loader
Picha

Nadharia ya Kant; nia njema ni kila kitu

Wiki iliyopita, tuliichambua nadharia ya Ross ili kuona kwa mtazamo wa nadharia hii, ni mambo gani mtu akifanya yanachukuliwa kuwa kama mambo mazuri na ni mambo gani mtu akifanya yanachukuliwa kuwa ni mambo mabaya ili kuweza kuona ni kwa vipi nadharia hii inaweza kusaidia katika kuyatazama maadili ya utumishi wa umma.

Leo tunaichambua nadharia ya Kant ili kuona kwa mtazamo wa nadharia hii, ni mambo gani mtu akifanya yanachukuliwa kuwa mambo mazuri na ni yapi huchukuliwa kuwa ni mambo mabaya ili vilevile tuweze kuona ni kwa vipi nadharia hii inaweza kusaidia katika kuyatazama maadili ya utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa Kaptein katika chapisho lake “The Ethics of Organizations, A Longitudinal Study of the U.S. Working Population la mwaka 2010 na Wilkinson katika chapisho lake “Principlism and the Ethics of Librarianship” la mwaka 2014 wanabainisha wazi kuwa nadharia ya Kant imejikita katika nia njema (good will) ya mtu husika.

Kimsingi, ili tabia au matendo ya mtu yachukuliwe kama mtendo mazuri, ni lazima yawe yamefanywa kwa nia njema kwa sababu kulingana na nadharia hiyo, hakuna kitu kizuri kama nia njema.

Kwa maana hiyo, tabia au matendo ya mtu yanaweza kuchukuliwa kama mabaya endapo yamefanywa kwa nia mbaya. Kwa mujibu wa Richter katika chapisho lake la mwaka 1992 lenye kichwa cha habari “Combating Corruption” anabainisha kuwa mtu anachukuliwa kuwa na nia njema endapo anaheshimu kanuni za maadili (moral laws) kama wajibu wake kwa sababu kanuni za maadili ndiyo msingi wa mema na mabaya.

Jambo kubwa katika kanuni ya Kant ni kwamba mtu anatakiwa kufanya mambo yanayozingatia kanuni za maadili bila kujali matokeo ya jambo hilo kwake. Kwa mfano ni jambo muhimu kusema ukweli hata kama ukweli huo utakuwa na gharama kwa mtu husika.

Kimsingi, Kant hakutumia nguvu kubwa kutaja ni mambo gani mazuri ya kufanya na mambo gani mabaya ya kuepukwa, isipokuwa aliegamea zaidi katika kufikiri kwa lengo la kutambua mambo mazuri yanayokubalika na mabaya yasiyokubalika kwa kuzingatia hoja bayana zenye mantiki.

Kwa mfano, Fallis katika andiko lake la mwaka 2007 “Information ethics for twenty first century library professionals nadharia ya Kant inataka mtu asitende jambo lolote analoliona liko vizuri kwake mpaka awe na uhakika kwamba anachokifanya kinaweza kuchukuliwa kama kitu kizuri siyo kwake tu bali kwa wote na kwamba kikizingatiwa na wote kinatengeneza kanuni mwafaka za maadili.

Kwa mantiki hiyo, ni jambo zuri kwa mfano, kusaidia watu wengine kutatua matatizo yao. Endapo kila mmoja ataamua kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa matatizo ya wengine yanatatuliwa ni wazi kuwa kusaidia huko kutabakia kuwa tendo zuri lenye kuifanya dunia kama sehemu nzuri ya kuishi.

Kwa upande mwingine endapo mtu atasaidia kwa namna mbaya kama upendeleo ni wazi kuwa endapo upendeleo huo unaendelezwa na wengine matokeo yake yatakuwa mabaya sana kwasababu watu wachache sana watanufaika na kusaidiwa huko kwasababu siyo kila mtu ana mtu wa kumpendelea mahali fulani.

Vilevile kwa mujibu wa Enderle katika chapisho lake la mwaka 1987 lijulikanaolo kama “Some Perspecfves of Managerial Ethical Leadership” nadharia ya Kant inasisitiza kuwa endapo unafanya jambo lolote kwa ajili yako mwenyewe au kwa ajili ya mtu mwingine yoyote lifanye kwa sababu jambo lenyewe ni zuri na lenye utu na siyo kwa sababu unategemea kufaidika baadaye kutokana na jambo hilo.

Kwa kupitia nadharia hii watumishi wa umma wanaweza kujihakikisha kuwa kila jambo wanalofanya linakuwa sahihi endapo lengo lao litakuwa ni kutoa huduma kwa manufaa ya mpewa huduma badala ya kutoa huduma hiyo kwa namna inayofaa kimaadili badaala ya kufikiria kwanza namna wanavyoweza kunufaika wenyewe binafsi kwa kupitia mambo mbalimbali mabaya kama vile rushwa.

Kwa mujibu wa Skidmore katika chapisho lake la mwaka 1995 lenye kichwa cha habari “Ethics and public service” nadharia ya Kant inaendana sana na ajenda za sasa za maadili zinazokubalika za kutengeneza kanuni bora za maadili zinazoweza kutumika kila mahali kwa vigezo vinavyotofautisha mambo mazuri yenye kuzingatia maadili na mambo mabaya ambayo kimsingi yanaenda kinyume na maadili

Kwa muktadha huo, ni wazi kuwa watumishi wa umma wanaweza kunufaika na nadharia hii kama wataitumia kujijengea uwezo wa kutafakari kwa lengo la kuja na hoja za msingi juu ya uhalali wa kufanya mambo fulani kama mambo mazuri na kuacha baadhi ya mambo ambayo yatadhihirika kuwa mabaya hata kama yana manufaa kwao binafsi na kwa taasisi zao.

UGONJWA wa Corona unaosababishwa na virusi vya ‘Covid 19’ ulianza ...

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi