loader
Picha

Wanaume waelimishwe kumaliza unyanyasaji

JANA ilikuwa siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo kwa hapa nchini kitaifa iliadhimishwa mkoani Simiyu ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na maelfu ya watu kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye” kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa jamii kuelimishwa kuhusu umuhimu wa uwepo wa usawa wa kijinsia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Binafsi naunga mkono kauli mbiu hii hasa ikizingatiwa kuwa inatoa mwanga juu ya umuhimu wa elimu ya usawa wa kijinsia katika kuleta maendeleo.

Kwa hapa nchini imekuwa ni muda mrefu sasa ambapo kila zikizungumziwa harakati za kumwezesha au kumsaidia mwanamke ushirikishwaji wa wanaume umekuwa ni wa kawaida yaani kama sio muhimu zaidi kushirikishwa katika harakati hizo.

Ifahamike, kuwa kwa asilimia kubwa kila inapozungumziwa ukiukwaji wa haki za wanawake nchini, wanaume ni ndio kisababishi cha kwanza cha ukiukwaji wa haki hizo hivyo kama wakielimishwa namna ya kuukabili unyanyasaji, mafanikio katika kuwawezesha wanawake kushiriki katika shughuli za kimaendeleo yatapatikana kwa haraka zaidi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika linalolenga kuibadilisha jamii kwa kutumia mbinu shirikishi (TIBA), Marcela Lungu katika semina zake za kuwajengea uwezo wanawake, amekuwa akisisitiza kuwa ripoti nyingi kuhusiana na uwezeshwaji wa wanawake hazioneshi kwa kiasi gani wanaume wanashirikishwa katika kuwawezesha wanawake hao.

Anasema, wanaume wakielimishwa namna ya kumsaidia mwanamke kufikia malengo na kisha akashirikishwa katika miradi mbalimbali ya kuwasaidia wanawake ni rahisi kuwana jamii yenye usawa wa kijinsia nchini.

Naungana na Mkurugenzi huyo hasa kuangalia uhalisia wa wanaume wanaofanya shughuli kadhaa ambazo kimsingi zina uingiliano na wasichana na wanaume hao wamekuwa wakitumia nafasi zao katika kazi hizo kuwarubuni wasichana hao.

Hapa nawagusia madereva wa bodaboda na daladala hili ni kundi ambalo lipo kwa ukaribu zaidi na wanafunzi wa kike na ni kundi linalotuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi hao, lakini je likielimishwa na kuhamasisha kuachana na tabia hizo, haliwezi kuwa kundi vinara la kuwasaidia wanafunzi wa kike kusoma?

Hivi karibuni Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki) linalotekeleza mradi wa ushirikishwaji wa madereva wa daladala na bodaboda katika kupigania haki za wanawake katika wilaya ya Kinondoni, limeonesha namna lilivyobadilisha tabia iliyokuwa ikifanywa na baadhi ya madereva wa bodaboda na daladala kutoka kuwa watu wanaotembea na wanafunzi hadi kuwa vinara wa kuwa-saidia wanafunzi hao.

Kwa sasa katika kituo cha mabasi cha Makumbusho mwanafunzi akionekana anazagaa kituoni hapo muda wa usiku wanakuwa na jukumu la kuwafuatilia na kuwalazimisha kurejea majumbani mwao ili kuwaepusha na ubaya unaoweza kuwakuta.

Nashauri harakati kama hizi za kuwashirikisha wanaume kuwa chachu ya maendeleo ya wanawake ziendelee katika ngazi nyingine mbalimbali kama vile kwenye kazi za ofisini, biashara hata katika kilimo ili kuwa na idadi kubwa ya wanaume vinara wa maendeleo ya wanawake. Zianzie shule za sekondari hadi vyuoni ili kuwa na kizazi cha wanaume kinachojua namna ya kumthamini na kumwezesha mwanamke.

MAPAMBANO ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) yanaendelea duniani ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi