loader
Picha

Nchi za EAC zisikubali majanga mvua zinazoanza mwezi huu

IKIWA ni wiki ya kwanza ya mwezi Machi, ambao Mamlaka za Hali ya Hewa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutabiri kuanza kunyesha mvua kwa miezi mitatu mpaka Mei mwaka huu hadi nchi nyingine kufi ka mwezi Juni.

Katika msimu wa mvua za Machi, Aprili na Mei tayari mamlaka hizo zimetoa tahadhari ya utabiri wa mvua hizo, ambazo hujulikana kama mvua za masika kwa nchi za Burundi, Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda Msemo wa wahenga unaeleza wazi kuwa “Kinga ni bora kuliko tiba“.

Hivyo ni vema kwa namna yeyote kuhakikisha madhara yanayotokana na kunyesha mvua kubwa, yanakingwa kuliko kuyasubiri yatokee. Mamlaka zote zimetahadharisha kunyesha kwa mvua hizo juu ya wastani, kwa maeneo makubwa ya nchi husika. Lakini, kuna maeneo ambayo mvua nje ya msimu, nazo zitaendelea kunyesha kutokana na mabadiliko mbalimbali ya hali ya hewa.

Wakati Mamlaka za hali ya hewa zikitoa utabiri huo, nchi za EAC zimekuwa zikikabiliwa na athari mbalimbali, zilizojitokeza kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kuanzia mwezi Oktoba mpaka Desemba mwaka jana na nyingine zikiendelea kunyesha mpaka mwezi uliopita. Majanga yaliyotokana na mvua hizo ni vifo vya watu kutokana na mafuriko, nyumba kubomoka, watu kuhama nyumba zao, barabara kukatika na hekta za mashamba kuharibiwa na mvua. Nchini Burundi kuna watu 461 wamekufa na zaidi ya 700 kujeruhiwa kwa mvua.

Kwa hapa nchini, nyumba 11,000 na hekta 65,000 zimeharibiwa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana. Hivyo mvua zilizotabiriwa kunyesha, ambazo kwa baadhi ya nchi zitafikia milimita 500, inaonesha dhahiri zitasababisha majanga makubwa zaidi ya zilizopita, hivyo kila mamlaka husika ni vema kuchukua hatua stahiki.

Kati ya hatua ambazo ni vema kuangaliwa ni kuwaondoa wananchi wanaoishi mabondeni ili kuepuka vifo na majanga mengine, lakini pia kutengwa kwa fedha maalum kwa ajili ya kukabiliana na maafa pale inapotokea kukatika kwa barabara au janga lingine ambalo halikutegemewa.

Lakini, pia ni vema mamlaka za serikali za mitaa, kutengeneza mitaro katika maeneo yote ya miji ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi. Lakini, wananchi wakipewa elimu ya kukinga maji kwa ajili ya matumizi ya aina mbalimbali, ikiwemo kuhakikisha hakuna maji yanayosababisha madhara kwa kuelekezwa sehemu stahili.

Kabla ya kuanza kwa mvua hizo, kila mwananchi ni lazima ahakikishe maeneo anayoishi, anafanyia ukarabati maeneo yake, kuruhusu maji kupita, huku nyumba zikifanyiwa ukarabati wa aina mbalimbali.

Lakini, pia vyombo vya usafiri vinatakiwa kuhakikisha wanafuatilia njia wanazopita, hususan maeneo yenye mito ili kuepuka vyombo hivyo kutumbukia majini, huku kukiwa na tahadhari kwa maeneo, ambayo ni korofi, yanayosababisha vifo kila wakati.

Hivyo ni vema kila nchi, kwa kutumia Mamlaka husika, kuchukua hatua kuhakikisha wanakinga majanga kutokea au kuyapunguza, kwa kutumia vifo au uharibifu, uliotokea katika mvua zilizopita na siyo kusubiri majanga na vifo kutokea.

Inaelezwa kuwa utabiri wa Mamlaka hizo, umekuwa na uhakika kwa asilimia kubwa, huku taasisi za hali ya hewa katika nchi za Pembe ya Afrika, zikisisitiza kutabiri mvua hizo nyingi, kama mamlaka za nchi moja moja zilivyofanya. Hivyo, ni lazima kuchukua hatua mapema bila kusubiri majanga.

UGONJWA wa Corona unaosababishwa na virusi vya ‘Covid 19’ ulianza ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi