loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera Polisi wanawake kusaidia waathirika Rufiji

MTANDAO wa Polisi Wanawake (TPFN) umeitaka jamii kuguswa na kuwasaidia wakazi wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani waliopata maafa ya mafuriko kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni katika wilaya hiyo na kupelekea baadhi yao kukosa makazi na chakula baada ya nyumba kuzingirwa na maji.

Mwenyekiti wa TPFN, Naibu Kamishna wa Polisi, Mary Nzuki alisema hayo wakati wa kukabidhi misaada mbalimbali kwa wakazi hao juzi ambapo walitoa msaada wa unga kilo 1000, maharage kilo 500, mafuta ya kula lita 120, sukari kilo 100 na sabuni boksi 18 kwa ajili ya wahanga waliopata mafuriko.

Alisema mafuriko yamesababisha hasara kubwa kwa makazi na uzalishaji mali kwa jamii kusimama. Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo ameushukuru mtandao huo kwa msaada huo utakaosaidia sana kwani hekta 4,000 za mazao zimesombwa na maji hivyo kuongeza mahitaji ya chakula kwa wakazi hao.

Tumeguswa sana na moyo huu wa kizalendo wa askari polisi wanawake nchini na tunaungana na DC wa Rufiji, Juma Njwayo kuwapongeza na kuomba makundi mengine yaige mfano wao wa kujitoa kwa jamii.

Tumefurahishwa zaidi na kujitoa kwao kwani hatua hiyo imethibitisha ile dhana potofu iliyojengeka katika vichwa vya baadhi ya watu kuwa, Jeshi la Polisi ni la kukamata wahalifu tu wakati kumbe siyo.

Kwa kutoa misaada hiyo, Polisi hawa wanawake wamethibitisha kwa niaba ya Polisi wanawake wote nchini na hata Polisi wanaume kuwa, Jeshi la Polisi kama yalivyo majeshi mengine, ni ya wananchi wote.

Wamethibitisha kuwa, pamoja na kazi yao kujielekeza zaidi katika kuzuia uhalifu na kulinda mali za raia, wako mstari wa mbele pia kujumuika na jamii wanayoisimamia nchini, katika shida na raha wanazoziishi.

Ni kutokana na ukweli huo, tunampongeza Mwenyekiti wa mtandao huo, DCP Nzuki kwa kuwa mbunifu na mwenye maono makubwa kuhamasisha askari Polisi wanawake kujitoa kwa ajili ya jamii yenye shida.

Ni wazi ili kupata vifaa mbalimbali walivyovitoa kwa waathirika hao wa mafuriko, askari hao na wenza wao watakuwa wamejitolea kiasi cha fedha kwenye mishahara yao na hivyo kujinyima kwa ajili ya jamii.

Ni moyo mkubwa wa kizalendo ambao unapaswa kuigwa na askari wa majeshi mengine na wafanyakazi wa taasisi nyingine za umma na binafsi kwani waliopatwa mafuriko ni ndugu zao, Watanzania wenzao.

Ni matarajio yetu kuwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro ataungana nasi kuwapongeza tena askari hawa wa kike walioonesha mfano mzuri wa kazi za askari kuwa si kukamata wahalifu tu. Kwa wana Rufiji, tunaomba misaada iliyotolewa kwao itumiwe vyema, iwasaidie kupanga maisha upya.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi