loader
Picha

Umeme REA ulivyoinua maisha ya vijana, wanawake

“AWALI nilikuwa mama wa nyumbani kwa kuwa sikuwa na eneo la kufanyia biashara. Baada ya umeme kufi kishwa kwenye eneo hili na wenye mitaji yao kufunga mashine za kukoboa mpunga nikachangamkia fursa ya kuja kuuza chakula. Mwanzoni nilianza kwa kupikia nyumbani na kuja kuuza baadaye nikaamua kujenga kibanda hapa hapa ili iwe rahisi kupika.”

Anasema mmoja wa mama lishe niliyemkuta kwenye eneo la viwanda vya kukoboa mpunga katika eneo la Relini, kata ya Rujewa wilayani Mbarali.

Hili moja kati ya maeneo nchini yaliyonufaika na mradi wa kusambaza umeme vijijini (Rea).

Mama huyu anayependa ajulikane kwa jina la Mama Jasmin anasema eneo wanalofanyia biashara awali lilikuwa msitu uliojaa vichaka na miti ya asili, lakini sasa lina mwonekano wa tofauti kwa kuwa limeanza kuwa mji.

Anasema sasa havijengwi viwanda pekee, kwani kutokana na fursa zilizopo watu wameanza kujenga makazi, maduka, vibanda vya simu, kunyoa na hivyo kuzidi kupanua wigo wa shughuli za kibiashara.

“Unaona upande ule wa pili wa barabara kulivyo… Ndivyo na huku kulikuwa kabla ya kujengwa viwanda. Ilikuwa ni vichaka na hapa hakukuwa na shughuli yoyote iliyokuwa ikiendelea. Hapa nilianza biashara ya kupika mwaka juzi mwezi wa sita,” anasema mama Jasmin.

Mama lishe wengine watatu walioungana na kufanya biashara pamoja wakiongozwa na aliyejitambulisha kwa jina la Jasmini Michael, wanasema kipindi cha mavuno ya mpunga yaani kuanzia mwezi wa nne wanapata wateja wengi zaidi kwenye kibanda chao.

Hiyo wanasema inatokana na uwepo wa watu wengi wanaokwenda hapo kwa ajili ya shughuli mbalimbali wakiwemo vibarua wa kushusha na kupakia mizigo kwenye malori.

Wanasema awali walikuwa wakifanyia biashara kwenye mashine za mpunga zilizokuwa mjini Rujewa eneo wanalosema halikuwa rafiki kwa kuwa viwanda hivyo havikuwekwa pamoja hivyo walikuwa mbalimbali.

Musa Ndelwa ni miongoni mwa wafanyabiashara wanaoendelea pia kunufaika na kufika kwa umeme kwenye eneo hili kutokana na uwepo wa shughuli za kibiashara zinazokusanya watu wengi sambamba na uwepo wa hali ya hewa ya joto katika wilaya ya Mbarali.

Yeye anasema aliona fursa ya kuuza vinywaji baridi kuwa yenye manufaa zaidi kwake na kwamba anajipatia kipato kutokana na kuuza soda, juisi na maji baridi.

Anasema bila umeme asingeweza kufanya biashara hii ambayo licha ya kumpa faida lakini pia inawasaidia watu wanaofanya shughuli kwenye eneo hilo kukata kiu wakiwa kazini. Fadhili Kilongo ni mmoja kati ya wafanyakazi watano walioajiriwa katika kampuni ya Baraka Rice Mill yenye viwanda viwili kwenye eneo hili. Yeye anasema katika eneo lote la Relini kuna viwanda nane vya kukoboa mpunga.

Hii imetoa fursa nyingi za ajira kwa vijana na akina mama wenye kupenda kujishughulisha. “Kwenye kampuni yetu pekee tumeajiriwa watu watano.

Hii ni kuanzia meneja na sisi tunaoendesha mitambo. Unaweza kuona kwenye eneo hili mashine zilizo- fungwa ni za kisasa na zina uwezo mkubwa tofauti na zile za kizamani zilizokuwepo kule Rujewa mjini.

Hapa kwa mashine moja tuna uwezo wa kukoboa gunia 300 za mpunga wakati zile hukoboa gunia zisizozidi 200,” alisema kijana Fadhili.

“Hapa kuanzia mwezi wa nne panachanganya sana.. Watu wanakuwa wengi kwa kuwa kazi nazo zinakuwa nyingi. Vijana kutoka maeneo mbalimbali huja kwa ajili ya kufanya vibarua. Na ongezeko la watu wengi ndilo lililosababisha hata mama lishe waje kufungua migahawa hapa. Imefika mahali sasa umekuwa mji kama unavyoona watu wamejenga makazi,” anasema.

Anaongeza: “Tunachoomba serikali ni kuwepo kwa umeme wa uhakika usiokatika katika maana ndiyo tegemeo letu na naweza kusema ndiyo maisha yetu. Yaani bila umeme uwepo wetu hapa hauna maana kabisa.”

Kwa upande wake, kijana Elihudi Lupenza anasema yeye kwenye eneo hilo ananufaika na ajira za aina mbili kutokana na vipaji alivyojaaliwa.

Ya kwanza ni kuendesha mitambo kwenye mashine za kukoboa mpunga na pili ni fundi ujenzi. Hivyo anasema shughuli za ujenzi zinapotokea hufanya kama nilivyomshuhudia akipiga sakafu kwenye moja ya jengo linalojengwa kwa ajili ya maduka.

“Majengo mengi hapa nimeshiriki kwenye ujenzi wake. Lakini nje ya kazi za ujenzi mie pia naendesha mitambo ya kukoboa mpunga. Na kuendesha mashine nimejifunzia hapahapa si unajua tena tunajiongeza. Ikipatikana kazi ya kusambaza mpunga unaoanikwa tunafanya. Hapa ni kazi tu,” anasema.

Uwepo wa viwanda na umeme umetoa pia fursa ya uchongaji vipuri na uchomeleaji. Emanuel Mwingila ni mmoja wa vijana waliojipatia ajira ya kuchonga vipuri kwa ajili ya mashine zilizopo kwenye eneo hili.

Anasema yeye aliona autumie ujuzi wake kwa kufanya kazi ya kuchonga vipuri kwa kuwa alikuwa amekwisha somea ujuzi huo Veta.

Baadhi ya vijana katika mji wa Rujewa wanasema kutokana na uzalishaji mkubwa wa zao la mpunga wilayani hapa bado vinahitajika viwanda zaidi vya kukoboa mpunga.

Hii wanasema inatokana pia na wananchi kuelimika kwa kutambua umuhimu ya kuuongezea thamani mpunga na kuukoboa kabla ya kuuza. Wanawake wanaouza mchele nje ya viwanda vilivyopo wanasema eneo hilo ni rafiki kibiashara tofauti na walikokuwa wakiuzia awali mjini Rujewa

HAKUNA aliyefahamu jina lake wala asili yake. Hata yeye mwenyewe ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi