loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Pamoja na maombi usipuuze maelekezo kujikinga na corona

NASHUHUDIA mama mmoja akisalimiana na mwenzake kwa kupeana mikono. Kisha anataka kunipa mkono lakini nikamwambia tumeshauriwa kutosalimiana kwa mikono ikiwa ni hadhari ya ugonjwa wa corona unaosababishwa na virusi ya COVID 19.

Mama huyo akanijibu, “sema kwa jina la Yesu corona haitakupata. Ukiwa na Mungu hakuna haja ya kuogopa kupeana mikono”. Bado natafakari msimamo wa huyu mama kwa ugonjwa huu ambao ni janga kwa dunia! Nikiendelea na tafakuri, nafika katika kituo cha daladala cha Mbezi Luis jijini Dar es Salaam. Inafurahisha kuona mamlaka zimechukua hatua ya kugawa kimiminika cha kutakasa mikono (sanitizer) kwa abiria wote wanaoingia kwenye mabasi hayo.

Wakati wafanyakazi wa mabasi hayo wakiendelea kugawa kimiminika kwa kila abiria anayeingia, mzee mmoja anagoma kupokea. Anasema anamuamini ‘Allah’ tu na si hizo dawa zinazotolewa na wanadamu. Hata hivyo nilifurahishwa na Mchungaji Daudi Mashimo ambaye mara nyingi huhubiri kituoni hapo. Akihimiza abiria wote kuhakikisha wanapokea kimiminika, alitaka wafanyakazi wasimruhusu mzee huyo kuingia ndani ya basi.

“ Serikali imetuelekeza, neno la Mungu linatuambia tutii mamlaka…Tusifanye mchezo na corona,” alisikika mchungaji huyo akihubiri kituoni hapo akikemea watu wanaopinga maelekezo haya yenye nia njema ya kunusuru jamii dhidi ya ugonjwa huo.

Ni wazi watu wa namna hii hawawezi kukosekana katika jamii huku baadhi yao wakifanya hivyo kutokana na ujinga wa maandiko ya Mungu. Upo umuhimu mkubwa wa viongozi wa kiroho na watu wanaojua maandiko kutoa elimu sahihi itakayowakomboa ‘wapinzani’ kimwili na kiroho.

Naamini kila dini ina maandiko na mifano ya kiimani inayoweza kusaidia kuondoa imani ambazo binafsi naona ni za kumjaribu Mungu. Itakumbukwa, yapo madhehebu yaliripotiwa kukataza watu kwenda hospitali wakiamini maombi pekee ndiyo tiba. Ina maana watu wenye imani za namna hii wanataka kuaminisha jamii kwamba nchi zote na watu wote waliokumbwa na maambukizi ya corona hawamjui Mungu au hawajui kuomba? Mchungaji Eliona Kimaro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama, Dayosisi ya Mashariki na Pwani ana neno juu ya watu wote wanaofanyia mzaha maelekezo ya kitaalamu juu ya namna ya kujikinga na corona.

Akihubiri katika ibada ya asubuhi (Morning Glory) hivi karibuni kanisani hapo Dar es Salaam, Mchungaji Kimaro alisisitizia waumini akisema, pamoja na maombi, wazingatie pia yanayoelekezwa na wataalamu juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya corona.

Alisema, “msifanye mzaha. Kwanza, nasema ni maombi lakini pia zingatia yale yaliyoelekezwa kwa mujibu wa afya pamoja na imani yako ya kilokole. Hiyo imani yako ya kilokole, ya Kikristo, ya Kiislamu, ya Kihindi, ya Kibudha ninaiheshimu na mimi nina imani lakini zile tahadhari lazima uzichukue. Wapo wanaosema tulishaomba damu ya Yesu…Damu ya Yesu inatufunika na ndiyo maana hata nyumbani kwako unafunga mlango na kuna hata geti…”

Washukuriwe viongozi wa dini na watu wengine wanaojua maandiko kwa kuendelea kuelimisha juu ya nafasi ya maombi sambamba na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu. Saphira Jagaji ni Mwinjilisti katika kanisa mojawapo la African Inland (AIC) mjini Geita anayeelimisha akisema: “kuna msemo wa Kisukuma unasema ‘kulomba na kusabula’.

“Maana yake ni kwamba unapokuwa kwenye mtumbwi unaovuja, lazima uombe huku ukitoa maji vinginevyo utazama. Ndugu yangu Yesu yupo na anafanya kazi ila tuchukua tahadhari.” Muumini wa KKKT, Novert Wilson alisema, “hata wana Israel wakiwa safarini, ulitokea mlipuko wa ugonjwa.

Ikawa kwamba kila aliyetazama sanamu mfano wa nyoka alipona. Je, waliogoma ilikuwaje?” Mchangiaji mwingine anaomba viongozi wa dini wasisitize waumini wao wawe na maarifa ya kutosha kuhusu maandiko.

“Tumeona viongozi wa dini zote wametoa matamko ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuzuia maambukizi. Hawa wanaopinga naona wamekosa maarifa,” anasema mchangiaji mwingine.

Ananukuu Biblia kupitia kitabu cha Hosea 4: 6 akisema inaweka bayana kwamba “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…” Nionavyo, nyumba za ibada ziendelee kuwa eneo muhimu la kukemea wazushi, wanaobeza, wanaopinga na kukwamisha mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu kwa sababu mbalimbali. Karipio lilenge pia watu wenye nia ya kugeuza ugonjwa huu kuwa fursa ya kibiashara na umaarufu.

Huenda tukaanza kushuhudia ‘mitume’, ‘manabii’ na waganga wa kienyeji wakitamba kuombea na kutibu watu wenye corona! Waumini waelezwe ukweli kuhusu corona kwamba haubagui dini, rangi, taifa, jinsi, tajiri au masikini. Wasisitizwe waepuke kusalimiana kwa mikono, waepuke safari zisizo za lazima, msongamano na wanawe mikono mara kwa mara.

Waambiwe kwamba masharti haya yote ni kwa nia njema ya kunusuru watu. Jamii haina budi kukubaliana nayo hata kama yanaweza kuleta usumbufu kwa namna moja au nyingine. Waelezwe virusi vinaweza kusambaa kupitia maji maji kutoka kwenye pua au mdomo wa aliyeathirika. Kugusa mafua, mate na makohozi ya mwenye virusi na kisha kujigusa mdomo, macho na pua kunaweza kusababisha kupata virusi vya corona. Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa kali, uchovu na kikohozi kikavu.

KATIKA jumla ya klabu 20 za Ligi Kuu England (EPL) ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi