loader
Picha

Kituo cha urasimishaji kinavyoinufaisha Singida

“MIAKA ya 1975 ukumbi huu ndiyo ilikuwa sehemu yetu ya kufanya mazoezi kwa maana ya kucheza muziki, bendi zote za muziki unazozifahamu zilizokuwa zinawika enzi hizo zilikuwa zikija kupiga muziki hapa kwetu Singida, zinapigia ukumbi huu.”

Anasimulia Athumani Sima (80), kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyofika Mjini Singida kwa ziara ya siku mbili kukagua miradi mbalimbali iliyo chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Anasema anaishukuru Serikali ya Mkoa wa Singida kwa kugeuza jengo la ukumbi huo kuwa kituo cha kisasa cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara ili kuwajengea uwezo wafanyabiashara ili biashara zao ziwe rasmi na kuendesha kwenye mfumo unaotambulika kisheria.

Kituo hicho kilianzishwa kwa ushirikiano wa Manispaa ya Singida na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita).

Baada ya ukarabati kukamilika na kuanza kutumika Desemba 10, 2019 Ofisi ya Biashara ya Manispaa Singida ilihamia rasmi kwenye jengo hilo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bravo Lyapembile anasema manispaa iliona umuhimu wa kufanya mchakato wa urasimishaji wa biashara kuwa wa haraka, rahisi na wa gharama nafuu kwa mfanyabiashara.

Anasema: “Urasimishaji na uendelezaji biashara katika Manispaa ya Singida lazima ufanywe kwa pamoja na taasisi zote muhimu na ufanyike katika sehemu moja kwenye jengo hilo.”

Lyapembile anazitaja baadhi ya taasisi zilizopo kwenye jengo hilo ili kufanikisha urasimishaji biashara haraka kuwa ni pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki za NMB, CRDB na NMB.

Nyingine ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Akizungumza na wafanyabiashara na vikundi vya wajasiriamali mbalimbali wa Singida katika jengo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Huruma Mkuchika anazielekeza halmashauri za wilaya zote nchini kwa kushirikiana na Mkurabita kuanzisha vituo hivi (One Stop Center) katika maeneo yao ili kuwajengea uwezo wafanyabiashara.

Hii itawezesha biashara zao kuwa rasmi na kuziendesha katika mfumo unaotambulika kisheria baada ya kuona ufanisi mkubwa wa kituo hicho baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kukikagua kituo hicho.

Waziri Mkuchika anasema amefurahishwa na ubunifu uliofanywa na Manispaa ya Singida kwa kuanzisha kituo hicho ambacho ni msaada mkubwa kwa ajili ya kuwakwamua wafanyabiashara na kuzitaka Halmashauri nyingine kuja kujifunza namna ya kuanzisha vituo kama hicho kutoka Manispaa ya Singida kwa kuwa kimekuwa kikifanya kazi zake vizuri.

“Ubunifu mlioufanya kwa kuanzisha kituo hiki kwa kuwa ni jambo muhimu sana linalotakiwa kwa wakati tulionao kwa maendeleo ya taifa letu,” anasisitiza Mkuchika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Dk Jasson Rweikiza anasema Kamati yake imeridhishwa na kazi inayofanywa na Kituo hicho na kuwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo vizuri kupata mikopo katika taasisi za kifedha ili kuziendeleza biashara zao.

Mjumbe wa kamati hiyo, Venance Mwamoto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilolo kwenye Mkoa wa Iringa anasema, mkakati wa kutumia vituo vya urasimishaji na uendelezaji biashara unapaswa kutiliwa mkazo na serikali ili kuifikisha Tanzania uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Akitoa taarifa ya kituo hicho mbele ya Kamati, Ofisa Biashara wa Manispaa ya Singida, Erick Sinkwembe anasema mwaka 2018/2019 Manispaa ya Singida kwa kushirikiana na Mkurabita imefanya urasimishaji biashara kwa njia ya kujenga uwezo kwa wafanyabiashara 777.

Anasema ukarabati wa kituo hicho umegharimu Sh 17,349,960. Gharama za ukarabati zilitolewa na Mkurabita wakati manispaa imegharamia uwekaji wa mifumo ya ukusanyaji mapato yatokanayo na ada za leseni. Sinkwembe anasema Mkurabita pia ilitoa vitendea kazi kuwezesha urasimishaji kwenye kituo vikiweno kompyuta moja, UPS, skana na printa vilivyogharimu Sh 4,071,000.

Anasema kituo kimeendelea kutoa huduma mbalimbali za urasimishaji na uendelezaji biashara katika Manispaa ya Singida zinazotolewa na maofisa biashara, ofisa mipango miji, ofisa afya na mwanasheria.

Anazitaja huduma zitolewazo kituoni hapo kuwa ni pamoja usajili wa majina ya biashara kupitia mtandao wa BRELA, upatikanaji wa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), uhakiki wa hesabu na tathmini ya kodi, ujazaji na usainishaji wa fomu za maombi ya leseni za biashara.

Huduma nyingine ni upatikanaji wa leseni za biashara, mafunzo ya utunzaji kumbukumbu muhimu za biashara na kuwezesha biashara kuwa na uhusiano na benki ili kupata huduma mbalimbali za kibenki.

Kwa mujibu wa Sinkwembe, tangu kuanzishwa kwa Kituo Kimoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara Desemba 2019, kimeleta matokeo chanya kwa wafanyabiashara wa Singida na taifa kwa jumla.

Matokeo hayo ni pamoja na kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara kwani sasa wanapata huduma za urasimishaji na uendelezaji biashara katika sehemu moja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na ada za leseni.

Serikali imepata Sh 52,324,060 tangu kuanzishwa kwa Kituo hadi Machi 6, 2020 na halmashauri imetoa leseni za biashara zipatazo 325 tangu kuanzishwa kwa Kituo hadi kufikia Machi 6, 2020.

“Wafanyabiashara 101 wamefungua akaunti katika benki ya NMB,” anasema.

Mafanikio mengine ni wafanyabiashara 47 kunufaika na mikopo ya Sh 188,000,000 kutoka benki ya NMB.

Anasema: “Mikopo hiyo imeinua mitaji ya biashara zao, wafanyabiashara wapatao 22 wameunganishwa na SIDO na kupata mafunzo ya utengenezaji wa sabuni za maji na miche pamoja na mifuko ya karatasi.”

Aidha, wafanyabiashara wengine 150 wanatarajiwa kupata mafunzo ya usindikaji wa vyakula yatakayotolewa na SIDO kuanzia mwezi Aprili 2020.

MKURABITA imeingia makubaliano na Benki ya NMB ambapo Wafanyabiashara 50 wataungwa katika Klabu ya NMB (NMB Business Clubs) ambako watakuwa wakipata mafunzo mbalimbali pamoja na kupata mitaji na kuunganishwa masoko na fursa nyingine zilizoko katika soko.

Mjasiriamali kutoka Iramba, Musa Mkumbo, aliieleza kamati kuwa pamoja na mafanikio hayo, kumekuwapo changamoto ya kukosekana kwa baadhi ya wataalamu kutoka katika taasisi zinazotoa huduma kituoni kwa muda wote kutokana na kuwa na idadi ndogo ya watendaji katika taasisi zao.

Anaiomba serikali kuwapunguzia kodi kwenye biashara zao akidai kumekuwapo kodi nyingi katika biashara moja jambo linalowafanya washindwe kupata faida.

Mratibu wa Mkurabita, Dk Seraphia Mgembe ameitaka Ofisi ya Biashara ya Manispaa ya Singida kuwa kiungo kikuu baina ya wadau katika mnyororo wa urasimishaji na uendelezaji wa biashara katika manispaa hiyo.

Sinkwembe anasema baada ya kujengewa uwezo na Mkurabita Halmashauri imekuwa ikiendelea kuzisisitiza taasisi husika kuajiri wataalamu watakaoendelea kutoa huduma kituoni hapo kwa muda wote na kuangalia uwezekanao wa kupanga siku na muda ambao wataalamu wa eneo fulani watakuwepo katika kituo.

“Muda na siku inayokubalika inajulishwa kwa watumiaji wa kituo. Kwa Mfano, TRA wamepanga kuwepo kituoni siku za Jumatano na Ijumaa,” alifafanua Sinkwembe Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi anaishukuru Kamati kwa michango yao waliyotoa ili kuboresha kituo na miradi yote waliyoikagua katika ziara yao ya siku mbili.

Anasema mkoa umepokea na utafanyia kazi kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa ili kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi wa Mkoa wa Singida kama inavyosema kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu!

Anasema urasimishaji biashara kwa dhana ya Kituo Kimoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Aidha, ni sehemu ya utekelezaji wa uchumi wa viwanda kupitia upatikanaji wa mitaji.

“Hivyo basi, huduma za Urasimishaji biashara zinazotolewa katika kituo hiki, zitakuwa endelevu ili kurahisisha urasimishaji wa biashara katika Mkoa wa Singida na kuzisaidia biashara rasmi kuendelea kutoa huduma katika soko pana nchini Tanzania,” anasema Dk Nchimbi.

JUHUDI za serikali kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi