loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wamiliki mabasi wasaidie kudhibiti msongamano

PAMOJA na kuchukua hatua mbalimbali ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona nchini, serikali pia imezuia msongamano wa abiria kwenye vyombo vya usafi ri.

Juzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumzia suala hilo, alisema hakuna haja kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri, kuwajaza sana abiria kwenye mabasi, isipokuwa wale tu waliopo kwenye siti.

Alisema abiria wakishajaa na kukaa kwenye viti, magari yote yaondoke vituoni. Pamoja na kwamba tayari serikali imetoa agizo hilo, katika maeneo mbalimbali nchini, imeripotiwa kuwepo kwa mabasi na vyombo vingine vya usafiri, vinavyobeba abiria wengi kuliko inavyostahili.

Ni kutokana na matukio hayo, ndio maana tumeona uwepo wa ulazima wa kuwaelimisha na kuwasisitiza wamiliki wa vyombo vya usafiri wakiwemo wenye mabasi yaendayo mikoani na daladala zinazotoa huduma ya usafiri katika majiji na miji, kusaidia utekelezaji wa agizo hilo la serikali.

Kama wamiliki wa mabasi ya abiria na vyombo vingine vya usafiri, watasimama kidete katika kuwasimamia madereva na makondakta wa mabasi yao, kutojaza abiria, kama ilivyoelekezwa na Waziri Mkuu, ni wazi kuwa hatua hiyo itarahisisha kampeni ya serikali ya kukabili kuenea kwa virusi vya corona.

Wamiliki wa vyombo vya usafiri, wasione kuwa kampeni hii ni ya vyombo vya dola pekee hususani askari wa usalama barabarani, bali ni ya kila Mtanzania, kwa kuhakikisha kuwa kila sehemu wanapokuwepo, inakuwa salama dhidi ya maambukizi ya corona.

Ni imani yetu pia kuwa kama kazi ya udhibiti wa msongamano wa abiria kwenye vyombo vya usafiri itakuwa ya wote, kwa maana ya abiria mwenyewe, madereva, makondakta, wamiliki na vyombo vya dola, kampeni hii itazaa matunda na vyombo vya usafiri vitakuwa si moja ya maeneo hatarishi, kama inavyohofiwa sasa.

Tunadhani pia ni wakati sasa wa wananchi, kuzingatia sana mabadiliko ya kitabia na kimtazamo kuliko kuhofia nguvu ya dola, kwani madhara ya corona yatawapata moja kwa moja wale ambao watashindwa kuchukua tahadhari dhidi ya maisha yao binafsi.

Tunatumaini kuwa endapo mafanikio yatakuwa katika mabadiliko ya kimtazamo na tabia kwa jamii nzima, suala la udhibiti wa virusi vya corona litapata wepesi mkubwa ; na ndani ya siku 30 zijazo, nchi itakuwa imepata picha kamili na mwelekeo wake kwa maisha ya Watanzania.

Hata hivyo, pale itakapobidi na katika dhana ya kuokoa maisha ya watu walio wengi, vyombo vya dola visisite kushughulika na wale wate watakaoshindwa kuzingatia maelekezo ya serikali katika kukabiliana na corona, kwani vitendo vyao vitageuka kuwa mauti kwa watu wengi.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi