loader
Picha

Fursa na upekee wa vyuo vya maendeleo

Katika nchi yetu, vyuo vya maendeleo ya wananchi vina historia ndefu tangu miaka ya 70. Duniani hapa kuna nchi tano tu zenye vyuo vya maendeleo ya wananchi katika mifumo yake ya kiserikali.

Nchi hizo ni Sweden, Norway, Denmark, Finland na Tanzania. Hata Marekani hawana. Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama, alipata kuonyesha nia ya Marekani kujifunza kwa wenye navyo. Ikumbukwe, Mei , 2016, Rais Obama aliwaalika mawaziri wa elimu kutoka nchi za Nordic na katika hotuba yake alisifu wazo la Folk High Schools kwa kusema;

“Rafiki zetu wa nchi za Scandinavia wamefika mbali kwenye eneo la vyuo vya maendeleo ya wananchi. Tuna mengi ya kujifunza kwenye falsafa hii ya elimu endelevu.”

Kwa hapa nchini, moja ya taasisi zisizo za kiserikali zinazofanya kazi na vyuo vya maendeleo ya wananchi ni Shirika la Karibu Tanzania Organization (KTO).

Hapa nyumbani, vyuo vya maendeleo ya wananchi vina nafasi kubwa katika kulipeleka taifa katika uchumi wa viwanda. KTO ni taasisi isiyo ya kiserikali inayofanya kazi na vyuo vya maendeleo ya wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Baadhi ya miradi ambayo taasisi ya KTO inashirikiana na wizara ni pamoja na ‘Elimu Haina Mwisho’, ambayo ni programu ya kuwapatia maarifa na ujuzi wanawake vijana waliokosa fursa hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Vilevile, KTO inaendesha programu ya ‘Mpira Fursa’ inayohusika na kuendeleza mpira wa wanawake na hapa nchini mafunzo hutolewa katika vyuo vya maendeleo ya wananchi na wanawake vijana wanaopata programu hiyo hawajifunzi kucheza mpira pekee, bali pia kupata mafunzo na ujuzi mwingine.

KTO imekuwa kiungo muhimu katika vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi nchini na wizara pamoja na wahisani wa maendeleo kama Sida (Sweden) HDIF (Uingereza) na Mastercard Foundation (Canada) na wengineo wamekuwa bega kwa bega na KTO pamoja na kushiriki katika kuboresha utolewaji wa mafunzo ndani ya vyuo hivyo.

Falsafa ya elimu nje ya mfumo rasmi, ikiwamo uwapo wa vyuo vya maendeleo ya wananchi hapa nchini, kwa kiasi kikubwa imejengwa na Mwalimu Julius Nyerere. Ikumbukwe, Mwalimu alikuwa na visheni kuhusiana na Elimu ya Watu Wazima.

Vyuo vya maendeleo ya wananchi ni taasisi za kiserikali ambazo zipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Vyuo hivi ni maono na mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, baada ya kutembelea nchi ya Sweden mwaka 1969.

Alivutiwa na mfumo wa elimu usiokuwa rasmi ulivyokuwa unaendeshwa na taasisi zinazojulikana kama Folk High Schools. Hivyo basi, vyuo ya maendeleo ya wananchi vilianzishwa mwaka 1975 kama awamu ya tatu ya elimu ya watu wazima.

Lengo lilikuwa ni kuimarisha maarifa na stadi kwa wananchi ili waondokane na ujinga, umaskini na maradhi na hatimaye kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Uamuzi wa kuanzishwa vyuo hivi ulitokana na Waraka wa Baraza la Mawaziri No. 96 wa mwaka 1974, ambapo vyuo 25 vilianzishwa mwaka 1975 na kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Hadi kufikia mwaka 1978, vyuo 53 vilikuwa vimeanzishwa. Ni kwa namna hiyo, uanzishwaji wa vyuo hivyo ulizingatiwa katika Sheria ya Elimu No. 9 ya mwaka 1978 chini ya Wizara ya Elimu.

Kwa sasa kuna vyuo 55 nchi nzima vinavyoendelea kutoa mafunzo ya ufundi (Vocational Trainings), maendeleo ya jamii (Community Development) na elimu ya watu wazima (Adult Education).

Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Dk John Magufuli, imekarabati vyuo vya maendeleo ya wananchi Tanzania ili kuviwezesha kuendelea kutoa maarifa, ujuzi na stadi anuwai kwa watu wa rika zote.

Kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa ambayo nchi yetu iliyapitia, kufikia mwaka 2002, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliandaa “Mwongozo wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi”, ambao unaainisha majukumu ya vyuo hivyo kama ifuatavyo; Vyuo hivi vimekuwa njia mbadala au ‘Altenative Settings’ katika kuwawezesha wanawake vijana kujitegemea kiuchumi, kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye mazingira na hali zao.

Sambamba na hilo, mafunzo haya yatawaandaa kuendelea na mafunzo mengine katika ngazi za elimu ya juu. Vyuo vya maendeleo ya wananchi (Folk Development Colleges-FDC’s) vimekuwa ni sehemu muhimu ya kuendesha mafunzo kwa kuzingatia kuwa vina sifa jumuishi za elimu ya watu wazima, mafunzo ya ufundi na maendeleo ya jamii.

Hivyo basi, chuo kimoja cha maendeleo ya wananchi kama vile Bigwa FDC, Newala FDC au Nzega FDC, kinatoa mafunzo ya taasisi tatu tofauti. Hii ina maana kwamba, kuanzisha chuo kimoja kutapunguza gharama za kuanzisha taasisi nyingine zitakazosimamia mafunzo ya ufundi, elimu ya watu wazima na maendeleo ya jamii. Mitaala na mafunzo hutolewa kwa lugha ya Kiswahili.

Tafiti zinaonesha kwamba, mwanafunzi au mtu anayepokea maarifa mapya huweza kujifunza vizuri kama lugha yake anayoitumia ndio itatumika. Rejea ya Criper na Dodd ya mwaka 1984 juu ya matumizi ya Kiswahili katika mfumo wa elimu Tanzania.

Kwa kutumia lugha ya Kiswahili, vyuo vya maendeleo ya wananchi vimekuwa vikipokea wahitimu wa darasa la saba, walioshindwa kumaliza elimu ya msingi na sekondari na hata wahitimu wa vyuo vikuu wanaohitaji ujuzi kwa ajili ya kujiajiri.

UGONJWA wa Corona unaosababishwa na virusi vya ‘Covid 19’ ulianza ...

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi