loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera TMA ufanisi utabiri hali ya hewa

TANZANIA jana iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

Katika salamu zake kwa siku hiyo muhimu, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema Tanzania kama ilivyo kwa wanachama wa wengine wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ina jukumu la kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri wa hali ya hewa, ambao huchangia kulinda vyanzo vya maji na hivyo kuboresha upatikanaji wa rasimali maji.

Waziri alisema upatikanaji wa rasilimali maji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya taifa na malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.

Alisema huduma za hali ya hewa ni muhimu katika malengo hayo, hususani lengo namba saba ambalo linahusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.

Kwa dhati kabisa tunaungana na Waziri Kamwelwe kuipongeza TMA kwa kazi kubwa na nzuri, inayofanya katika kufuatilia na kuhabarisha umma juu ya mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri, ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi na wananchi.

Pamoja na kuwa Waziri ametaja tu baadhi ya manufaa ya taarifa za TMA, lakini kwa ujumla wake utabiri wa TMA umekuwa chanzo kikubwa cha taarifa kwa wananchi katika kupanga mipango yao ya maisha iwe ni katika biashara, kilimo, maeneo muafaka ya kujenga na mengineyo.

Tunafahamu kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa, kwa kuhakikisha TMA inatoa huduma za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa.

Hii ni pamoja na kuijengea uwezo TMA kwa upande wa vifaa na wataalamu ili kuhakikisha wanafuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote.

Katika kipindi cha miaka michache iliyopita tumeshushudia TMA ikitoa taarifa ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya watu na mali zao, kwa kutabiri uwepo wa mvua kubwa zenye kuambatana na upepo mkali na matokeo ya utabiri kuwa sahihi kwa zaidi ya asilimia 90 na kile kilichotabiriwa.

Ni imani yetu kuwa mafanikio haya ya TMA katika kutabiri matukio ya hali ya hewa kwa uhakika mkubwa, yametokana na namna serikali inavyoendelea kuijengea uwezo wa wataalamu na vifaa mamlaka hiyo na kuifanya kuwa moja ya taasisi, inayoaminika nchini tofauti na miaka iliyopita.

Kwa kuzingatia pongezi hizi, tunatoa rai kwa watendaji na wafanyakazi wa TMA kuendelea kuongeza juhudi na maarifa katika utendaji wao wa kazi ili kuwafanya wananchi waendelee kujivunia, uwepo wa mamlaka hiyo muhimu katika ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi