loader
Picha

Jamii iandaliwe kujikinga virusi vya corona

UGONJWA wa corona unaotokana na virusi ya Covid-19, unazidi kusambaa katika nchi mbalimbali duniani, huku hofu kubwa ikiwa ni namna ya kuukabili ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya hewa, ambapo iwapo mwenye ugonjwa atakohoa anaweza kuusambaza.

Pia, kama mgonjwa huyo atashika kitu ambacho kitashikwa na mtu mwingine, maambukizi yatatokea. Ugonjwa huo ulioanzia nchini China umesambaa hadi Ulaya, Amerika na nchi nyingine duniani zikiwamo za Afrika.

Kwa nchi za Afrika Mashariki ugonjwa huo umeshathibitishwa kuingia Kenya, ambapo hadi jana kulikuwa na taarifa za mtu mmoja kuambulizwa. Hivyo basi kwa kuwa umeingia Kenya, jirani kabisa na nchi yetu, maandalizi ya kuukabilia yanapaswa kupamba moto.

Hatua ya Rais John Magufuli kuweka msisitizo wa namna ya kukabiliana na Corona wakati akizindua Karakana ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Lugalo juzi, ituzindue na kutupa mkakati mpya wenye kuelimisha wananchi namna bora ya kukabili corona, badala ya kuwaongezea hofu.

Rais amewataka wadau kama vile vyombo vya Habari, wachezesha muziki katika kumbi za starehe, wafanyakazi katika sekta za usafiri kama vile daladala, meli na mabasi ya mwendokasi,kuendelea kutoa elimu ya kukabiliana na corona.

Hakika elimu sahihi ikitolewa, itaiepusha jamii dhidi ya hofu ya corona, hasa hofu eti kuwa kama China na nchi za Ulaya ugonjwa huo tayari umeua watu wengi, hivyo ukija hapa nchini wengi tutakufa.

Hivyo, watu mbalimbali katika jamii wanavyoeneza hofu, huenda inatokana na kukosa elimu ya kukabiliana na corona. Hivyo, sasa ni muda wa kujipanga na kuitoa elimu hiyo kwa ufanisi.

Ni muda kwa vyombo vya habari hasa redio na televisheni, kuweka utaratibu wa kutoa tangazo la elimu ya corona kila baada ya saa kadhaa ili jamii iuelewe ugonjwa huo kwa undani zaidi.

Pia katika ngazi za familia, ni muda muafaka kwa wazazi au walezi, kuzungumzia ugonjwa huo ili elimu iwaingie kwa undani zaidi wanafamilia. Tuielimishe jamii kwa pamoja namna ya kuikabili corona na kuondoa hofu inayoweza kuzorotesha jitihada za kusukuma mbele maendeleo.

MAPAMBANO ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) yanaendelea duniani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi