loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uamuzi wa BoT uungwe mkono

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imetangaza kuanzisha utaratibu wa kusajili watoa huduma za fedha nchi nzima.

Kupitia utaratibu huo mpya, miongoni mwa wanaotakiwa kujisajili na kupatiwa namba ya utambulisho itakayoanza kutumika Julai mwaka huu ni, mawakala wa benki, mawakala wa pesa kwa njia ya simu za mkononi na mawakala au madalali wa bima.

Wengine ni wakusanyaji wa malipo kwa njia ya kadi (POS), wakala wa hisa za masoko ya mitaji na dhamana, maduka ya kubadilisha fedha na huduma ya kutoa fedha katika mashine za benki (ATM).

Tunaunga mkono uamuzi huu wa BoT, tukiamini kuwa, utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizopo katika huduma za fedha nchini, ikiwamo utapeli wanaofanyiwa wateja kupitia simu za mkononi na kupoteza fedha nyingi.

Hatua hii pia itaondoa tatizo la watoa huduma vishoka ni mawakala wa fedha na bima, ambao wamekuwa wakiliza watu kila siku Tunaaamini utaratibu huu utapunguza changamoto hizo kwasababu, utawezesha kujua maeneo ambayo huduma za kifedha hupatikana nchi nzima na kuonesha eneo ambalo mtoa huduma yupo kijiografia, ili pale litakapotokea tatizo iwe rahisi kumjua na kumpata.

Aidha, utarahisisha na kuzuia tabia ya wizi kwani wakala atakuwa eneo linalotambulika na iwapo atahamia sehemu nyingine itamlazimu kutoa taarifa ili afanyiwe marekebisho kwenye taarifa zake.

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya watu kutapeliwa na kuibiwa fedha zao na baadhi ya watoa huduma wasio waaminifu ambao hushirikiana na wezi na matapeli kufanikisha vitendo hivyo viovu.

Aidha, serikali imekuwa ikipoteza mamilioni ya fedha kila mwaka kutokana na kutokuwapo usimamizi mzuri wa wakusanyaji wa malipo kwa njia ya kadi (POS) na hivyo kutumia mwanya huo kuhujumu mapato yanayokusanywa.

Hivyo, tuna amani kuwa, utaratibu wa kusajili mawakala wa pesa kwa njia ya simu za mkononi, madalali wa bima, wakusanyaji wa malipo kwa njia ya kadi na wengineo wanaotoa huduma za fedha, utakuwa mwarobaini wa kuondoa wizi na utapeli katika huduma hizo muhimu zinazotegemewa na watu wengi nchini.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi