loader
Picha

Historia na ugunduzi wa karibuni virusi vya corona

UWEZO wa virusi vya corona kumshambulia mwanadamu katika mfumo wake wa hewa na upumuaji, ulianza kuonekana kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1960 na hasa wakati huo watoto ndio walishambuliwa zaidi kulinganisha na watu wazima.

Tangu mwaka 2003, takribani aina tano ya virusi vya corona vyenye uwezo wa kumshambulia binadamu zimetambuliwa kwani pia vipo aina vya virusi hivyo kwa wanyama ambavyo havina uwezo kumshambulia mwanadamu. NL63, inayowakilisha kundi jipya la virusi vya corona ni pamoja na NL na virusi vingine vya kundi la New Haven ambavyo vimeonekana ulimwenguni kote.

Virusi hivi huleta ugonjwa katika sehemu ya juu ya njia ya hewa na upumuaji na sehemu ya chini ya mfumo huo wa upumuaji. Katika siku za karibuni virusi hivi vimeendelea kujitokeza na kumshambulia mwanadamu. Uhatari wa virusi vya corona ulionekana wakati ugonjwa uliopewa jina la SARS (severe acute respiratory syndrome) ulipoibuka.

Historia ya virusi vya corona kwa binadamu ilianza mnamo 1965 wakati Tyrrell na Bynoe walipogundua uwepo wa virusi hivyo walivyoviita B814. Iligundulika kwamba virusi hivyo vilikuwa vinashambulia njia ya hewa kupitia koo na kusababisha mafua, kikohozi na homa.

Ugunduzi huo wa Tyrrell na Bynoe ulizidi kuendelezwa na wataalamu wengine kama Hamre, Procknow na wengineo hadi kuwa rahisi kugundua SARS ilipoibuka.

Corona iliyosababisha SARS

Kwa kuzingatia uwepo wa aina ya virusi vya corona vinavyoshambulia wanyama, haikushangaza sana wakati ugonjwa mpya katika mfumo wa hewa na kupumua uliopewa jina la SARS ulipoibuka mwaka 2002- 2003 kama ilivyo sasa kwa corona iliyoanzia China Kusini na sasa inaendelea kuenea ulimwenguni kote kwa kasi kubwa. Virusi vya SARS vilisumbua sana kulinganisha na aina nyingine ya virusi vinavyoshambulia wanadamu.

Uchunguzi wa virusi vya corona vilivyokuwa vinasababishwa na SARS havikuelekea kwa asilimia 100 kwamba vinatokana na mwanadamu au wanyama hasa walioko katika milima ya Himalaya ulikoanzia ugonjwa.

Wakati wa kuibuka kwa SARS mwaka 2002–2003 mataifa ambayo watu wake walishambuliwa na virusi hivyo yalikuwa 29 katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Ulaya na Asia.

Takribani watu 8,098 waliugua ugonjwa huo huku vifo vikiwa 774 na kama virusi hivyo vilitoka kwa wanyama bado haieleweki vizuri namna vilivyofanikiwa kumwingia mwanadamu.

Uchunguzi uliofanyika katika eneo ambalo SARS ilianzia ulionesha kwamba asilimia 40 ya wafanyabiashara wa wanyama na asilimia 20 wachinja nyama waliugua SARS.

Covid-19

Kuibuka kwa virusi vipya vya corona vilivyopewa jina la Covid-19 ni matokeo ya uchunguzi ulioanza miaka ya 60. Awali ilidhaniwa virusi hivi ni sawa na SARS lakini uchunguzi wa kimaabara ukaonesha vina tofauti kidogo. Virusi vinavyosababisha Covid- 19 vina uwezo wa kusambaa haraka sana kuliko vile vya SARS.

Kama ilivyodokezwa hapo juu tangu 2003, kuna aina tano tofauti za virusi vya corona vinavyomshambulia mwanadamu. Aina tatu miongoni mwa hizo ni vurusi vinavyofanana zaidi na inaonesha asili yake ni moja.

Uvumi virusi vya corona

Kinyume na kile ambacho huenda utakuwa umekisikia, virusi vipya vya corona havikutengenezwa katika maabara ya kijeshi ya China au Marekani na wala Waalbania hawana kinga mwilini kuzuia maambukizi ya kirusi hicho.

Shehe mmoja hivi karibuni alisema kwamba kimsingi, kila kiumbe kimeumbwa na Mwenyezi Mungu na kwamba binadamu hana uwezo huo ingawa anaweza kukifanya kiumbe kilichoumbwa na Mungu tayari kuwa na tabia tofauti na zake za asili. Madai mengi yasiyokuwa na ukweli kuhusu virusi vya corona yamekuwa yakisambaa kwa siku za karibuni, kuanzia yale ya kushangaza, kipuuzi na mengine ya kushtua.

Kwa mfano mwana blogu wa YouTube, Dana Ashlie, aliweka video kuelezea kila alichodai kuwa ni sababu ya kweli kuhusu mlipuko wa virusi hivyo. Ashlie, ambaye ana mamia kwa maelfu ya wafuasi kwenye akaunti yake ya YouTube na Facebook, alidai kuwa Covid -19 ilizuka kwa sababu teknolojia ya mtandao wa simu wa 5G ilizinduliwa katika mji wa China wa Wuhan, ambao ndio kitovu cha mlipuko huo.

Huku ugonjwa huo wa Covid-19 ukitawala vichwa vya habari, haishangazi kuwa habari potofu za virusi vya corona zimeongezeka. Ndio maana Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limezindua tovuti maalumu ya kuondoa uwongo na madai yasiyo na ukweli kuhusu tiba za virusi vya corona na namna vidudu hivyo vinavyosambaa.

Kihistoria, milipuko ya majanga kila mara yaliandamana na usambazaji wa uvumi na nadharia za uwongo. Profesa Michael Butter, ambaye anafundisha katika Chuo Kikuu cha Tübingen, anasema nadharia za uongo au uzushi hudai kuwa kundi la watu linafanya kisiri njama ya kudhibiti na kuharibu taasisi, nchi au dunia nzima. Hata wakati wa janga la ebola kulikuwa na uvumi pia kuwa ugonjwa huo umetengenezwa na Marekani

TANZANIA inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Sita katika Mfumo wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi