loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Agizo la Rais JWTZ lizingatiwe

RAIS John Magufuli ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwekeza katika teknolojia ili baadaye liweze kuzalisha silaha zake na kutengeneza magari na kuwa sehemu ya mafunzo.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo juzi jijini Dar es Salaam baada ya kuzindua karakana kuu ya JWTZ katika kambi ya JWTZ Lugalo, akisema ni ndoto yake kuliona jeshi hilo siku moja likitengeneza silaha zake lenyewe na kuwaona Watanzania wakinunua magari yaliyotengenezwa na jeshi hilo hapa nchini.

Ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa kuidhinisha Sh bilioni 13 za ujenzi wa Hospitali Kuu ya jeshi itakayojengwa makao makuu ya nchi, Dodoma kuonesha wanavyoheshimu uamuzi wa Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere kuhamishia makao makuu huko.

Hospitali Kuu JWTZ ni Lugalo, Dar es Salaam. Tumeguswa na kauli ya Rais Magufuli kuitaka JWTZ kuwekeza katika teknolojia na viwanda hasa wakati huu wa sera ya serikali ya awamu ya tano ya ujenzi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati 2025.

Ni muhimu sana kwa wapiganaji wetu kuwa mstari wa mbele katika maeneo hayo wakati ambao hawako katika vita, wakati wa amani ili hazina za askari, maofisa kwa wapiganaji wadogo, za ujuzi mbalimbali kutoka vyuo vya ndani na nje ya nchi, zitumike kwa manufaa ya Taifa kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Ikumbukwe Ujerumani ni moja ya nchi wahisani wanaolisaidia jeshi letu kwa teknolojia, vifaa na hata mafunzo hivyo ni matarajio yetu kuwa JWTZ watatekeleza agizo la Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa kujihusisha na ubunifu zaidi katika teknolojia za mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda nchini.

Mpaka sasa JWTZ kama taasisi mama na kupitia kampuni tanzu ya Suma JKT imekuwa ikijihusisha na ushiriki wa uchumi wa viwanda kwa kuzalisha bidhaa za chakula zitokanazo na mahindi Nachingwea na pia ujenzi wa majengo ya serikali na mengine ikiwemo ukuta maarufu wa madini ya Tanzanite Mererani.

Ushiriki wa Suma JKT katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya serikali na mafanikio ya kikosi cha JWTZ Nyumbu cha kuunda magari yanayotumiwa na jeshi hilo na pia magari ya zimamoto ni ushahidi tosha wa uwezo mkubwa wa akili, ubunifu, kujituma, walionao askari wa JWTZ unaostahili kuenziwa.

Ndio maana tunaungana na Rais Magufuli katika ndoto yake kuwa iko siku, kama askari hao na wengine wajao watalelewa vyema kwa kusomeshwa ndani na nje na kuwa na uzalendo kwa nchi yao, wataweza kuunda silaha zao, magari yao na kuwawezesha wananchi kununua magari yaliyotengenezwa nao nchini.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi