kwenye mwelekeo sahihi

HAPA nyumbani, huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Rais aliyepo madarakani, Dk John Magufuli anamaliza muhula wake wa miaka mitano ya kwanza ya utawala wake.

Anatarajiwa na umma wa Watanzania, kuwa ataomba tena ridhaa ya wananchi aweze kutuongoza kwenye miaka mingine mitano. Watanzania wanaona kwa macho yao mabadiliko makubwa ya kimfumo yaliyotokea kwenye nchi yao.

Ni mabadiliko yaliyoleta maendeleo ya haraka ikiwamo ukarabati na ujenzi mpya wa miundombinu ikiwamo barabara na reli. Ndani ya miaka hii mitano kumekuwepo pia na utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama vile ufufuaji wa Shirika letu la ndege, ujenzi wa vituo vya afya, miradi ya usambazaji maji vijijini na hata umeme vijijini.

Bila shaka yoyote, Rais wa Awamu ya Tano, Dk Magufuli amesimama upande wa walio wengi na anaonekana, kuwa anakerwa sana na rushwa na ufisadi. Maana, haijapata kutokea kwa miaka mingi, Rais mwenyewe akiwatumbua watendaji wake hata walio waandamizi, mara anapobaini, kupitia vyombo vyake, kuwa wameingia kwenye kashfa za kula rushwa na ufisadi. Ni ukweli, rushwa na ufisadi ni kero nambari moja ambayo umma umeifanya kuwa ajenda ya uchaguzi kwa miaka ya nyuma.

Rais waliyemtaka Watanzania walitaka amaanishe kwa vitendo, kuwa yuko tayari kupambana na rushwa na ufisadi. Na hakika, Rais amelifanya hivyo tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani.

Na kwa kauli na matendo yake, umma wa Watanzania umekuwa nyuma yake katika kumuunga mkono kwenye kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi. Ajenda hii ya kupambana na rushwa na ufisadi, wakati huo huo Serikali kuboresha na kujenga miundo mbinu.

Kusimamia Mpango wa Elimu Bila Malipo na mengineyo, ndiyo masuala yenye kuufanya Uchaguzi Mkuu unaokuja kuwa mwepesi zaidi kwa Rais aliye madarakani na hata chama chake, CCM, ni kwa sababu, chini ya Uenyekiti wake, ameonesha kusimamia nidhamu na maadili ya viongozi, ndani ya chama chake. Na tuwe wa kweli. Rais Magufuli amefanya vema sana kwenye uongozi wake kwa kipindi hiki cha miaka mitano.

Ameonesha kuwa anaaminisha anaposema anachukia rushwa na ufisadi. Tunaona hata serikalini, watendaji wasio waadilifu wanaishi kwa mashaka. Na kwa anavyojitahidi kuwamulika watendaji wengine wenye kuhusishwa na rushwa na ufisadi imesaidia sana kwenye kuleta nafuu ya maisha kwa wanyonge walio wengi. Na haya aliyokuja nayo kwenye Awamu hii ya Tano, yatabaki kuwa ni mapinduzi makubwa kimfumo yatakayobaki katika historia ya kukua kwa nchi yetu kwa karne nyingi zijazo.

Bila shaka, kuna changamoto ndogo na kubwa katika kutekeleza mapinduzi haya, lakini, tuna lazima ya kuzikabili na kuzishinda kwa pamoja kama taifa. Na kuna waliotutangulia kufanya mapinduzi ya kimfumo na wamefanikiwa.

Tuone mfano wa nchi ya Singapore. Imeandikwa, kuwa Singapore, ‘chunusi kwenye uso wa Malaysia ’ ina eneo dogo sana (kilomita-mraba 646 sawa na eneo la Jiji la Chicago, Amerika). Idadi ya watu haifikii milioni tano, ambao wamejigawa ki-uzawa; yaani, wa-Hindi, wa-Malay na wa-China. Zaidi, wamejigawa kidini; yaani, wa-Islamu na wa-Budha. Masuala ya siasa, ubaguzi wa rangi au dini hayaruhusiwi kuwa viini-zungumziwa na wasanii.

Kisiwa cha Singapore kilianza kama kijiji cha wavuvi wachache. Kilijaa mabwawa ya mbu wengi wenye kueneza ugonjwa wa malaria. Bandari na madhari ya ufuko wake kulijaa mitumbwi .

Walevi wa dawa za ‘opium’ walijaa kwenye sehemu walikoishi jamii ya wa-China, ambao walikuwa wakichungulia madirishani na huku wamewaka chakari, mbali ya wacheza kamari na kusheheni biashara ya umalaya na u-shoga (changudoa). Licha ya sifa hizo mbaya, Kisiwa cha Singapore kilikuwa kikishindaniwa kati ya Uingereza na China kutokana na jiografia yake.

Waingereza walikitawala kwa muda wa miaka 149 kwa lengo la kukifanya mahali pa biashara na maghala/soko makubwa kama Hongkong, kwa masoko makubwa ya kikoloni ya kifedha na dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya chini ya China. Mwaka 1963 kilijitawala chini ya Muungano wa Malaya na Majimbo ya Sabah na Sarawak.

Lakini Mungano ulivunjika 1965 kutokana na wa-China na wa-Malaysia kugombana. Vyuo vikuu vilijaa wasomi wa itikadi za mrengo wa kushoto; ma-Komunisti waliingilia vyama vya wafanyakazi; na haikuwa na jeshi la ulinzi. Haikuwa na maliasili na eneo la kuzidi kupanuka; mji mchafu wa kunuka, mifereji ya maji machafu na taka kila mahali na ajira haba.

Zaidi, ilikuwa inaagiza maji na chakula kutoka nje ili kusaidia lishe nchini ingawa ilikuwa na nguruwe, matunda na mboga; majitaka yalinuka kila mahali; na ajira haba sana kiasi cha asilimia 14 na wenye manywele marefu kutapakaa kila mahali. Singapore ilijiuliza maswali mazito: Kama vile inaishi katika ulimwengu wa hali gani? Imetoka, iko na inakwenda wapi? Itilie mkazo mafunzo gani mashuleni ili kuweza kufanikisha ndoto ya maisha bora kwa wananchi wake? Hivyo, kama nchi, iliamua kujijenga ili kujikomboa kutoka madhambi, majuto na mavune ya miaka mingi kabla ya 1960.

Ilipiga marufuku makasino, kamari na kuongeza kodi kwa tumbaku, na vinywaji vikali na kudhibiti biashara ya dawa za kulevya. Ili kudhibiti umaskini na mazoea yasiyo ya maadili mema, serikali ililivalia njuga suala la kupambana na rushwa na ufisadi ili ifanikiwe kupunguza umasikini. Singapore ilianza kufyeka na kujenga upya bandari na madhari yake, ingawa iliashiria kutambulika kama nchi itakayojiunga na maswaiba wa nchi fukara za Dunia ya Tatu. Lakini Singapore ilijinasua kuitwa hivyo. Wafanyakazi walihimizwa kuchapakazi.

Leo hii, Singapore ni bandari-ghala (entrêport) kubwa kwa nchi zote za Australia, New Zealand na Asia Mashariki ya Mbali. Biashara ya huko ni kubwa sana; haiwezi kulinganishwa na biashara inayopita Dar es Salaam kwenda nchi za jirani.

Biashara nchini humo ilikuza miundombinu iliyojengwa kwa ajira ya unyonyaji wa mfumo wa manamba (wa- China, wa-Sri Lanka na wa-Hindi). Wananchi walitokana na mchanganyiko wa mataifa, dini na lugha nyingi, kwa mifano, wa-Uingereza, wa-Hindi, wa-Malalysia, wa-China na wa-Japani; dini nyingi, kwa mifano, wa-Budha, wa-Tao, wa-Islamu, wa-Confucius, wa-Kristo na wa-Hindu); na lugha nyingi, kwa mifano, ki-Ingereza, ki- Mandarini, ki-Malaysia, na ki-Tamili). Lakini leo hii kuna mataifa matatu makubwa” wa-Hindi, wa-China na wa-Malasia.

Waziri Mkuu awamu ya Tatu Lee Hsien Loong alipanua mianya ya biashara. Alitaka Singapore kuingiza mapato zaidi. Aliruhusu watalii, na kuzidisha biashara kwa ajili ya kujenga tabaka la kati bila upendeleo. Singapore ikatajirika kushinda nchi nyinginezo za Asia. Shirika la Ndege (Singapore Airlines) lilinaongoza duniani kwa sifa za juu; kiasi cha asilimia 90 ya wananchi wake wanaishi majumbani mwao; biashara inasheheni bila urasimu, ufisadi na rushwa. Singapore inasifika kwa uwazi na utawala bora huku nikishindana kila mara kuwa ya kwanza; ilikataa kuwa namba mbili.

Kuna majengo marefu na alama za utajiri. Mji ni msafi sana – hakuna uchafu wa mazingira. Bandari yake leo hii inag’aa kwa biashara. Elimu ni ya kiwango cha juu na wengi wameelemika hadi chuo kikuu na wengi wamehitimu elimu-kazi/ ajira kupitia vyuo vya ufundi mbalimbali; wanatumia ‘internet’ ya spidi kali (broadband); kuna uhuru wa biashara na serikali inapendelea wawekezaji; kuna uwazi wa hali ya juu katika fani za kazi na biashara; na hakuna ufisadi na rushwa.

Kuna utawala bora; hakuna upendeleo kazini – wafanyakazi wanaajiriliwa na kupandishwa vyeo kulingana na sifa zao za ujuzi na ufanisi. Wafanyaazi wa umma wanalipwa sawa na wale wa sekta binafsi. Nionavyo, na sisi Watanzania chini ya Dk Magufuli tunaweza kufika mbali, kwa vile, Rais wetu wa Awamu ya Tano anamaanisha kwa vitendo kuwa anachukia rushwa na ufisadi.

UGONJWA wa Corona unaosababishwa na virusi vya ‘Covid 19’ ulianza ...

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

1 Comments

  • avatar
    Daniel Kashuliza.
    05/03/2020

    Ni kweli tunaelekea kwenye mwelekeo Sahihi.!..Fikra zetu vijana zimebadilika na tumeweza kufikiri nje Ya fikra za kawaida.Kuweza kuona fursa kwenye matatizo,Na pia kuwa na uthubutu.Huku tukifanya biashara halali na zinazozingatia sheria.Mtazamo chanya na uthubutu.Asante.

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi