loader
Picha

Ni wakati wa mshikamano EAC

KUTHIBITIKA kwa virusi vya corona maarufu COVID- 19 katika baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni ishara kuwa jumuiya hiyo kwa ujumla si salama na kwamba kinachohitajika sasa ni mshikamano miongoni mwa nchi wanachama ili kuhakikisha kuwa kirusi hakisambai kwa nchi nyingine.

Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mataifa matatu ambayo yamethibitisha kuwepo kwa wagonjwa wa corona, Kenya ambayo raia wake aliyetokea nchini Marekani akipitia London, Uingereza alipatikana na corona Machi 5 mwaka huu na mpaka kufikia jana, idadi ya wagonjwa iliongezeka na kuwa watu watatu.

Rwanda ndilo taifa la pili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuripoti mgonjwa mmoja ambaye ni raia wa India aliyetokea Mumbai na alithibitika kuwa na virusi vya corona Machi 14 mwaka huu.

Na tatu ni hapa nchini ambapo Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu aliueleza umma jana kuwa mtu mmoja tayari alikutwa na ugonjwa huo kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro.

Nchi zote hizo zimechukua hatua zinazofanana katika kukabiliana na kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.

Mpaka sasa nchi za Kenya na Rwanda zimefunga shule zote pamoja na sehemu za kuabudu huku wasafiri kutoka nje hasa mataifa yaliyoathirika wakizuiwa kwa muda.

Kinachotakiwa hapa sasa ni kushirikiana kwa nchi zote za Afrika Mashariki ili kusaidia virusi visisambae katika mataifa mengine ambayo bado hayajapata kama vile Uganda, Sudan Kusini na Burundi.

Nasisitiza kuhusu ushirikiano kwa sababu virusi kutoka nchini Kenya kuja Tanzania ni rahisi na kutoka Rwanda kwenda Uganda pia ni rahisi kutokana na muingiliano uliopo unaorahisishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bila ushirikiano wa karibu wa mataifa haya itakuwa ni rahisi kwa virusi vya corona kusambaa kwani hata Waswahili waliwahi kusema Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Tahadhari inayochukuliwa nchini Rwanda na Kenya inapaswa kuchukuliwa pia katika mataifa mengine ambayo hayajapata virusi hivyo vya corona. Mfano kuweka dawa maalumu ya kunawa mikono kabla ya kuingia katika usafiri wa umma.

Hatua zingine ni pamoja na kuhakikisha hakuna abiria anasimama katika usafiri wa umma kwamba wote wakae katika siti watulie huku wakiwa wamenawa mikono kwa maji na dawa maalumu ya kuua vijidudu.

Vile vile kuzuia wasafiri wanaowasili kutoka katika mataifa yaliyoathirika na corona pamoja na kuwaweka karantini ya siku 14 abiria wote kutoka nje ya nchi ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Mpaka kufikia jana, Kenya ndiyo ilikuwa ikiongoza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa na watu watatu wanaougua ugonjwa huo hatari. Rwanda ni taifa la pili katika Afrika Mashariki ikiwa na mgonjwa mmoja hadi jana ikifuatiwa na Tanzania yenye mgonjwa mmoja pia.

Wananchi tunatakiwa kuwasikiliza viongozi wetu na kutii maelekezo yao ili kuhakikisha kuwa hata katika nchi ambazo hazijapata wananchi wafuate maelekezo kuhusu ni kitu gani cha kufanya.

Wananchi katika nchi hizo tunatakiwa kutoa ushirikiano wa moja kwa moja kwa viongozi wetu pale tunapowaona watu na kuwatilia mashaka tutoe taarifa katika mamlaka zinazohusika.

Mpaka jana ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu zaidi ya 6,000 na wengine zaidi ya 150,000 wameambukizwa kote duniani huku wagonjwa zaidi ya 70,000 wametibiwa na kupona.

MAPAMBANO ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) yanaendelea duniani ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi