loader
Picha

Maelekezo mapya kuzuia corona

TANZANIA leo inatimiza siku sita leo katika mapambano dhidi ya virusi vya corona vinavyosababisha homa ya mapafu, tangu ilipotangazwa kuingia nchini na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Machi 16 mwaka huu.

Katika siku hizo sita, Serikali imetoa maelekezo kadhaa ya kukabiliana nao ikithibitisha wagonjwa sita wameambukizwa virusi vya corona. Jana serikali ilitoa maagizo mapya kuhusu mapambano ya watanzania dhidi ya ugonjwa wa corona. Maagizo hayo yalitolewa baada ya mkutano kati ya wataalamu wa afya na Viongozi wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, uliojadili hali ya mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini.

Waziri Ummy Mwalimu katika taarifa ya wizara yake kwa vyombo vya habari baada ya mkutano huo alizitaka hospitali za Serikali na binafsi kuzingatia miongozo ya wizara kuhusu magonjwa ya mlipuko kabla ya kuwahamisha wagonjwa kwenye hospitali za rufaa za serikali.

Aidha maelekezo mengine aliyoyatoa jana ni wananchi kuendelea kupewa elimu na maelekezo sahihi kuhusu kujikinga na maambukizi; wananchi kujua kuwa siyo kila homa na mafua ni corona, kupuuzwa kwa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutumia wataalamu wa afya wizarani na taasisi zake na waganga wakuu wa mikoa na wilaya kupata taarifa sahihi za corona.

Kabla yake serikali ilitoa maagizo ya kuzuia misongamano kwenye mabasi na kufunga shule na vyuo vya juu visiwe chanzo cha madhara makubwa kwa wananchi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zimeendelea kuchukua hatua mbalimbali za dharura ambazo nyingi zimeungwa mkono na jamii na taasisi za kidini ikiwa kutoa utaratibu wa ibada na kufunga shule za kidini kuidhibiti.

SMZ jana ilitangaza kufuta safari za ndege zote zinazioleta watalii nchini na wageni kuwekewa siku 14 karantini wakifika nchini humo. Aidha katika mapitio yake ya hali halisi na wataalamu wa afya, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nayo jana iliendelea kusisitiza hatua za kujikinga ikiwa na kuagiza hospitali za serikali na binafsi kuacha kuhamisha wagonjwa kiholela.

Tangu homa ya Corona ilipuke mwishoni mwa mwaka jana Jiji la Wuhan katika Jimbo la Hubei, nchini China, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mpaka sasa homa hiyo imeshaenea katika nchi 169 duniani na kusababisha watu 209,839 kuugua na vifo 8,778. Hatua zilizochukuliwa Kutokana na mlipuko wa virusi hivyo, Serikali imechukua hatua kadhaa tangu mgonjwa wa kwanza aripotiwe Arusha mwanzoni wa wiki hii.

Akilihutubia taifa Machi 17 mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizitaja hatua ambazo serikali imezichukua kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo kuwa ni pamoja na kusitisha mbio za Mwenge wa Uhuru zilizopangwa kuanza Aprili 2, 2020 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili yake, shilingi bilioni moja kuelekezwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, wazee na Watoto kuikabili.

Pia serikali imezuia mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje, semina, warsha, makongamano, mikutano ya siasa na mahafali kwa siku 30. Pia imefunga shule zote za awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu, kusitisha michezo yote inayokusanya makundi makubwa ya watu ikiwemo Ligi Kuu Tanzania, Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili, Umitashumta, Umiseta na michezo mingine mbalimbali.

Majaliwa alisema Serikali inawataka Watanzania kusitisha safari zisizo za lazima kwenda nje ya nchi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu maeneo yote na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kwa wageni wanoonekana katika maeneo yao. Pia alisema, serikali imewataka wananchi wenye dalili za ugojwa huo kufikishwa kwenye vituo vya afya ili kupatiwa matibabu haraka.

Mambo muhimu Katika kuhakikisha maambukizi ya virusi vya corona yanadhibitiwa ipasavyo hapa nchini, Serikali kupitia Waziri Mkuu, Majaliwa pia imewataka watumishi wote wa taasisi mbalimbali zinazosimamia uingiaji wa wageni katika mipaka, viwanja vya ndege na bandarini, kusimamia kwa ukamilifu, kufanya uchunguzi wa kiafya na kuimarisha mipaka yote ili watu waingie nchini kupitia mipaka rasmi.

Jambo lingine muhimu ambalo serikali inataka lizingatiwe na wananchi ni kwa wenye dhamana ya kusimamia utoaji huduma zenye mikusanyiko kama vile ofisi za umma, mabenki, vituo vya mabasi na masoko kuweka vimiminika au vitakasa mikono vya kuua vijidudu. Sambamba na hilo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza taasisi kuhakikisha vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo vinapatikana muda wote na kwa bei ya kawaida na serikali itachukua hatua kwa watakaopandisha bei hovyo.

Idadi ya wagonjwa Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Serikali, mpaka sasa Tanzania ina wagonjwa sita walioambukizwa corona, Watanzania watatu waliowasili nchini kutoka nchi zilizokumbwa na maambukizi na wageni wawili, raia wa Ujerumani na wa Marekani na mwingine ambaye hajatajwa. Waliowekwa karantini Kwa kuwa baadhi ya wagonjwa hao walikutana na watu mbalimbali walipoingia nchini, serikali imewaweka karantini baadhi ya watu waliokutana nao.

Jijini Dar es Salaam, serikali ilisema imewaweka karantini watu 66 na Arusha watu 46 kuchukua sampuli kuwapima. Muda wa dalili kujitokeza Kwa mujibu wa Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza Kitengo cha Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Rogath Kishimba, muda wa kupata maambukizi hadi kuonesha dalili ni kuanzia siku mbili hadi 14.

Dk Kishimba alisema kutokana na muda huo wa kujitokeza dalili, ndiyo maana watu huwekwa karantini kwa siku 14 kwa kuwa ndani ya muda huo, kama washukiwa hawana dalili maana yake ni kwamba hawajaambukizwa. Hospitali zilizoandaliwa Waziri Mkuu, Majaliwa aliyataja maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu waliambukizwa na watakaoambukizwa virusi vya corona kuwa ni Hospitali ya Mloganzila iliyopo Dar es Salaam ambapo kumejengwa kambi maalum kwa ajili ya kazi hiyo.

Maeneo megine ni Kituo cha Afya Buswelu, Mwanza, Hospitali ya Mawenzi, Kilimanjaro, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar na Hospitali ya Chake Chake, Pemba. Hatua mpya Kwa jana taasisi mbalimbali na serikali zimechukua hatua mpya kudhibiti ugonjwa huo na kumetolewa ushauri mbalimbali kwa serikali. Ndege za utalii Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza kusitisha safari za ndege zote zinazoleta watalii nchini kama tahadhari ya kujikinga na corona.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari,Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo wakati akiwa Kidimni wilaya ya Kati Unguja, alipotembela kituo cha kupokea wagonjwa wa corona ambapo hadi sasa yupo mgonjwa mmoja.

“Tumechukua tahadhari ya kujilinda na ugonjwa wa corona. Kwa hivyo, Serikali imetangaza uamuzi wa kuzuia ndege zote zinazotoka nje kuingia nchini.......awali tulizuia ndege zilizokuwa zikileta watalii moja kwa moja kutoka Italia,’’alisema.

Kombo alisema kwa sasa wapo watalii kutoka Russia ambao wanatarajiwa kuondoka nchini huku wakisubiri ndege yao kuwachukua. Alifahamisha mgeni ambaye atakuwepo nchini atalazimika kukaa katika karantini kwa siku 14 ikiwa ni tahadhari baada ya kuchunguzwa afya yake kujua vipi kama yupo salama na ugonjwa huo. Wiki iliyopita zaidi ya watalii 1,800 walichukuliwa na ndege na kurudishwa nyumbani kupitia wakala wa makampuni yaliyowaleta hatua ambayo imezifanya jumla ya hoteli sita za ukanda wa Kiwengwa kufungwa.

Bei za vikinga corona Jana katika mahojiano na kituo cha Independent Television ( ITV), Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Lawrean Bwanakunu alisema si sahihi kwa wafanyabiashara kupandisha maradufu bei ya vikinga Corona na wakiendelea MSD itaingia mtaani kuwauzia wananchi moja kwa moja.

Alisema anashangazwa na dawa za kuoshea mikono (sanitizer) kuuzwa Sh 5,000 wakati bei halali ni Sh 2,500. Aidha alisema, bei halali ya dawa za kuoshea mikono ni shilingi 85,000 kwa lita tano na Sh 200,000. Pia vidonge vinavyotumika kuweka kwenye maji ya kunawa mikono bei halali kwa kidonge k MSD ni shilingi 360 na wafanyabiashara wanauza sh 5,000.

Aidha alisema anashangazwa kwa kopo lote lenye vidonge 100 kuuzwa sh 500,000 wakati bei halali ya MSD niSh. 36,000. Bwanakunu, alisisitiza MSD haifanyi kazi ya kuuza dawa za bidhaa zinazotumika kwenye afya lakini kama itabidi ifanye kazi hiyo ya kusambaza mitaani kuwadhibiti wafanyabiashara wanaotumia tishio la Corona kuumiza wananchi, itafanya hivyo.

Ibada Anglikana Katika kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na ugonjwa hatari wa corona, Kanisa la Anglikana nchini limetangaza kuongeza ibada zake katika makanisa yake yote ili kuondoa msongamano ambao ungesababisha maambukizi zaidi.

Akitoa tamko hilo jana Jijini Arusha, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Tanga, Askofu Dk Maimbo Mndolwa alisema wamejipanga kuendelea kuunga mkono jitihada zote za serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo kwa kushirikiana na wananchi na waumini wa kanisa hilo.

Askofu Mndolwa alisema wamejipanga kufanya ibada maalumu za mara kwa mara katika dayosisi zote 28 bara na visiwani ,jumuiya na familia kwa ajili ya kumwomba Mungu kuliepusha taifa na ugonjwa huo usiendelee kusambaa zaidi hapa nchini. Alisema wao kanisa wana imani kubwa hakuna lisilowezekana kwa Mungu ,hivyo wanaendelea kupiga goti kutafuta uso wa Mungu katika kipindi hiki Cha kwaresma ili asikie sala zetu na kuturehemu ili kutuepusha na gonjwa hilo linalotikisa dunia.

Alisema kanisa linaelekeza kila dayosisi itenge siku maalumu ya maombi kuanzia machi 19 kuomba Mungu atuepushe na Corona. Chadema washauri Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kudhibiti kusambaa kwa Corona, Chadema kimeishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kufunga mipaka ya nch ili kudhibiti wageni wanaoingia nchini.

Akizungumza jijini Dodoma jana, Waziri Kivuli wa Afya wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Secilia Pareso alisema kambi hiyo inashauri Serikali kufunga mipaka kutokana na wagonjwa wengi wanaojulikana wamepata maambukizi ya virusi kubainika kuwa wanatoka nje ya nchi wala si waliopo hapa nchini.

Pareso alisema kambi hiyo inajua kufunga mipaka italeta athari katika uchumi, biashara na utalii na maeneo mengine, lakini kutapunguza kasi ya kuingia virusi nchini ambavyo kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakikutwa navyo wageni wanaokuja nchini.

Pia waliishauri serikali kuweka bei elekezi kwa vifaa vya kujikinga na maambukizi zikiwemo vitakasa mikono, mipira ya kuvaa mikononi na dawa ili kusaidia wananchi kuzipata kwa bei nafuu badala ya sasa ambapo vimepanda bei zaidi ya mara tatu. Zimechangiwa na Khatib Suleiman,Zanzibar; John Mhala,Arusha;Magnus Mahenge, Dodoma.

WATU 11 wamekamatwa katika mpaka wa Horohoro uliopo kati ya ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi