loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukweli corona uelezwe bila kuzua hofu

WAKATI tayari Tanzania imeripotiwa kuwa na mgonjwa mwenye virusi vya corona, kumekuwepo na mijadala inayotofautiana ya namna vyombo vya habari vinavyopaswa kufikisha taarifa juu ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo kwa jamii.

Pande mbili katika mjadala huo zimekuwa zikitofautiana kwa pande moja kueleza kuwa ni vizuri kama taarifa zitakuwa zikifikishwa kwa umma kwa vyombo vya habari kuelezea ukweli au uhalisia wa ukubwa wa tatizo, huku upande wa pili ukisimamia msimamo kuwa uhalisia au ukweli uelezwe lakini kwa busara.

Upande unaosisitiza umuhimu wa wananchi kuelezwa ukweli na uhalisia bila suala la busara kuzingatiwa, unadai kuwa endapo jamii itaelezwa ukweli bila kupepesa itasaidia watu kuona ukubwa wa tatizo na hivyo kuchukua hadhari kubwa zaidi, huku upande unaosisitiza busara ukidai kuwa wananchi wakielezwa bila busara kuzingatiwa kunaweza kuzua hofu na madhara makubwa zaidi kujitokeza.

Kwa upande wake akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam juzi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema vyombo vya habari vieleze jamii na kutoa elimu kuhusu corona bila kupotosha na bila kuzua hofu.

Waziri Ummy alisema pamoja na kwamba tayari ugonjwa huo umeripotiwa kuingia nchini, lakini zipo hatua zinachukuliwa na serikali katika kuhakikisha kuwa unadhibitiwa ili usisababishe madhara makubwa na hivyo hakuna sababu kwa vyombo vya habari kuzua taharuki kwa jamii zaidi ya kutoa elimu ya namna ya kujilinda.

Tunaungana na Waziri Ummy katika kuvihamasisha vyombo vya habari nchini kuandika uhalisia na ukweli wa maambukizi ya ugonjwa wa corona kwa kutumia busara na hekima, kwani hatua hiyo pamoja na kuwa itapunguza hamaki katika jamii lakini pia itatoa nafasi kwa wananchi kuwa na utulivu wa moyo na akili katika kupokea maelekezo, elimu, maoni na ushauri wa namna ya kujikinga.

Kama vyombo vya habari vitafikisha taarifa kwa umma katika mwelekeo utakaosababisha au kuzua hofu ni wazi kuwa hata lengo zima la mapambano dhidi ya virusi vya corona halitafikiwa kwani jamii yenye hamaki na isiyo na utulivu wa akili hushindwa kupokea maarifa kwa kiwango kinachotarajiwa.

Kwetu sisi mbali ya kuona kuwa busara na hekima ndio njia sahihi ya kufikisha habari za maambukizi ya corona kwa wananchi, lakini pia tunadhani kuwa njia hiyo ndiyo itakayotoa dira na mwelekeo kwa vyombo vya habari vya kimataifa vinavyotegemea vyombo vya ndani kama vyanzo vyao vya habari, kuripoti taarifa sahihi na kwa mwelekeo sahihi kuhusu hali ya maambukizi bila kutia chumvi.

Kama hilo litafanyika na kufanikiwa ni wazi kuwa hakutakuwa na athari kubwa kiuchumi, kwani kama nchi tutaendelea kupambana na ugonjwa huo huku tukitekeleza mipango yetu ya kiuchumi bila hofu.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi