loader
Picha

Kutolala usingizi wa kutosha hatari kiafya

KUMBE watoto wenye umri wa kuanzia miaka sita hadi 13 wanapaswa kupata usingizi kuanzia jumla ya saa kati ya tisa na saa 11! Ukweli huu niliopata kupitia wataalamu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCD) unanifikirisha.

Nawaza kuhusu hatma ya watoto wa shule. Najiuliza, namna gani familia kwa maana ya wazazi na walezi pamoja na shule zinazingatia kanuni hii ya watoto kupata usingizi wa kutosha.

Napiga picha ya wanafunzi hususani katika jiji la Dar es Salaam ambako hukosi kushuhudia walio kwenye vyombo vya usafiri wakienda shuleni kuanzia saa 10 alfajiri.

Utashuhudia baadhi ya watoto kwenye daladala au kwenye magari ya shule wakisinzia hali ambayo inadhihirisha hali hiyo hujitokeza hata wawapo darasani kutokana na kutotoshelezwa usingizi nyumbani.

Mtoto aliye barabarani kuanzia saa 10 au 11 alfajiri ina maana huamka saa kumi kasoro. Unaweza kujiuliza, mbona kila eneo lina shule ya msingi na sekondari kiasi cha kutoruhusu watoto kusoma mbali na kulazimika kuamka mapema?Jibu ni kwamba, baadhi wanasoma shule za mbali kwa sababu mbalimbali ikiwamo utashi wa wazazi au aina ya shule wanayotaka.

Mathalani, shule za umma zinazofundisha kwa Kiingereza ambazo karibu zote ziko katikati ya jiji, ni miongoni mwa ambazo zimekuwa zikipokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali yakiwamo ya pembezoni. Lakini pia zipo shule binafsi zilizojenga utamaduni wa magari yao kuwachukua watoto mapema sana na kulazimu watoto kuamka mapema.

Baadhi ni zenye magari machache ambazo huanza safari saa 10 alfajiri ambazo huzungukia maeneo mengi.

Aidha, kutokana na baadhi ya shule kuibuka na mtindo wa madarasa ya mitihani kuanza masomo mapema tofauti na muda wa kawaida, watoto wanaoishi mbali na shule hulazimika kuamka mapema zaidi wawahi.

Watoto hao hao ambao huamka kuwahi masomo ya asubuhi na mapema , bado hutoka shuleni wakiwa wamechelewa. Wakati mwingine hupewa kazi za kufanyia nyumbani ambazo zinaweza kuwa sababu mojawapo ya kuchelewa kulala.

Hata hivyo, ikiachwa watoto hawa ambao usingizi wao unaweza kuathiriwa na ratiba za shule, pia lipo kundi linalokosa kulala mapema kutokana na wanafamilia ama kutojali au kutoelewa umuhimu wa kupata usingizi wa kutosha. Kulingana na wataalamu, ili mtoto aamke saa 10 alfajiri anapaswa angalau awe amelala kati ya saa 12 jioni na saa 2 usiku. Tujiulize, je wangapi wanalala muda huo na je wazazi, walezi, shule na jamii nzima inafahamu hilo na inazingatia? Laiti kila mtu angefahamu kwamba kulala usingizi wa kutosha kuna umuhimu mkubwa kiafya siyo tu kwa watoto bali pia kwa watu wazima, familia, shule na jamii kwa ujumla ingeona umuhimu wa kuzingatia saa za usingizi. Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) kupitia kitabu chake cha ‘Mtindo wa Maisha na Magonjwa yasiyoambukiza’linaweka bayana faida za usingizi.

Wataalamu wanaainisha zaidi umri na saa za usingizi zinazostahili siyo tu kwa watoto wa shule bali pia vijana na watu wazima.

Vijana wenye umri wa miaka kuanzia 14 hadi 17 wanapaswa kulala saa nane hadi 10; Watu wazima wenye umri wa miaka 18 hadi 64 wanastahili kulala saa saba hadi tisa na wazee wenye umri wa miaka 65 na zaidi wanapaswa kulala saa saba hadi saa nane.

Wataaalamu wanasema mtu akiwa amelalala, ngozi hujijenga na homoni zinazohusika na msongo wa mawazo hupungua sana hivyo kufanya awe mpya anapoamka.

Kutolala vya kutosha huongeza uwezekano wa kupata na kutodhibiti magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu, unene na sonona.

Kusinzia mara kwa mara hupunguza ufanisi na usalama shuleni na kazini. Wataalamu wanashauri kila mtu ahakikishe anapata usingizi mzuri na unaotosha.

Kwa hiyo wazazi, walezi na shule hazina budi kutambua kuwa watoto wa shule kutolala usingizi wa kutosha ni hatari kwa afya yao.

UGONJWA wa Corona unaosababishwa na virusi vya ‘Covid 19’ ulianza ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi