loader
Picha

Abiria washushwa kwenye mabasi kudhibiti corona

UDHIBITI wa ugonjwa wa corona umeshika kasi katika maeneo ya usafi ri jijini Dar es Salaam, baada ya magari ya abiria kulazimishwa kupakia kwa idadi ya viti.

Abiria walioonekana kuzidi, walishushwa na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).

Gazeti hili limeshuhudia hayo jana asubuhi katika vituo vya mabasi vya Mbezi Luis, Mawasiliano Simu 2000 na Ubungo, ambako abiria waliokuwa wamesimama kwenye daladala, walilazimishwa kushuka.

Zoezi hilo lilifanywa na maofisa wa Latra wakishirikiana na askari wa usalama barabarani. Katika kituo cha Mbezi Luis, maofisa wa Latra waliokuwa wamevaa vitambulisho kwa kushirikiana na Polisi, walikagua kila basi lililokuwa linaingia na kutoka kituoni hapo, yakiwamo mabasi ya mkoani na kushusha abiria waliosimama kwenye gari.

“Samahani, nawaomba abiria wote mliosimama kwenye gari mshuke. Hii ni amri, si hiari na ni kwa manufaa yenu. Mjifunze kusikiliza vyombo vya habari ndugu zangu, mnavyofanya ni kama hamjui kinachoendelea, shukeni wote mliosimama sasa hivi,” alisikika akisema Ofisa wa Latra, Benedict Mwapwele.

Hata hivyo, baadhi ya daladala pamoja na kuamriwa kuondoka na abiria waliokaa peke yake, walipakia abiria katika vituo vya katikati vyote hadi kujaza mabasi huku wakilalamika kuwa kama wataendelea kulazimishwa, watasimamisha huduma, kwa kuwa wanapata hasara au la nauli ipandishwe.

Katika Kituo cha mabasi Mawasiliano Simu 2000, daladala nyingi hasa za Mbagala na Gongo la Mboto, zinazokuwa na abiria wengi kwa kawaida, zilipakia kwa kuzingatia idadi ya viti. Lakini, zilipofika vituo vya katikati, zilijaza abiria hadi kusongamana bila tahadhari.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano alipoulizwa kuhusu daladala kujaza abiria kama kawaida katika vituo vya katikati, alisema watalifuatilia na kulidhibiti.

Kondakta wa daladala inayofanya safari kati ya Mbezi Luis -Temeke, Juma Suleiman alisema hali ya biashara kwa sasa ni mbaya na huenda nao wakaambiwa na mmiliki wasitishe huduma, kwa kuwa wanajua hatari ya ugonjwa lakini pia hawawezi kujiendesha kwa hasara.

Abiria waliozungumza na gazeti hili walidai kuwa tatizo hasa kwa kituo cha Mbezi Luis ni uchache wa daladala, hasa zinazofanya safari kati ya Mbezi na Temeke kupitia Ubungo, jambo linalosababisha msongamano mkubwa na watu kusubiri usafiri muda mrefu.

“Ukikaa hapa angalia basi la Temeke vurugu yake, sasa tutakaa hapa mpaka saa ngapi ili upate usafiri wa kukaa? Tunaomba serikali itoe tamko mtu asifukuzwe kazi kipindi hiki kwa sababu ya kuchelewa kazini, hasa maeneo yenye changamoto ya usafiri kama Morogoro Road,” alisema Dora Michael, abiria aliyekuwa Kituo cha Mbezi Luis na mkazi wa Kibamba wilayani Ubungo.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi wa Latra, Gilliad Ngewe, aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari wenyewe, kwa kuzingatia miongozo ya kujikinga na kuacha kupanda daladala zilizojaa ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona

JAJI Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk Eliezer Feleshi amewataka ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi