loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwenyekiti wa zamani CCM wa wilaya kuburuzwa kortini

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma itampandisha kizimbani aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya Dodoma Mjini, Robert Mwinje (39) na mhudumu wa ofi si hiyo ya chama, Nyemo Malenda (20) kwa makosa ya kula njama, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema jana kuwa Mwinje na Malenda watapandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa tuhuma ya kutenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura Namba 16 iliyofanyiwa Marejeo mwaka 2018.

Alisema uchunguzi wa Takukuru, ulibaini kwamba kati ya Oktoba 18 na Oktoba 20 mwaka 2019, Mwinje ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya Dodoma na Malenda ambaye alikuwa mhudumu wa ofisi hiyo, walighushi barua ya uteuzi wa waomba uongozi ndani ya chama hicho.

Watuhumiwa hao wawili walighushi barua za uteuzi, wakijifanya kwamba imetolewa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma na wakaikabidhi kwa mwanachama mmoja kwa hatua nyingine zaidi, huku wakijua kwamba ni uongo.

Wakati huo huo, katika Mahakama ya Wilaya ya Bahi, Adam Richard (49) ambaye ni Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu Wilaya ya Bahi amefunguliwa mashtaka manne ya kuomba Sh milioni 1.05 na kupokea Sh 553,000 kutoka kwa walimu wanne, ili awasaidie katika mchakato wa kupandishwa madaraja au vyeo.

“Alifanya kosa hilo ikiwa ni kinyume na Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2018,” alisema.

Kibwengo alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa walimu, kwamba mtuhumiwa ana tabia ya kutumia rushwa kama kigezo cha kufanikisha waliotaka kupandishwa madaraja, walianzisha uchunguzi na wamepata ushahidi kwamba kati ya Aprili na Juni 2019 mtuhumiwa alitenda kosa hilo.

“Taarifa tulizopata dhidi yake ni nyingi, bado uchunguzi wa taarifa zilizosalia unaendelea na ukikamilika atafikishwa mahakamani,” alisema.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi