loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusidharau, tudhibiti corona kwa umoja, uaminifu

JOKA limeingia nyumbani. Halibagui baba, mama, wasomi, tajiri wala masikini. Joka limeingia ndani. Joka linatakiwa kuuawa na si kulijeruhi kisha kujifungia ndani, kwani litatufuata hadi huko vyumbani. Joka limevamia dunia, Bara la Afrika na kubwa zaidi limeanza kuitesa Afrika Mashariki.

Joka hili la ugonjwa wa corona au COVID-19, halina kinga wala tiba, lakini linaweza kudhibitiwa kwa umoja na uaminifu wa dhati.

Rais John Magufuli ametoa maagizo sita kukabili ugonjwa huo hapa nchini, wakati Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, nao wamechukua hatua mbalimbali na mikakati kabambe kudhibiti janga hili katika mataifa yao.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Tanzania na Uganda ni kuzuia watu wanaotoka nchi zilizoathirika na ugonjwa huo kuingia. Wale wanaothubutu kuingia, sasa wanatengwa kwa siku 14, ili kujiridhisha kuwa hawana maambukizi na hawataleta maambukizi mapya.

Nampongeza Rais Magufuli kwa kuchukua hatua mpya na muhimu zaidi, kupambana na ugonjwa huo, ikiwemo kuimarisha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na ugonjwa huo, inayoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisaidiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Kimsingi, serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa joka hilo, linapondwa kichwa na kuuawa na si kulijeruhi tu, ingawa wapo baadhi ya watu wanaojaribu kulitekenya joka hilo, wakijidanganya kuwa haling’ati.

Rais Magufuli anasisitiza akisema Watanzania tusitishane, lakini tusiuchezee ugonjwa huo, maana unaua. Miongoni mwa wanaolitekenya joka hili ni waendeshaji bodaboda maeneo ya mipakani kama Sirari (Tarime) na kwingineko, wanaoongozwa na tamaa ya pesa wanaodaiwa kuvusha watu kupitia vichochoroni kwa malipo ya zaidi ya Sh 10,000, badala ya Sh 1,000 ya kawaida.

Hao wanadhani hiyo ni fursa ya kibiashara, bila kujua kuwa wanahatarisha wengine na wanajihatarisha wenyewe na familia zao, kwa kuwa wanabeba watu wasiopimwa kwa uchu wa Sh 10,000.

Hivyo ni vyema wafanyiwe mtego, wanaswe na kuchukuliwa hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine.

Katika miji mingi ikiwemo Dar es Salaam, daladala nyingi zinaonekana kupuuza agizo la kuweka vitakasa mikono na zinaendelea kujaza abiria, kwa madai kuwa hiyo ni biashara. Jeshi la Polisi liagize watendaji wake, kusimamisha kila daladala na kukagua kama ina vitakasa mikono.

Daladala zinazojaza kupindukia zitiwe hatiani. Heri kinga kuliko kuponya. Tukumbuke kuwa tukilijeruhi joka hili na kujifungia vyumbani, litatuafuata huko huko. Tuliue.

Wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa za kujikinga, wachukuliwe kama wahujumu uchumi na wasaliti wa taifa. Wamulikwe.   Aidha, familia nazo ziache utani huko mitaani. Suala la kutembeleana bila sababu za msingi liachwe.

Tusipuuze kunawa mikono na kuchukua tahadhari. Kila mmoja awe mwalimu, mlinzi, mlezi na mshauri wa mwingine katika vita hii inayotuunganisha, maana madhara ya corona, hayana ubaguzi wa kitabaka, kidini, kikabila wala kisiasa.

ZLATKO Krmpotic hadi sasa hajamaliza hata mwezi, tangu amejiunga na ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi