loader
Picha

Walanguzi wanawaibia wakulima wa choroko

VIONGOZI wa vyama vya ushirika na mazao mkoani Shinyanga wanasema bado wakulima wa choroko hawana uelewa kuhusu ununuaji kwa mfumo wa kuangalia bei kwa njia ya mtandao na kufanya ununuzi kwa mnada.

Kimsingi kwa sasa changamoto kubwa kwa sasa ipo kwa wakulima wenye madai katika zao la pamba, hali inayowafanya wengine kupata kigugumizi kupeleka tena mazao yao katika vyama hivyo hususan zao la choroko.

Hii inatokana na madai waliyo nayo hali inayowafanya wengine waamue kuwatumia wafanyabiashara wanaolangua na mazao yao kwa kuwapunja wakulima hao.

Katika Mkutano Mkuu wa 25 wa Chama Kikuu cha Ushirika (Shirecu), viongozi wa vyama hivyo (Amcos) kutoka maeneo mbalimbali mkoani hapa wanahoji sababu za ushuru kutokuletwa huku zao la choroko likisisitizwa liuzwe katika soko la mnada, jambo walilodai ushuru ulipwe kwanza.

Domick Lema kutoka Amcos ya Mhunze anasema bado hata wao viongozi hawajauelewa mfumo huu na siyo kwamba wanapingana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Anasema hii ni kwa sababu wakulima wenye shida ya fedha wanapopata matatizo, huwa hawezi kusubiri mnada, hivyo ni vyema walanguzi nao wapigwe marufuku.

Ndaturu Sangwe kutoka Amcos ya Sayu anasema wamekuwa wakipambana na wafanyabiashara wa zao la choroko kwani hawapendi mfumo huu. Wanaomba kupata barua za zuio ili watakapo ingia kwa wakulima ili waoneshwe badala ya kusikia kwa maneno tu.

Mwenyekiti wa Ikumbo Amcos, Paul Gwachele anasema wakulima wamelima zao la choroko kwa wingi, lakini walanguzi wameingia na kununua kwa bei ya Sh 800 kwa kilo na vipimo visivyo vya uhakika.

Aliishukuru serikali kuwaletea mfumo huo ili kuondokana na walanguzi. Habibu Twaha kutoka Amcos ya Mwenge anasema kwa mfumo huu wa mazao, hata mkulima mdogo anaweza kuuza kwenye soko la kimataifa kwa kuwa unakwenda kuoneshwa bei ya ushindani moja kwa moja kama ilivyo sasa kwenye dhahabu.

Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika (Shirecu), Ramadhani Kato, anasema kuna Amcos 129, lakini Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika, Hussein Bashe amekwishasaini ununuaji wa mazao kwa skabadhi ghalani kwa zao la choroko na dengu hivyo wakulima watumie Amcos zilizopo kwenye maeneo yao.

“Tumekwishazunguka na wataalamu tukagundua wakulima wanaibiwa kwani vipimo vinavyotumika kupima choroko ni ndoo ambazo zimechakachuliwa, lakini tumewapatia elimu ili watumie Amcos ili wasipunjwe; huko watachukua bei wanayoitaka wao kupitia mnada ikiwa mizani zipo sahihi,” anasema Kato.

Kato anasema mfumo huu utaendelea hata katika mazao mengine, kama mpunga ambao umekuwa ukilimwa kwa wingi katika baadhi ya maeneo mkoani Shinyanga.

“Mkulima anachotakiwa kufanya ni kukusanya mazao yake na kuyapeleka kwenye Amcos kusubiri mnada ambao haukai na fedha zake kwa muda mrefu na anazipatana kupitia benki,” anasema.

Mrajisi kutoka mkoani Shinyanga, Winston Msemwa, anasema mfumo ulioanzishwa na serikali hautamuumiza mkulima kwa kuwa upo wazi na makini.

Anasema baadhi ya watu wamekuwa wakiupinga kwa kuonesha na kulinda maslahi yao binafsi na kwamba, hata mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri pia, hivyo wakulima wautumie.

Kwa mujibu wa Msemwa, halmashauri zitapewa maelekezo kupitia kwa watendaji wa kata na vijiji ili kuzuia walanguzi kwani kwa kufanya hivyo, wakulima hawatarubuniwa na wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakitoa lugha za uongo ili wapate wao soko.

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dk Titus Kaman anasema ushuru wa vyama vya msingi unalipwa kwa kipindi kifupi kwani maamuzi yamekwishatolewa na serikali hivyo, wawe na subira.

Anasema mfumo wa kununua choroko kwa njia ya mnada ni mzuri kwani mapato ya serikali hayapotei hovyo na mkulima hapunjiki.

Dk Kamani anawataka wakulima wa zao la choroko mkoani Shinyanga kuepuka kulanguliwa hali inayowafanya wapunjike na badala yake, anawataka watumie vyama vya ushirika Amcos vinavyoonesha ushindani wa bei.

“Kipimo wanachotumia walanguzi kwenye mazao kinaitwa kitini, ambacho kinawapunja nyie na wamekuwa wakitumia wakikitanua kwa mafuta na kukiweka juani au kukiweka kwenye mchanga wa moto ili kuongeza ujazo kwa karibu kilo tano kwa kitini; hapo mkulima unapunjika,” anasema Dk Kamani.

Kamani anasema mfumo wa bei ya ushindani katika mnada wa soko la choroko mkoani Shinyanga ambao wakulima walioneshwa bei ya wanunuzi wawili walioingia kwenye ushindani.

Mnunuzi mmoja alitoa bei ya Sh 1,248 huku mwingine akitoa bei ya shilingi 1,340 kwa kilo moja.

Anasema zao la choroko linatumika duniani kote na hapa nchini wakulima wanadanganywa na wajanja wachache wanaowanyonya ndio maana serikali imeamua kulianzishia zao hilo mfumo wa ununuaji kwa njia ya ushindani wa bei na minada itakayokuwa ikifanyika kupitia Amcos.

Anasema ni vyema wazitumie ili kuwapa soko la uhakika na kujichagulia bei waitakayo kupitia mfumo huo. Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Charles Malunde anasema wakulima wamekuwa wakiuza choroko kwa walanguzi kwa Sh 800 hadi 1000 kwa kilo moja tena wakitumia vipimo vya kitini na kupotoshwa kuwa kwenye vyama vya ushirika wanakopwa.

Aliwataka watumie Amcos inayoonesha ushindani wa bei kupitia mtandao na stakabadhi ghalani.

“Nawaomba wakulima wafungue akaunti za benki ili fedha wanazouza mazao yao zipitie benki kwani zitakuwa salama pia mfumo ulioletwa na serikali ni rahisi hata wakala atakayetumiwa kukusanya mazao atayapata kwa haraka, bei nzuri yenye uwazi, vipimo vya uhakika na halmashauri itapata ushuru wa uhakika bila kuweka vizuizi vya mazao barabarani,”anasema Malunde.

Ofisa kutoka Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Augostino Mbulumi anasema serikali imeanzisha mfumo huo kabambe ili wakulima wanufaike kwa kuwashirikisha wanunuzi na wakulima.

Anasema kazi ya serikali ni kutangaza bei ili atakaye kuwa na bei ya juu, awe ndiye mshindi hivyo, haihitaji wakulima kusafirisha mazao yao kwani sokoni litawakuta kupitia vyama vya ushirika.

Aidha, serikali imetangaza mazao matano ambayo ni dengu, ufuta, soya, mbaazi na choroko yatakayopitia katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye vyama vya ushirika pia Mkoa wa Shinyanga kwani mwaka 2017/18 ulikuwa na tani 17642 za choroko na mwaka 2018/19 ni tani 15,143.

TANZANIA inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Sita katika Mfumo wa ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi