loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanafunzi watumie vizuri siku 30 nyumbani

KATIKA kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, serikali imetangaza kuzifunga shule zote za awali, msingi, sekondari na vyuo kwa kipindi cha siku 30.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akieleza mikakati mbalimbali inayochukuliwa na serikali ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, baada ya kuripotiwa kuwepo kwa wagonjwa nchini.

Waziri Mkuu amesema wanafunzi wa kidato cha sita, walipaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020, lakini nao pia watapaswa kusubiri wizara ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.

Alisema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima, imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali, ikiwemo shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.

Kutokana na agizo hilo la Waziri Mkuu, wanafunzi wengi wamerejea majumbani na wachache hususani wa vyuo vya elimu ya juu waliokuwa katika mitihani, wamesalia vyuoni wakikamilisha taratibu za kielimu kabla ya kurejea majumbani.

Ingawa familia zitakuwa zimeelekeza macho na masikio yao katika kuwakinga watoto dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, ni jukumu letu kuwakumbusha wazazi pia kuwa makini katika kuhakikisha kuwa watoto wao, wanatumia muda mwingi kusoma na kujifunza wakiwa nyumbani.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kuwa wapo wanafunzi hususani katika vyuo na kidato cha sita, ambao walikuwa wameanza mitihani na wengine walikuwa katika maandalizi ya kuanza mitihani, lakini sasa wamelazimika kurudi nyumbani.

Inawezekana wanafunzi hao, wakapewa muda zaidi wa kujiandaa, baada ya maambukizi kudhibitiwa na wao kurudi masomoni, lakini inawezekana pia muda utakaoongezwa usitoshe kujiandaa vizuri katika mitihani.

Njia pekee ya kuwafanya wanafunzi kufaulu mitihani yao na wasio na mitihani kuendelea vizuri na masomo, ni kwa wanafunzi wote kutumia siku 30 ya mapumziko, kusoma kwa bidii na kurejea mambo yote waliyojifunza darasani na hivyo kuwa tayari kwa lolote.

Hivyo moja ya majukumu ya wazazi katika kipindi cha siku 30 zijazo wakati watoto wakiwa majumbani, itakuwa ni kuwasimamia watoto ili kuhakikisha kuwa wanasoma kwa utulivu, bila ya kuwa na hofu yoyote na hivyo kuwa na maarifa makubwa.

Pamoja na hilo, ni matumaini yetu pia kuwa wazazi watakuwa makini katika kuhakikisha kuwa wakati wakiwa katika harakati za kujifunza wakiwa nyumbani, watoto hawajiingizi katika mikusanyiko hatari, ambayo inaweza kuwafanya kuambukizwa virusi vya corona.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi