loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EAC ishirikiane kutokomeza corona

NCHI za Mashariki mwa Afrika zimeanza kampeni kabambe ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona baada ya kuripotiwa kuwepo kwa wagonjwa katika baadhi ya nchi hizo.

Kenya kupitia kwa Rais wake, Uhuru Kenyatta imetangaza kuingia kwa ugonjwa huo na kutangaza hatua mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha kuwa maambukizi ya virusi hivyo yanadhibitiwa kabla ya kuleta maafa makubwa.

Tanzania kwa upande wake nayo kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu pia imetangaza kuripotiwa kwa mgonjwa wa corona na imetangaza hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo.

Katika kuonesha msisitizo, Rais Dk John Magufuli ametangaza kufutwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu na ameagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya mbio hizo kuelekezwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili zitumike kuweka mazingira ya kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo ili visiendelee kuenea kwa watu wengine.

Jitihada kama hizo zimeoneshwa pia na viongozi wa Mataifa mengine ya Afrika Mashariki ya Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Pamoja na kwamba inaonekana kama vile bado maambukizi hayo hayajaenea sana katika mataifa hayo, lakini kwa ujumla wake hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa zinaonesha namna mataifa hayo yalivyojipanga kikamilifu katika kupambana na maambukizi.

Kwa dhati kabisa tunachukua fursa hii kuzipongeza serikali za mataifa ya Afrika Mashariki kwa kuanza kampeni za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona kwa kasi na nguvu kubwa hatua ambayo tuna imani kuwa itasaidia kudhibiti maambukizi yake katika eneo hilo.

Kama wasemavyo waswahili kuwa kinga ni bora kuliko tiba, hatua hiyo ya viongozi wa Afrika Mashariki kuendesha kampeni za kabambe za kupanua uelewa kwa wananchi wake ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona itasaidia sana kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mengi na hivyo kupunguza ukubwa wa madhara kwa wananchi.

Ni kutokana na msukumo wa viongozi hao, ndio maana uelewa dhidi ya maambukizi ya corona umeongezeka sana miongoni mwa raia hivi sasa kuliko ilivyokuwa kabla ambapo wananchi walikuwa wakidhani kuwa ni ugonjwa wa mataifa ya Asia, Marekani na Ulaya na si Afrika wala Afrika Mashariki.

Pamoja na kuwa tayari kumeripotiwa kuwepo kwa wagonjwa katika mataifa hayo ya Afrika Mashariki ni imani yetu kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo hayataachwa kwa nchi moja moja bali yataratibiwa na kuendeshwa na mataifa yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na ukweli kuwa kuna muingiliano mkubwa wa watu wake.

Tuna imani kuwa kama EAC itafanikiwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona ambavyo tayari vimeripotiwa kuwepo, madhara yake yatakuwa madogo na kupunguza vifo lakini pia kutoathiri shughuli za kiuchumi.

TANZANIA itakuwa na ugeni mkubwa wa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi