loader
Picha

Wazazi simamieni usafiri watoto wanapokwenda shule

IMEKUWA ni kawaida kuona katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam wanafunzi hasa wa shule za awali au za msingi wakiwa wamepakizwa wawili au hata watatu katika pikipiki wakati wa kwenda au kutoka shule.

Licha ya kuwa ni hatua hatarishi zaidi kwa maisha ya wanafunzi hao hasa ikizingatiwa kuwa mbali na kupakiwa wawili wawili au hata watatu lakini bado pia hawavai kofia ngumu.

Binafsi nikiwa kama mdau wa masuala ya usalama barabarani kupitia vyombo vya habari, nilichobaini hapo ni kuwa kosa linaanzia kwa wazazi au walezi wa watoto husika.

Licha ya kuwa wengine wanaweza kuona kuwa kosa ni la dereva wa bodaboda anayewabeba watoto hao, kwa kuwa yeye anaweza kukataa kuwabeba, lakini wazazi au walezi ndio watu wa kwanza kuanza kuchukua hatua.

Hii inatokana na kuwa wengi wao wanaona kuwa ni gharama kuwakodishia kila mtoto boda boda yake ili awahi shuleni, lakini pia wengine wanaona kuwa ni gharama hata kuwakodishia usafiri wa pikipiki za matairi matatu maarufu kwa jina la Bajaji ambao pengini ni salama zaidi kwa wanafunzi hao.

Hivyo, wanaona kuwa kama Bajaji inawatoza Sh 3,000 wakati boda boda ni Sh 1,000, ni bora kuwapandisha watoto wao wawili wawili katika bodaboda licha ya kuwa ni whatarishi kwa usalama wao.

Napenda kushauri wazazi, walezi na jamii nzima kwa ujumla, kubadili tabia hii ya kuwasafirisha wanafunzi kwa njia ya bodaboda kwa kuwa sio salama kwa maisha yao.

Sina maana ya kuwa usafiri wa bodaboda sio salama kabisa, la hasha, ila huu sio usafiri rafiki kwa wanafunzi tena hao wa shule za awali na za msingi kutokana hasa na udogo wao.

Inasikitisha zaidi kuona baadhi ya waendesha bodaboda hao, licha ya kuwa wamewapakiza wanafunzi hao kwa staili iitwayo ‘mshikaki’, lakini utakuta bado wanakwenda kwa mwendokasi huku wakiyavuka magari bila hata ya kuzingatia utaratibu wa uendeshwaji wa chombo hicho.

Ni muda sasa kwa wazazi na walezi kuzingatia usalama wa matumizi bora ya usafiri wa watoto wao na hata kwa wale ambao wataendelea kuwasafirisha kwa kutumia bodaboda, basi wasipande wawili au watatu kwenye bodaboda moja.

Hata uongozi wa shule husika nao, wasitumie njia hizi hizi, kama mabasi yao yakiharibika. Unapaswa kukodisha daladala kuwabeba wanafunzi hao na sio kuwasafirishia kwa bodaboda.

Pamoja na kuwataka wazazi kuwa makini katika suala hili, lakini bado ni mtambuka, kwa mana ya wazazi, walezi, kikosi cha usalama barabarani, vyombo vya habari na jamii nzima kwa ujumla kutupia jicho la tatu katika kusaidia uboreshwaji wa usafiri wa wanafunzi hao.

Napongeza mbinu inayotumiwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani pale wanapoona wanafunzi wamebebwa mishkaki kuelekea au kutoka shuleni.

Wao hawaikimbizi bodaboda husika kumkamata mwendeshaji, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, wanaweza kusababisha ajali itakayowaumiza wanafunzi, isipokuwa wanaandika namba ya bodaboda kisha kumshughulikia baada ya kushusha wanafunzi hao.

MAPAMBANO ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) yanaendelea duniani ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi