loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tuzingatie sheria kwenda kufanya kazi nje

KATIKA miaka ya karibuni vijana wengi wa Tanzania, wamekuwa wakitafuta fursa mbalimbali kwenda nje ya nchi kufanya kazi kwa lengo la kupata malipo mazuri na kupata ujuzi na teknolojia ya kisasa.

Kwa upande wake, serikali imekuwa ikisisitiza kuwa haijatoa katazo lolote kwa Watanzania kwenda kufanya kazi nchi za nje, bali wanapaswa kufuata taratibu.

Kwamba wanaotaka kwenda nje, wanatakiwa kuwa na nyaraka, kuthibitisha kazi wanayoenda kufanya ili kuiwezesha serikali kuwa na taarifa zao huko.

Tumeguswa na hatua ya serikali ya kuwataka wanaotaka kwenda nje ya nchi, kufanya kazi kuwa na vithibitisho vya kazi wanazozifanya.

Ni muhimu kwa watu hao kuwa na vielelezo hivyo ili kuondoa malalamiko, ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi wanaonyanyaswa nje ya nchi.

Kutokana na ukweli huo, tunaomba kila mtu anayetamani kwenda nje kufanya kazi, awe na vielelezo hivyo kwa usalama na maslahi yake. Kinyume chake ni kuitafuta serikali lawama zisizo na msingi, kwa matatizo ya kujitakia.

Wahenga walisema ‘Kinga ni bora kuliko tiba’, hivyo tuzingatie onyo hilo. Pamoja na nia njema ya watu kutaka kufanya kazi nje ya nchi, wanatakiwa wajue kuwa si kila mtu anayeahidiwa kazi nje, atatendewa haki huko.

Wako baadhi ya wananchi ambao walienda nje mfano nchi za Arabuni na India, wamejikuta katika wakati mgumu kimaisha kutokana na kunyanyaswa.

Ni vyema basi wanaotaka kwenda nje kwa ajili ya kutafuta kazi, wazingatie ukweli huu na kuchukua tahadhari kujilinda na hayo.

Ni kweli serikali iko tayari kuwatetea raia wake pale wanapopatwa na matatizo kokote nje ya nchi. Lakini, hali hiyo isiwe kigezo cha watu kukimbilia holela kwenda nje.

Lazima watu wafuate taratibu za kisheria za ajira, zilizowekwa na serikali ya Tanzania na za nchi wanakokwenda kufanya kazi ili wasidhurike, kupunjwa au kunyanyaswa.

Ni muhimu pia kwa wanaotaka kwenda kufanya kazi nje, wajue fursa nzuri za ajira, haziko nje tu, bali hata hapa nchini zipo tele, mradi tu wawe na sifa na wajitahidi kuzitafuta.

Na kwa sababu hiyo, tunaomba watu wote wenye sifa, watafute kwanza fursa za kazi nzuri hapa nchini, kabla ya kukimbilia nje, ambako kuna matatizo.

Kwa waajiri, tunasema kuondoka kwa watu wa kawaida na wataalam kwenda nje ya nchi kutafuta kazi, ni changamoto kwao, hivyo waboreshe maslahi.

Kwa hakika, ni vema waajiri, kampuni za binafsi na taasisi za serikali, zione hilo na kulifanyia kazi ili kudhibiti utitiri wa wanaoenda nje kufanya kazi, ambao wengine wameishia kuteseka na kunyang’anywa hati zao za kusafiria.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi